Prime
Tatizo Yanga latajwa, wachezaji waonywa
YANGA imerejea nchini ikitokea Botswana na leo itaanza ratiba ya mazoezi kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Gaborone United kufuatia sare ya 1-1 ugenini, lakini kocha wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi ameshtukia kitu kuhusu kikosi chake akitaja tatizo lilipo.
Yanga kwenye mechi sita za mashindano msimu huu 2026-2027, imekuwa bora ikifunga mabao 16, ikiwemo michezo mitano ya Ligi Kuu Bara na mmoja wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha Manqoba Mngqithi ameshtukia kitu akiona bado kuna huduma zinahitajika kwa washambuliaji wake.
Manqoba amegundua kwamba licha ya kwamba washambuliaji wake wamekuwa wakipoteza nafasi, lakini bado hawajaweza kucheza kwa ubora sambamba na viungo wa timu hiyo katika kuwapa mipira ya mwisho.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amesema benchi lake la ufundi bado linaendelea kuboresha muunganiko huo ambapo anatamani kuona kikosi hicho kinakuwa na njia nyingi za kutengeneza nafasi kuanzia katikati ya uwanja mpaka pembeni kwa mawinga.
“Hatupo sehemu mbaya sana, ukitazama tunatengeneza nafasi lakini tunatakiwa kuongeza njaa ya kuzitumia, nakubali kwamba tunapoteza naadhi ya nafasi lakini bado tunatakiwa kuwa bora kwenye kutengeneza nafasi zaidi ya tunachofanya sasa,” amesema Manqoba.
“Ukiangalia kuna chan gamoto bado kwenye utengenezwaji wa mashambulizi ya pembeni, bado krosi nyingi zinakuwa sio muafaka sana na zingine zinapotea, hili linatakiwa kurekebishwa tunaendelea kulifanyia kazi.
“Ukiacha pembeni, tumeanza kutengeneza nafasi kutoka katikati ya uwanja lakini bado tunatakiwa kuongeza ubora zaidi, bahati mbaya kuna wachezaji bado tunawajenga ambao wanaweza kutupa kitu zaidi eneo hilo.”
Hata hivyo, Manqoba amesema kazi hiyo ataendelea taratibu kuijenga, lakini kwasasa kitu muhimu ni kujipanga kuingia kwenye mchezo ujao dhidi ya Gaborone na kasi kubwa ya kuwalazimisha wapinzani wao kufanya makosa.
“Hakuna kitu kingine kinahitajika hapa zaidi ya ushindi, kwangu mimi kitu bora kutoka kwenye mchezo uliopita ni kupata bao la ugenini lakini wakati tunarudi nyumbani tunatakiwa kujipanga kuwapa wakati mgumu wapinzani wetu, tunatakiwa kuwalazimisha kufanya makosa, hilo tunaliweza.
“Jambo zuri ni kwamba hatuna majeruhi wa muda mrefu, kidogo Ngoma (Fredy) ambaye alipata maumivu kwenye mechi za ligi lakini wengine wako sawa, tutajipanga kushinda, tunataka kufika mbali.”
Jumamosi Septemba 12, 2026, Yanga itaikaribisha Gaborone United kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza baada ya ile ya kwanza ugenini kutoka sare ya bao 1-1.
Yanga inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare isiyo na mabao ili kufuzu hatua ya pili ambapo itakwenda kukutana na mshindi kati ya CFFA ya Madagascar na Lijabatho ya Lesotho.