Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Timu 48, mechi 104: Safari ya Kombe la Dunia 2026 kuaanza leo

Muktasari:

  • Mchezo huo wa leo ni mwanzo wa uhondo na msisimko wa tukio hilo kubwa la soka duniani ambalo litafikia tamati Julai 19 mwaka huu kwa mchezo wa fainali utakaofanyika katika Uwanja wa MetLife, New York, Marekani.

MEXICO CITY, MEXICO. Pazia la Fainali za Kombe la Dunia 2026 linafunguliwa rasmi leo kwa mchezo baina ya wenyeji Mexico dhidi ya Afrika Kusini utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azteca, kuanzia saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Mchezo huo wa leo ni mwanzo wa uhondo na msisimko wa tukio hilo kubwa la soka duniani ambalo litafikia tamati Julai 19 mwaka huu kwa mchezo wa fainali utakaofanyika katika Uwanja wa MetLife, New York, Marekani.

Ni ufunguzi unaoleta ukumbusho wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 ambazo zilifanyika Afrika Kusini ambazo mechi yake ya kufungua mashindano ilizikutanisha timu hizi mbili za leo na ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mchezo wa leo utachezeshwa na Refa Willy Sampaio kutoka Brazil ambaye atasaidiwa na Wabrazil wenzake, Bruno Pires na Bruno Boschilia huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Gabriel Benitez wa Paraguay.

Jumla ya timu za taifa 48 ndizo zinashiriki mashindano hayo, zikigawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja.


MVUTO WA VIWANJA

Mechi 104 za Kombe la Dunia mwaka huu zitachezwa katika viwanja 16 vilivyopo katika majiji tofauti kwenye nchi hizo.

Kati ya hivyo, viwanja 11 vipo Marekani, vitatu vipo Mexico na Canada kuna viwanja viwili.

Viwanja vya Marekani vitakavyotumika ni Dallas, MetLife, Atlanta, Arrowhead, Houston, San Francisco Bay, SoFi, Lincoln Financial Field, Lumen, Gillette na Hard Rock.

Nchini Mexico, viwanja vitakavyotumika ni Azteca, Monterrey na Guadalajara huku Canada wakiwa na viwanja vya Vancouver na Toronto.


MPIRA GUMZO

Mpira utakaotumikwa kwa Kombe la Dunia mwaka huu unaitwa TRIONDA.

Maana ya jina hilo ni kuonyesha ushirikiano wa mataifa matatu ambayo ni Marekani, Canada na Mexico yanayoandaa mashindano hayo.

Mpira huo umepambwa kwa rangi nyekundu, bluu na kijani pamoja na alama maalumu zinazowakilisha nchi hizo tatu na una sensa maalumu yenye uzito wa gramu 14 iliyowekwa ndani.

Sensa hiyo ina uwezo wa kurekodi kila mguso wa mchezaji, kasi ya mpira, mzunguko wake na mwelekeo wake kwa usahihi.

Taarifa hizo hutumwa na kuunganishwa na mfumo wa VAR ili kufanya maamuzi ya haraka na sahihi zaidi katika matukio ya kuotea, mipira ya kushika, mipira iliyovuka mstari wa goli pamoja na matukio mengine yenye utata.

Unatumia betri ndogo inayoweza kuchajiwa na ikadumu na chaji kwa muda wa saa sita.


TIMU KUOGA NOTI

Bingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu anapata kitita cha Dola 50 milioni (Sh130 bilioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Mshindi wa pili ataondoka na Dola 33 milioni (Sh86 bilioni), mshindi wa tatu atapata Dola 29 milioni (Sh76 bilioni) na mshindi wa nne ataondoka na kitita cha Dola 27 milioni (Sh70 bilioni).

Ni mashindano ambayo yanaihakikishia kila timu shiriki kupata kiasi kikubwa cha fedha hata kama itaishia hatua ya makundi.

Kwa kuanzia, FIFA linatoa kiasi cha Dola 1.5 milioni (Sh3.9 bilioni) kwa kila timu kwa ajili ya maandalizi.

Timu inayoishia hatua ya makundi, ina uhakika wa kuvuna kiasi cha Dola 9 milioni (Sh23 bilioni) na inayokwamia katika hatua ya 32 bora inapata kiasi cha Dola 11 milioni (Sh29 bilioni).

Kwa itakayoishia hatua ya 16 bora inapata kitita cha Dola 15 milioni (Sh39 bilioni) na ambayo shughuli yake itaishia robo fainali itapata kiasi cha Dola 19 milioni (Sh49 bilioni).

WACHEZAJI MKAO WA KULA

Kila timu imewasilisha majina ya wachezaji 26 na hivyo kufanya jumla ya wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo kuwa 1,248.

Kutoa wachezaji 16 wanaoshiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, kunaifanya Man City iwe klabu iliyotoa idadi kubwa ya wachezaji kwenye mashindano hayo.

Kipa wa Scotland mwenye umri wa miaka 43, Craig Gordon, ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi katika Kombe la Dunia mwaka huu huku mchezaji mwenye umri mdogo akiwa ni Gilbert Mora wa Mexico.

Cesar Yanis wa Panama, ndiye mchezaji mfupi zaidi akiwa na kimo cha mita 1.60 huku mchezaji mwenye kimo kirefu zaidi akiwa ni Kipa wa Austria, Florian Wiegele, mwenye kimo cha mita 2.05.