Dar City yaifanyizia Stein Warriors
Muktasari:
- Mchezo huo, uliovunja rekodi ya kuwa na watazamaji wengi, ulifanyika katika Uwanja wa Don Bosco, Upanga, Dar es Salaam.
DAR City imeinyamazisha Stein Warriors katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), baada ya kuifunga kwa pointi 67-54.
Mchezo huo, uliovunja rekodi ya kuwa na watazamaji wengi, ulifanyika katika Uwanja wa Don Bosco, Upanga, Dar es Salaam.
Tambo za Stein Warriors zilianza kabla ya mchezo huo, baada ya timu hiyo kujigamba kuwa ingekuwa ya kwanza kuifunga Dar City katika msimu huu.
Kutokana na hali hiyo, kocha wa Dar City, Mohamed Mbwana, aliamua kushusha kikosi chake cha kwanza, kilichowajumuisha Elijah Mukelabi, raia wa Zambia, Chelkh Diallo wa Senegal na Nkosiath Sibanyoni wa Afrika Kusini, huku wakishirikiana na wazawa Ally Abdallah, Amin Mkosa na Jonas Mushi.
Kwa upande wa Stein Warriors, kikosi hicho kilijumuisha Daniel Kola, Moise Bukengu, Jimmy Brown, Tyrone Brown, Tyrone Edward na Ally Mohamed.
Hata hivyo, Stein Warriors itabidi ijilaumu yenyewe kwa kupoteza mchezo huo kutokana na benchi la ufundi kushindwa kusimamia vizuri muda wa kumpumzisha mchezaji na kumrejesha uwanjani.
Dar City ilitumia udhaifu huo kupata nafasi ya kufunga pointi na kuongeza pengo dhidi ya wapinzani wao.
Katika mchezo huo, Moise Bukengu wa Stein Warriors alifunga pointi 19, huku Chelkh Diallo wa Dar City akiongoza upande wa timu yake kwa kufunga pointi 16.
Mmoja wa mashabiki wakubwa wa Dar City, John Joseph, amesema mchezo dhidi ya Stein Warriors umewapa ladha na tathmini ya ugumu wa michezo wanayotarajia kukutana nayo katika hatua ya mchujo (playoff).
Joseph aliiambia Mwanaspoti kuwa ushindi huo ulikuwa muhimu kwa Dar City katika mchezo wao wa mwisho wa mzunguko, huku timu hiyo ikimaliza hatua hiyo bila kupoteza mchezo wowote katika michezo 15.
Ameongeza kuwa ushindani walioupata dhidi ya Stein Warriors umewapa picha ya namna hatua ya playoff itakavyokuwa, huku Dar City ikielekea hatua hiyo ikiwa na rekodi nzuri na morali kubwa baada ya kumaliza mzunguko bila kufungwa.
Dar City imemaliza mzunguko huo ikiwa na pointi 30, ikifuatiwa na Stein Warriors yenye pointi 28, Pazi pointi 26, Vijana ‘City Bulls’ pointi 25, UDSM Outsiders 25, ABC 24, Mlimani BC 23 na JKT 22.
Katika hatua ya robo fainali (playoff), Dar City itacheza dhidi ya JKT, Stein Warriors itakutana na Mlimani BC, Pazi itacheza dhidi ya ABC, huku Vijana ‘City Bulls’ wakikabiliana na UDSM Outsiders.
Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), Shabani Mahobonya, amesema ratiba ya mechi za hatua ya robo fainali ya mchujo (playoff) itatangazwa hivi karibuni.