Tacko Fall arejea NBA
Muktasari:
- Mchezaji huyo mwenye umbo kubwa kutoka Senegal ambaye sasa yupo katika miaka ya mwanzoni ya 30, atapata fursa mpya ya kuthibitisha kwamba bado anastahili kucheza katika ligi hiyo na kupigania nafasi ya kudumu katika kikosi cha timu wakati wa msimu wa kawaida kupitia Philadelphia 76ers iliyompa nafasi.
PHILADELPHIA, MAREKANI: NYOTA wa kikapu Tacko Fall amerejea katika Ligi ya Kikapu Marekani kwa ajili ya msimu ujao, huku akipewa nafasi nyingine.
Mchezaji huyo mwenye umbo kubwa kutoka Senegal ambaye sasa yupo katika miaka ya mwanzoni ya 30, atapata fursa mpya ya kuthibitisha kwamba bado anastahili kucheza katika ligi hiyo na kupigania nafasi ya kudumu katika kikosi cha timu wakati wa msimu wa kawaida kupitia Philadelphia 76ers iliyompa nafasi.
Philadelphia 76ers, ambayo ni miongoni mwa timu zinazofuatiliwa kwa karibu kuelekea msimu wa NBA wa 2026/27, imemwita Fall kwenye kambi ya mazoezi ya maandalizi ya msimu ujao.
Baada ya LeBron James sasa kuwa Philadelphia, 76ers ghafla imekuwa miongoni mwa timu zinazotajwa kuwa zina nafasi kubwa ya kushinda ubingwa, siyo katika Kanda ya Mashariki pekee bali katika ligi nzima.
Ukiongeza Jaylen Brown pamoja na nyota wanaorejea kama Joel Embiid na Tyrese Maxey, na kipaji kinachochipukia kutoka Bahamas, V.J. Edgecombe, Philadelphia ina kikosi chenye nguvu kubwa.
Fall ametumia miaka minne iliyopita akicheza nje ya Marekani, hasa barani Asia ambako alikipiga vipindi viwili nchini China, akiwa Urumqi na Nanjing, huku pia akipita Puerto Rico na New Zealand. Mara ya mwisho kuonekana katika tukio linalohusiana na NBA ilikuwa Februari, mwaka huu wakati wa All-Star Weekend aliposhiriki katika mchezo wa watu mashuhuri maarufu kama Celebrity Game.
Na sasa atajaribu kutumia urefu wake wa futi 7 na inchi 6 ili kujihakikishia nafasi miongoni mwa wachezaji bora wa ligi.
Timu hiyo pia imesaini mikataba ya muda mfupi kwa ajili ya maandalizi ya msimu na mshambuliaji, Saint Thomas, pamoja na Jameer Nelson Jr ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mchezaji wa nafasi ya point guard katika NBA, Jameer Nelson.
Miongoni mwa wachezaji warefu zaidi katika historia ya NBA ni Elhadji Tacko Sereigne Diop Fall aliyezaliwa Dakar 1995 sawa na Gheorghe Mureșan, Manute Bol, Shawn Bradley pamoja na Yao Ming waliokuwa warefu zaidi.