Soko lao limeshuka baada ya kutua Saudia
Muktasari:
- Mchezaji anayeweza kushuka thamani yake sokoni kwa sababu nyingi tofauti. Inaweza kuwa kiwango kushuka, majeruhi au umri kuwa mkubwa, kwa sababu soko la wachezaji na thamani zao zinapanda na kushuka kwa mara kwa mara.
RIYADH, SAUDI ARABIA: BAADHI ya masupastaa wa soka wenye majina makubwa kwenye mchezo huo ni miongoni mwa wakali 10 wanaokipiga kwenye mikikimikiki ya Saudi Pro League ambao thamani zao sokoni zimeshuka kwa kiwango kikubwa sana kwa mwaka huu wa 2024 kwa mujibu wa Transfermarkt.
Mchezaji anayeweza kushuka thamani yake sokoni kwa sababu nyingi tofauti. Inaweza kuwa kiwango kushuka, majeruhi au umri kuwa mkubwa, kwa sababu soko la wachezaji na thamani zao zinapanda na kushuka kwa mara kwa mara.
10. Yannick Carrasco (-Euro 10 milioni)
Baada ya kutoka China na kurudi kukipiga Atletico Madrid na kuisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa La Liga mwaka 2021, Yannick Carrasco aliachana tena na maisha ya Ulaya mwaka 2023 na kwenda kujiunga na Al-Shabab. Kiungo huyo amekuwa na maisha yenye mapito mengi huko Saudi Arabia, ikiwamo kushindwa kuonyesha kiwango bora kwenye soka la kimataifa huku jambo hilo likitibua thamani yake sokoni na kushuka kwa Euro 10 milioni.
9. Sadio Mane (-Euro 11 mil)
Sadio Mane kiwango chake kimeshuka tangu alipoondoka Liverpool mwaka 2022 na kushtusha watu wengi. Msenegali huyo alishinda namba mbili kwenye Ballon d’Or mwaka huo, lakini alikosa fainali za Kombe la Dunia za Qatar kutokana na kuwa majeruhi na mwaka wake aliokuwa Bayern Munich unakumbukwa zaidi kwa kutibuana na Leroy Sane. Licha ya kufunga mabao 24 na kuasisti 16 huko Al-Nassr, thamani yake imeshuka kwa Euro 11 milioni sokoni.
8. Otavio (-Euro 12 milioni)
Wakati Otavio akiwa mchezaji maarufu kwenye kikosi cha Al-Nassr, kwa mujibu wa Transfermarkt ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa kwenye kikosi hicho kwa mwaka huu wa 2024. Otavio, 29, thamani yake ipo juu kuzidi Cristiano Ronaldo, Sadio Mane na Talisca, lakini kushuka kwa kiwango chake kimekuwa na madhara makubwa Al-Nassr ikiachwa pointi kibao, huku yeye mwenyewe thamani yake sokoni ikishuka kwa Euro 12 milioni.
7. Ruben Neves (-Euro 12 mil)
Kiungo, Ruben Neves kwa sasa yupo kwenye kiwango bora kabisa cha maisha yake ya soka na ndio maana haishangazi kuona anashika namba mbili kwa wachezaji wenye thamani kubwa kwenye mikikimikiki ya Saudi Pro League. Staa huyo amekuwa kwenye kiwango bora na kushuhudia Al-Hilal ikibeba ubingwa wa ligi kirahisi. Lakini, kwa kulinganisha thamani yake huko sokoni kwa mwaka jana na mwaka huu, Neves ameshuka kwa Euro 12 milioni.
6. Kurt Zouma (-Euro 13 mil)
Alikuwa staa kwenye Ligi Kuu England alipocheza katika vikosi vya Chelsea, Everton na West Ham United. Beki Kurt Zouma aliondoka England kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa mkopo kwenda Al-Shabab ili kuipunguzia bajeti ya mishahara West Ham. Beki huyo wa kati amecheza mechi tatu tu kwenye klabu yake mpya, lakini majeraha ya goti yametibua sana kiwango chake na kufanya thamani yake sokoni kushuka kwa Euro 13 milioni.
5. Sergej Milinkovic-Savic (-Euro 15 milioni)
Al-Hilal ilivutiwa na kiwango cha Milinkovic-Savic kwenye mchango wake kwa msimu uliopita, ambapo kiungo huyo alichangia mabao 29 katika michuano yote. Kutokana na mshahara wake wa Pauni 21 milioni, hiyo ina maana Al-Hilal ililipa Pauni 724,000 kwa kila bao la Milinkovic-Savic alilohusika msimu uliopita. Amefunga mabao sita na kuasisti mara tatu msimu huu, lakini thamani yake sokoni kwa mwaka huu imeshuka kwa Pauni 15 milioni.
4. Fabinho (-Euro 17 mil)
Al-Ittihad ililipa Pauni 40 milioni kunasa saini ya Fabinho akakipige Saudi Arabia mwaka 2023, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya thamani yake ya sokoni kwa sasa. Mbrazili huyo alizoea mazingira mapya kwa haraka sana, lakini hilo halikumfanya kucheza kwa kiwango bora kwenye kikosi cha waajiri wake wapya kitu ambacho kwa mujibu wa Transfermarkt inaonyesha thamani yake imeshuka kwa Euro 17 milioni.
3. Joao Cancelo (-Euro 22 mil)
Licha ya Cancelo kupambania uhamisho wa jumla wa kujiunga Barcelona, jambo hilo lilishindikana na badala yake Manchester City iliamua kumuuza kwenda Al-Hilal kwa dau la Pauni 21.2 millioni. Mreno huyo anacheza beki ya kulia kwenye kikosi kwa mabingwa hao wa Saudia, ikishinda mechi 12 kati ya 13. Amechangia mabao tisa kwenye mechi 21 za kichuano yote, lakini thamani yake sokoni imeshuka kwa kiwango kikubwa sana, Euro 22 milioni.
2. Moussa Diaby (-Euro 25 milioni)
Akinaswa na Al-Ittihad kutokea Aston Villa kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, Diaby ndiye mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi sokoni kwenye ligi ya Saudi Arabia, akiwa na thamani ya Euro 35 milioni. Winga huyo amefunga bao moja na kuasisti mara 10 kwenye mechi 10 za Saudi Pro League, huku kiwango chake hicho kikifanya thamani yake sokoni kushuka kwa Euro 25 milioni.
1. Neymar(-Euro 30mil)
Hakuna ubishi kwamba uhamisho wa Neymar kwenda Al-Hilal umekuwa ni wa majanga tu. Akilipwa mshahara wa Pauni 1.6 milioni kwa wiki, Mbrazili huyo amecheza mechi saba tu tangu alipotua kwenye timu hiyo akitokea PSG kwa ada ya Pauni 75 milioni. Hakucheza kwa mwaka mzima kutokana na kuwa majeruhi na jambo hilo limeshusha thamani yake sokoni kwa Euro 30 milioni na haionekani kama mkataba wake utavuka zaidi ya mwaka 2025.