Man United yaingia anga za Simba
Muktasari:
- Julai mwaka jana, Simba iliingia kwenye historia baada ya kusaini mkataba wa udhamini wenye thamani ya Sh20 bilioni na Betway kwa kipindi cha miaka mitatu, hatua iliyoiweka miongoni mwa klabu zenye mikataba mikubwa ya udhamini Afrika Mashariki.
Manchester United imefuata nyayo za Simba SC baada ya kutangaza rasmi kampuni ya Betway kuwa mdhamini mpya wa jezi za mazoezi za klabu hiyo, kampuni ambayo tayari ni mshirika mkuu wa miamba ya Msimbazi.
Julai mwaka jana, Simba iliingia kwenye historia baada ya kusaini mkataba wa udhamini wenye thamani ya Sh20 bilioni na Betway kwa kipindi cha miaka mitatu, hatua iliyoiweka miongoni mwa klabu zenye mikataba mikubwa ya udhamini Afrika Mashariki.
Sasa, Betway imepanua ushirikiano wake katika soka kwa kufunga mkataba mwingine mkubwa na Manchester United, ambao unakadiriwa kuingiza zaidi ya Pauni milioni 20 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, makubaliano hayo yanatajwa kuwa mkataba mkubwa zaidi kuwahi kufungwa duniani unaohusu udhamini wa jezi za mazoezi au nembo kwenye mikono ya jezi za kuchezea.
United ilikuwa haina mdhamini wa jezi za mazoezi za timu za wanaume na wanawake tangu mkataba wake na Tezos ulipomalizika Juni 2025.
Taarifa zinaeleza kuwa viongozi wa United walichagua kusubiri kwa makusudi kabla ya kuingia kwenye mkataba mpya, wakiamini thamani ya klabu ingeongezeka baada ya kufuzu tena Ligi ya Mabingwa Ulaya chini ya kocha Michael Carrick.
Mkataba huo ni sehemu ya mkakati wa United wa kuongeza mapato ya kibiashara na kuimarisha nguvu yake kifedha kuelekea msimu wa 2026/27.
Kwa namna hiyo, Betway sasa imeendelea kujitanua kwenye soka la kimataifa kwa kuwa mshirika wa klabu mbili zenye mashabiki wengi, Simba nchini Tanzania na Manchester United nchini England, jambo linaloonyesha ukubwa wa uwekezaji wa kampuni hiyo katika mchezo wa soka.