Steven Gerarrd na Alexandra, ujana unaondoka bila kashfa
Muktasari:
- Mke wake Alexandra, 43, ambaye ni mwanamitindo na mwandishi, alikuwa ni kati ya wake au wapenzi wa wachezaji (WAGs) ambao waliangaziwa sana na vyombo vya habari kwa wakati huo.
NAHODHA wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard, 45, ni miongoni mwa wachezaji waliokuwepo katika kizazi cha dhahabu cha timu ya taifa ya England, jambo lilofanya maisha yake binafsi kuwa na mvuto zaidi.
Mke wake Alexandra, 43, ambaye ni mwanamitindo na mwandishi, alikuwa ni kati ya wake au wapenzi wa wachezaji (WAGs) ambao waliangaziwa sana na vyombo vya habari kwa wakati huo.
Alipata umaarufu mkubwa wakati michuano ya Kombe la Dunia la FIFA 2006 nchini Ujerumani ambapo yeye na warembo wengine kama Victoria Beckham na Coleen Rooney, waliwasindikiza wenza wao.
Kutokana na kuibuka kwa kizazi hicho cha dhahabu, wakati huo kulikuwa na hamasa kubwa kwa mashabiki waliotaka kujua kuhusu maisha yao binafsi hasa upande wa mahusiano, ndoa na hata familia.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2002, kwa mujibu wa Alexandra hakukubali ombi la Gerrard kwa haraka, alitaka kumzungusha kidogo kama wanavyofanya warembo wengi.
"Nilimkataa mwanzoni lakini ninafurahi nilifanya hivyo kwa sababu alikuwa amezoea wasichana wote kumkubalia," alisema na kuongeza:
"Nadhani kwa sababu sikuonekana kuwa na hamu sana ya kuwa naye kama warembo wengine, ilimfanya anipende zaidi."
Hata hivyo, kabla ya uhusiano wake na Gerrard, Alexandra alikuwa akitoka kimapenzi na mfanyabiashara, Tony Richardson, huku mchezaji huyo akiwa kwenye uhusiano na mwigizaji na mwanamitindo, Jennifer Ellison kutokea England pia.
Wakati fulani mnamo 2002, kuliibuka madai kuwa Alexandra na Jennifer waliwahi kubadilishana wapenzi, jambo ambalo The Guardian iliandika kuwa bado lina mjadala mzito kuhusu nani hasa alimchukua mpenzi wa mwenzake!.
Kufikia Juni 16, 2007, ndipo Gerrard na Alexandra walifunga katika hoteli ya kifahari ya Cliveden House huko Buckinghamshire. Kitu cha kipekee ni kwamba siku hiyo hiyo pia wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya England, Gary Neville na Michael Carrick, nao walifunga ndoa zao.
Awali Cliveden ilikuwa ikitumiwa na Chuo Kikuu cha Stanford ila kwa sasa jumba hilo linaendeshwa kama hoteli yenye hadhi ya nyota tano.
Gerrard na Alexandra walifunga ndoa wakiwa tayari wana watoto wawili, Lily-Ella (2004) na Lexie (2006), na baadaye wakaja kujaliwa wengine wawili ambao ni Lourdes (2011) na Lio (2017).
Hata hivyo, maisha yao hayakukosa changamoto, mathalani Desemba 2007, wakati Gerrard akiwa safarini pamoja na kikosi cha Liverpool, nyumba yao ilivamiwa na majambazi. Inadaiwa majambazi hao walikuwa wakitafuta saa yenye thamani ya Pauni 10,000 ambayo Alexandra alikuwa amenunua kama zawadi ya Krismasi kwa Gerrard.
Mwaka 2015, baada ya Gerrard kuondoka Liverpool, familia hiyo ilihamia nchini Marekani ambapo mchezaji huyo alijiunga na LA Galaxy inayoshiriki ligi ya MLS. Waliishi Los Angeles, California katika eneo la kishua lijulikano kama Beverly Hills.
Nyumba yao yenye vyumba sita vya kulala, thamani yake ilikuwa Pauni 18 milioni na walikuwa wakilipa kodi ya Pauni 35,000 kwa mwezi, huku wakati huo Gerrard alikuwa akilipwa takribani Pauni 74,000 kwa wiki.
Je, Alexandra ni nani hasa?, mrembo huyo alizaliwa Septemba 23, 1982 huko Aintree, Merseyside, na kukulia Maghull, mjio uliopo kaskazini mwa Liverpool na magharibi mwa Kirkby. Kabla hajawa maarufu kwenye vyombo vya habari, alikuwa akifanya shughuli za urembo lakini maisha yake yalibadilika haraka baada ya kuanza kuhusishwa na Gerrard.
Katika kipindi hicho cha mwanzoni, Alexandra alianza kuonekana mara kwa mara kwenye magazeti na televisheni kutokana na mvuto wake kama mwanamtindo, na maisha yake ya kifahari. Kila wiki alipewa nafasi ya kuandika safu mbalimbali za mitindo katika magazeti ya Daily Mirror na baadaye OK! Magazine kuanzia mwaka 2009 hadi Januari 2013.
Safu yake maarufu ilijulikana kwa jina la “Go Shopping With Alex Curran”, ambapo alikuwa akizungumzia masuala ya mitindo, maisha ya mastaa na bidhaa mbalimbali za kifahari. Mbali na uandishi na umaarufu katika vyombo vya habari, pia alifanya biashara zake binafsi. Mnamo Oktoba 2007, alizindua manukato yaliyoitwa “Alex”, ambayo yalifanikiwa kuwa miongoni mwa bidhaa zilizouzwa sana kwa mwaka huo.
Baadaye mwaka 2010, aliingia kwenye ulimwengu wa ubunifu wa mavazi kwa kuzindua “Forever Unique by Alex Gerrard Collection”. Mafanikio ya mradi huo wa kwanza yalimfanya azindue mwingine mwaka 2011. Pia mwaka 2013 alitangazwa kuwa balozi rasmi wa Lipsy VIP Collection.
Hadi leo, Gerrard na Alexandra wanaendelea kutajwa kama moja ya familia maarufu na zilizodumu zaidi katika ulimwengu wa soka la England. Umaarufu wao umetokana si tu na mafanikio ya Gerrard uwanjani, bali pia maisha yao ya kifamilia, biashara na ushawishi mkubwa waliokuwa nao kwenye vyombo vya habari kwa zaidi ya miongo miwili.