Fenerbahce yatia maguu kwa Rashford
Muktasari:
- Rashford ambaye msimu uliopita aling'ara akiwa na Barcelona kwa mkopo, kwa sasa amerejea Manchester United akisikilizia ofa kutoka timu kubwa za Ulaya baada ya Barca kugoma kumnunua kwa zaidi ya Pauni 35 milioni ambazo waajiri wake wamemwekea kwenye ofa kwa klabu inayomtaka.
FENERBAHCE ipo tayari kutumia fedha nyingi kumshawishi mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, mwenye umri wa miaka 28, kuhamia Uturuki msimu huu wa kiangazi.
Rashford ambaye msimu uliopita aling'ara akiwa na Barcelona kwa mkopo, kwa sasa amerejea Manchester United akisikilizia ofa kutoka timu kubwa za Ulaya baada ya Barca kugoma kumnunua kwa zaidi ya Pauni 35 milioni ambazo waajiri wake wamemwekea kwenye ofa kwa klabu inayomtaka.
Mchezaji huyo ambaye ni zao la akademi ya Manchester United ameendelea kushawishiwa na timu mbalimbali kujiunga nazo kutokana na kiwango alichoonyesha alipokuwa Barcelona, ambapo Bayern Munich na Atletico Madrid ni miongoni mwa zile zilizoonyesha nia ya kumtaka awali, ingawa hazijarudi tena.
Hata hivyo, Manchester United imeendelea kuonyesha nia ya kuendelea kumtumia kwa msimu ujao, ambapo kocha mpya, Michael Carrick ameshazungumza na wawakilishi wa mchezaji huyo kuwaelezea kuwa yupo kwenye mipango yake na kwamba, hata akibaki hakuna kitakachoharibika.
Yan Diomande
WINGA wa kimataifa wa Ivory Coast, Yan Diomande, mwenye umri wa miaka 19, hatahudhuria kambi ya maandalizi ya msimu mpya ya RB Leipzig, huku klabu hiyo ikisisitiza kulipwa ada ya uhamisho ya Pauni 111 milioni katika mazungumzo na Real Madrid ambaye imeonyesha nia ya kumsajili. Diomande ameendelea kuwa kipaumbele cha Madrid kwa ajili ya msimu ujao ambapo kikosi hicho kinapambana kurejesha ubingwa wa LaLiga na Ulaya.
Bruno Guimaraes
ARSENAL imeanza upya mazungumzo na Newcastle United kuhusu uhamisho wa kiungo wa kimataifa wa Brazil, Bruno Guimaraes, mwenye umri wa miaka 28. Arsenal inatarajia kumsajili kwa ada ya kati ya Pauni 70 na 80 milioni. Taarifa za jana zilionyesha kwamba mchezaji huyo alikuwa katika hatua za mwishomwisho kutua Emirates, ingawa pia kulikuwa na ugumu katika kukamilisha dili hilo kwa sababu za kifedha.
Ferran Torres
PSG imeongeza kasi katika harakati za kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Ferran Torres, mwenye umri wa miaka 26 ambaye taarifa za ndani zinadai kwamba ameshaonyesha dhamira ya kuondoka kikosini kwenda kusaka changamoto sehemu nyingine. Torres anataka kuondoka ili akapate mahali atakakokuwa anaanza kikosini.
Cody Gakpo
LIVERPOOL haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi, Cody Gakpo, mwenye umri wa miaka 27, licha ya Tottenham Hotspur kuonyesha nia ya kumsajili. Gakpo ameelezea nia ya kubaki Liverpool, lakini klabu yake imefungua milango kusikiliza ofa kutoka timu mbalimbali.
Wilson Isidor
SUNDELAND haitamuuza mshambuliaji wa Haiti, Wilson Isidor, mwenye umri wa miaka 25, msimu huu wa kiangazi licha ya kuvutiwa na klabu kadhaa hasa West Ham United. Isidor anataka kuondoka Sundeland ili aende timu atakayopata namba katika kikosi cha kwanza baada ya kuingia mara chache chache kikosini msimu uliopita.
Marc-Andre ter Stegen
KIPA wa Barcelona na timu ya taifa ya Ujerumani, Marc-Andre ter Stegen, mwenye umri wa miaka 34, anadaiwa kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Uholanzi, Ajax, kwa mkopo wa mwaka mmoja. Msimu uliopita Stegen alicheza kwa mkopo katika kikosi cha Girona baada ya kuondoka Barca. Hata hivyo, kwa sasa amedhamiria kuondoka jumla, ingawa Girona pia inataka abaki.
Marc Bernal
ASTON Villa inapanga kutoa ofa ya Pauni 30 milioni kwa ajili ya usajili wa kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Marc Bernal, mwenye umri wa miaka 19. Hata hivyo, mchezaji huyo anadaiwa kuuambia uongozi wa Barca usimuuze ili abakie kupigania namba katika kikosi cha kwanza msimu ujao.
Endrick
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Endrick, 20, ameanza kuvutia macho ya AS Roma katika dirisha hili la usajili wa kiangazi, ingawa Lyon pia inataka kumbakiza Ufaransa. Wawakilishi wa mchezaji huyo wanataka kumbakiza Real Madrid ambako alianza kutengeneza jina kabla ya kutimkia Lyon kwa mkopo msimu uliopita.
Mykhailo Mudryk
KLABU iliyopanda Ligi Kuu England msimu uliopita, Coventry City ni miongoni mwa timu tatu za Ligi Kuu England zinazomtaka winga wa Chelsea na timu ya taifa ya Ukraine, Mykhailo Mudryk, mwenye umri wa miaka 25. Mchezaji huyo alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na tuhuma za matumizi ya dawa zilizopigwa marufu michezoni, lakini hivi karibuni alishinda kesi.