TP Mazembe yavuliwa ubingwa CAFWCL, Asec, FAR Rabat kukipiga fainali
Muktasari:
- Mechi zote mbili za nusu fainali zimepigwa katika Uwanja wa Suez Canal jijini Ismailia, Misri na matokeo ya ushindi yamezipeleka timu hizo mbili moja kwa moja kwenye fainali ya mashindano hayo.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast imetinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake baada ya kulichapa chama la Watanzania, FC Masar, kwa bao 1-0 na nusu fainali nyingine FAR Rabat imeshinda kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya TP Mazembe baada ya suluhu hadi dakika 120 za mchezo huo kumalizika.
Mechi zote mbili za nusu fainali zimepigwa katika Uwanja wa Suez Canal jijini Ismailia, Misri na matokeo ya ushindi yamezipeleka timu hizo mbili moja kwa moja kwenye fainali ya mashindano hayo.
Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa licha ya chama la Watanzania, Hasnath Ubamba na Violeth Nickolaus, kupambana kupata bao kipindi cha kwanza. Ubamba ambaye alionekana kuwa mchezaji hatari walinzi wa Asec Mimosas walimkaba vilivyo kuhakikisha haleti madhara kwenye lango lao na hakuwa huru kwenye kutengeneza nafasi.
Dakika ya 73, mshambuliaji Essi Dagba wa Asec alifunga bao muhimu lililowapa ASEC uongozi na kuwahakikishia tiketi ya kuelekea fainali.
FC Masar walijitahidi kusaka bao la kusawazisha, lakini safu ya ulinzi ya ASEC ilionyesha uimara na utulivu chini presha na kuhakikisha Waivory Coast hao wanafika mwisho wakiwa mbele.
Mechi nyingine ilikuwa na upinzani mkali ni kati ya mabingwa watetezi TP Mazembe walioondolewa kwa mikwaju ya penalti 4-2 kufuatia sare ya bila kufungana na Asec Mimosas. AS Far Rabat walilipiza kisasi cha msimu uliopita ambao walifungwa bao 1-0 na Mazembe walionyakua ubingwa huo.
Katika mechi hiyo AS FAR walimiliki mpira, wakidhibiti kasi ya mchezo na kushambulia kwa kasi, huku Mazembe wakibaki imara, wenye nidhamu na hatari kwa mashambulizi ya kushtukiza. Licha ya umuhimu wa mechi hiyo ambayo ilionekana kama fainali safu zote mbili za ulinzi zilikuwa imara na makipa wakifanya kazi nzuri ya kuokoa mipira ya hatari.
Dakika 90 ziliisha bila timu yoyote kupata bao ukafanya mechi kuongezwa dakika 30 nyingine kisha kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Mikwaju ya penalti ilijaa drama na wasiwasi, lakini Zineb Erroudany alifunga penalti ya nne iliyotoa ushindi kwa AS FAR na kuwapeleka rasmi kwenye fainali.
Sasa fainali itapigwa Novemba 21 AS Far dhidi ya Asec Mimosas huku ile ya mshindi wa tatu ikiwakutanisha mabingwa watetezi Mazembe dhidi ya Masar.