Chipukizi Amen Thompson avuna milioni NBA
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Shams Charania wa ESPN, mkataba huo pia una kipengele cha asilimia 10 ya bonasi endapo mchezaji huyo atahamishwa, na utamfanya Thompson kuendelea kuwa sehemu ya Rockets hadi mwaka 2032.
HOUSTON, MAREKANI: MVUA ya fedha inazidi kumiminika kwenye Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA), huku Amen Thompson akiwa nyota mpya wa kizazi cha wachezaji chipukizi kuvuka kiwango cha kuwa milionea wa mamilioni ya dola baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Dola 208 milioni na Houston Rockets.
Kwa mujibu wa Shams Charania wa ESPN, mkataba huo pia una kipengele cha asilimia 10 ya bonasi endapo mchezaji huyo atahamishwa, na utamfanya Thompson kuendelea kuwa sehemu ya Rockets hadi mwaka 2032.
Akiwa na miaka 23, Thompson amehalalisha thamani hiyo kutokana na kupanda kwake kwa kasi tangu alipochaguliwa na Rockets kama mchezaji wa nne kwa jumla katika NBA Draft ya mwaka 2023. Msimu uliopita aliweka rekodi bora zaidi za maisha yake kwa wastani wa pointi 18.3, pasi za mwisho 5.3 na kuiba mipira 1.5 kwa mchezo.
Pia, alikuwa mchezaji aliyecheza dakika nyingi zaidi NBA, huku akimaliza miongoni mwa vinara wa ligi kwa kuiba mipira na kurejesha mipira iliyopotea.
SI SHOOTING GUARD PEKEE
Uwezo wa Thompson hauishii kwenye nafasi moja pekee.
Kutokuwepo kwa Fred VanVleet kulimfanya acheze zaidi kama point guard, lakini Thompson ana uwezo wa kucheza nafasi zote za pembeni na hata kushuka kucheza karibu na paint.
Msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji tisa pekee waliomaliza msimu wakiwa na wastani wa angalau pointi 18, rebounds saba na assists tano kwa mchezo.
Alikuwa sambamba na mastaa wakubwa kama Nikola Jokic, Luka Doncic, Giannis Antetokounmpo na Jayson Tatum.
ROCKETS YAFUNGA KIKOSI CHA VIJANA
Mkataba huo unaifanya Rockets kuendelea kuwalinda mastaa wake vijana kwa muda mrefu.
Kabla ya Thompson, klabu hiyo tayari ilikuwa imewaongezea mikataba Alperen Sengun, Jabari Smith Jr. na Tari Eason, huku uwepo wa Kevin Durant ukiipa timu hiyo uzoefu wa nyota mkubwa.
Thompson pia amekuwa mchezaji wa pili kutoka kundi la Draft ya 2023 kusaini mkataba mpya wa muda mrefu akiwa bado kwenye kipindi chake cha mkataba wa rookie, baada ya Victor Wembanyama.
Huenda mvua ya mamilioni ikaendelea kunyesha kwani Brandon Miller, Ausar Thompson, Keyonte George, Cason Wallace, Jaime Jaquez Jr na Brandin Podziemski ni miongoni mwa wachezaji wa kizazi hicho wanaotajwa kuwa kwenye foleni ya kusaini mikataba mikubwa hivi karibuni.