Timu kibao zinamtaka Darwin Nunez
Muktasari:
- Nunez ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wanaodaiwa kutaka kuuzwa na Liverpool, kabla ya kutakiwa na vigogo hao alihusishwa pia na Napoli ambayo inadaiwa kujiondoa.
BARCELONA, AC Milan, Al Hilal na Al Nassr zote zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez, 26, katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Nunez ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wanaodaiwa kutaka kuuzwa na Liverpool, kabla ya kutakiwa na vigogo hao alihusishwa pia na Napoli ambayo inadaiwa kujiondoa.
Staa huyu amewaambia watu wake wa karibu kuwa anatamani sana kuendelea kusalia katika kikosi cha kwanza cha Liverpool kwa msimu ujao na ikishindikana ndio ataangalia ustaarabu mwingine lakini bado atajiunga na timu inayocheza moja kati ya ligi tano bora barani Ulaya.
Licha ya kuwekewa pesa na Waarabu staa huyu amesisitiza kuwa kipaumbele chake cha kwanza kwa sasa ni kuendelea kuonyesha makucha yake Ulaya. Liverpool imekuwa ikiripotiwa kuwa katika harakati za kutafuta mshambuliaji mpya licha ya uwepo wa Nunez kwa sababu Arne Slot hamwamini sana mchezaji huyu.
Katika msimu uliopita Nunez alicheza mechi 47 za michuano yote na kufunga mabao saba. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.
Cristhian Mosquera
DILI la beki wa Valencia, Cristhian Mosquera kwenda Arsenal linaonekana kuwa tayari limeshakamilika baada ya kuvuja kwa picha zake za utambulisho akiwa na jezi ya timu hiyo wakati wa utambulisho wa Noni Madueke aliyesajiliwa kutoka Chelsea.
Arsenal ilikuwa ikipambana vita dhidi ya timu mbalimbali barani Ulaya wakiwamo majirani zao, Tottenham lakini kwa kuvuja kwa picha hizo inaonekana kuwa imeishinda vita.
Mkataba wa Mosquera na Valencia unatarajiwa kumalizika mwakani.
Ilya Zabarnyi
TOTTENHAM imeulizia uwezekano wa kuipata saini ya beki wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ukraine, Ilya Zabarnyi, 22, katika dirisha hili.
Staa huyu amekuwa katika rada za vigogo wengi barani Ulaya na ili kumpata Spurs itatakiwa kushinda vita dhidi ya Paris Saint-Germain ambayo pia inahitaji saini yake. Timu nyingi zimevutiwa na kiwango ambacho beki huyu alikionyesha msimu uliopita katika Ligi Kuu England. Mkataba wake wa sasa unaisha mwaka 2029.
Bryan Mbeumo
KATIKA kuhakikisha inaziba mapengo, Brentford inaonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Celtic na timu ya taifa ya Japan, Daizen Maeda, 27, katika dirisha hili.
Timu hii yenye maskani yake jijini London inakabiliwa na kuondokewa wachezaji wake wengi katika dirisha hili ambao ni pamoja na Bryan Mbeumo anayenukia Manchester United na Yoane Wissa, 28, anayehusishwa na Newcastle.
Josh Sargent
NORWICH ipo karibu kumuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Marekani, Josh Sargent, 25, kwenda Wolfsburg kwa ada ya Pauni 21 milioni katika dirisha hili.
Josh alikuwa akihitajika pia na baadhi ya timu za Ligi Kuu England lakini hazikuwa tayari kutoa kiasi cha pesa ambacho Wolfsburg imekiweka mezani.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Victor Osimhen
DILI la mshambuliaji wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen kwenda Galatasaray liko karibu kukamilika baada ya timu zote mbili kufikia makubaliano katika masuala ya ada ya uhamisho.
Osimhen ambaye mkataba wake na Napoli unamalizika mwakani ataigharimu Galatarasau jumla ya Pauni 65 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Marcus Tavernier
WEST Ham imeongeza juhudi katika harakati za kumsajili kiungo wa Bournemouth, Marcus Tavernier, 26, katika dirisha hili. Benchi la ufundi linahitaji sana huduma ya Tavernier kwa ajili ya kuboresha eneo la kiungo ambalo lilikuwa na upungufu. Mkataba wa Tavernier unatarajiwa kumalizika 2028, msimu uliopita alicheza mechi 32 za michuano yote.
Pervis Estupinan
MANCHESTER United imefanya mazungumzo na wawakilishi wa beki wa Brighton na timu ya taifa ya Ecuador, Pervis Estupinan, 27, kujua kama iko tayari kumuuza katika dirisha hili.
Mbali ya Man United, Estupinan pia anawindwa na baadhi ya timu za Saudi Arabia zinazomhitaji katika dirisha hili.
Mataba wa Estupinan unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 36 za michuano yote.