Kiungo Simba afichua siri, aitaja Mighty Wanderers
SIMBA imerejea nchini jana usiku na kesho itaanza maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi sasa kiungo wake mmoja amefunguka kwamba mechi hiyo itakuwa kwenye uamuzi wao zaidi.
Kiungo aliyesema hayo ni Ibraheem Jabaar ameliambia Mwanaspoti kuwa baada ya ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya timu hiyo, sio kwamba kikosi hicho kimemaliza kazi na kwamba watakuwa na dakika zingine 90 za kuthibitisha ubora wao.
Jabaar amesema mchezo wa marudiano ambao utapigwa Septemba 13, Uwanja wa Uhuru utakuwa ni maalumu kwa wao wachezaji kuwafurahisha mashabiki wao kwa kutafuta ushindi mkubwa zaidi lakini pia kucheza soka la kuvutia.
“Tulikuwa ugenini kwenye mchezo uliopita, tulipambana tupate pointi tatu, tukafanikiwa, hatukucheza vizuri sana kama ambavyo tunataka lakini kitu muhimu tulipata ushindi tukiwa ugenini, bado hatujamaliza hii mechi,” amesema Jabaar.
“Tunaporudi nyumbani jukumu la kuamua huu mchezo linabaki kwetu kama wachezaji, tunatakiwa kucheza vizuri na kuthibitisha ubora wetu tena kwa kushinda nyumbani, tutakuwa mbele ya mashabiki wetu wana nafasi kubwa ya kufurahia kile ambacho tutakifanya.”
Aidha Jabaar raia wa Nigeria, ameongeza kwamba kadiri ya muda unavyosogea kikosi chao kinazidi kuimarika huku akivutiwa na ubora wa wachezaji wenzake katika kikosi hicho.
Amesema licha ya kushindwa kuumiliki mchezo katika mechi dhidi ya Mighty Wanderers bado walifanikiwa kupata bao huku ukuta wao ukitoka bila kuruhusu bao.
“Sina wasiwasi na namna timu inavyocheza, kadiri ya muda unavyosogea tunazidi kuimarika kutoka mechi moja kwenda nyingine, hii ni nzuri, ushindani kwetu wachezaji na ushirikiano ni mkubwa sana unavutia.
“Unaweza kuangalia juzi hatukucheza sana kwa maana ya kumiliki mchezo lakini tulifanikiwa kupata goli ambalo lilitofautisha faida kati yetu na wapinzani, ukiangalia upande wa ulinzi nako hatukuruhusu bao, hii ni kubwa na muhimu.”
Tangu kusajiliwa Simba akitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini, Jabaar amefanikiwa kuonyesha ubora mkubwa kwenye eneo la kiungo la Wekundu hao.