Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri nyuma ya hat-trick za Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Baada ya Messi, muhtasari wa ukweli bora zaidi kuhusu hat-trick za Kombe la Dunia pamoja na orodha kamili ya kila hat-trick iliyowahi kufungwa katika fainali hizo unaohusisha wachezaji wa kariba zote yaani vijana na wazee ni huu.

NEW YORK, MAREKANI: KOMBE la Dunia lina vitu vyake buana na wanasema raha ya mechi bao! Zimekuwapo hat-trick 55 zilizofungwa katika michuano ya fainali hizo upande wa wanaume hadi ile ya jana iliyotupia na staa wa Argentina, Lionel Messi.

Baada ya Messi, muhtasari wa ukweli bora zaidi kuhusu hat-trick za Kombe la Dunia pamoja na orodha kamili ya kila hat-trick iliyowahi kufungwa katika fainali hizo unaohusisha wachezaji wa kariba zote yaani vijana na wazee ni huu.


MWAMBA SALENKO

Ni mchezaji mmoja tu aliyewahi kufunga mabao matano katika mechi moja ya fainali za Kombe la Dunia, Oleg Salenko wa Urusi. Mabao yake matano yalikuja katika ushindi mkubwa wa mabao 6-1 dhidi ya Cameroon kwenye hatua ya makundi mwezi Juni 1994.

Mabao hayo matano katika mechi hiyo yalifunika mafanikio ya mshambuliaji wa Cameroon, Roger Milla ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga bao katika Kombe la Dunia. Wakati huohuo, mabao hayo yalimfikishia jumla ya mabao sita katika Kombe la Dunia 1994 nchini Marekani, kufuatia bao alilofunga awali dhidi ya Sweden katika hatua ya makundi. Mabao hayo yalitosha kumpatia Kiatu cha Dhahabu (Golden Boot) cha mashindano hayo, ambacho alikigawana na gwiji wa Bulgaria, Hristo Stoichkov.

Ingawa mabao yake yaliisaidia Urusi kupata ushindi, yalikuja kwa kuchelewa mno kuisaidia kufuzu hatua ya mtoano. Mchezo dhidi ya Cameroon haukuwa na umuhimu wa kuamua nafasi ya kufuzu, kwani Sweden na Brazil tayari walikuwa wamejihakikishia nafasi mbili za juu zilizowapeleka hatua ya 16 bora. Salenko hakuwahi tena kuichezea Urusi baada ya hapo, na mabao yake sita katika Kombe la Dunia 1994 ndiyo yalikuwa  pekee kwa timu ya taifa. Hata hivyo, ilikuwa ni njia ya kipekee ya kuhitimisha safari yake.


HAT-TRICK YA HARAKA ZAIDI

Erich Probst hakupoteza muda Juni 1954. Muaustria huyo alifunga hat-trick ndani ya dakika 24 za mwanzo za mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Czechoslovakia na kuiwezesha Austria kuongoza kwa mabao 4-0 kabla ya robo ya kwanza ya mchezo haijamalizika.

Baada ya Ernst Stojaspal kuipa Austria uongozi katika dakika ya tatu, Probst aliongeza mabao mengine matatu katika dakika ya nne, 21 na 24 na hivyo kukamilisha hat-trick ya mapema zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Kombe la Dunia.

Ingawa ilikuwa hat-trick ya mapema zaidi kufungwa, haikuwa ya haraka zaidi kwa kuzingatia muda kati ya mabao matatu. Heshima hiyo inakwenda kwa Laszlo Kiss wa Hungary, ambaye alifunga hat-trick ndani ya dakika saba na sekunde 42 katika Kombe la Dunia 1982 dhidi ya El Salvador ikiwa ni ya haraka zaidi katika historia ya mashindano hayo.


WACHEZAJI WADOGO NA WAKUBWA ZAIDI

Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele bado ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi aliyefunga hat-trick katika Kombe la Dunia.

Hat-trick yake katika ushindi wa Brazil dhidi ya Ufaransa kwenye nusu fainali 1958 ilikuja akiwa na umri wa miaka 17 na siku 244 na ndiye mchezaji pekee aliyewahi kufunga hat-trick akiwa chini ya miaka 18. Mchezaji mwingine mdogo zaidi aliyefunga hat-trick ya Kombe la Dunia ni Edmund Conen wa Ujerumani, aliyetupia dhidi ya Ubelgiji, Mei 1934 akiwa na umri wa miaka 19 na siku 198.

Lionel Messi ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia, akifanya hivyo katika mechi yake ya 200 akiwa na Argentina. Katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao mawili kwenye fainali ya Kombe la Dunia la 2022, gwiji huyo wa Barcelona alifunga hat-trick yake ya kwanza ya Kombe la Dunia katika mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Dunia 2026 kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Algeria, jana, Juni 16, 2026 akiwa na umri wa miaka 38 na siku 357.

Kilichofanya mafanikio hayo kuwa ya kipekee zaidi ni kwamba bao lake la tatu katika mechi hiyo liliifikia rekodi ya Miroslav Klose ya mabao 16 katika historia ya Kombe la Dunia. Pia ulikuwa mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia la sita kwa Messi ikiwa ni rekodi ya kipekee kwake.

Messi alivunja rekodi ya Cristiano Ronaldo, ambapo nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid alikuwa na miaka 33 na siku 130 alipofunga mabao yote matatu ya Ureno katika sare ya 3-3 dhidi ya Hispania kwenye hatua ya makundi 2018.

Bao lake la tatu lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa kwa ustadi mkubwa dakika mbili kabla ya mwisho wa mchezo. Hiyo ilikuwa hat-trick yake ya 51 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, huku pia ikiwa hat-trick ya 51 katika historia ya Kombe la Dunia. Kabla ya Ronaldo, Rob Rensenbrink alikuwa anashikilia rekodi hiyo kwa miaka 30 tangu hat-trick yake kwa Uholanzi dhidi ya Iran katika Kombe la Dunia 1978 akiwa na umri wa miaka 30 na siku 335.


KUFUNGA HAT-TRICK NA KUPOTEZA MECHI

Ni wachezaji watatu tu waliowahi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia na bado wakamaliza upande wa timu iliyopoteza mechi ambao ni Ernst Wilimowski wa Poland dhidi ya Brazil 1938 (walipoteza 6-5), Josef Hügi wa Uswisi dhidi ya Austria 1954 (walipoteza 7-5), na Igor Belanov wa USSR dhidi ya Ubelgiji 1986 (walipopoteza 4-3 baada ya muda wa nyongeza).

Mpe pole Wilimowski hasa kwani alifunga mabao manne katika kipigo cha 6-5 dhidi ya Brazil. Hayo ndiyo yalikuwa mabao yake manne pekee katika Kombe la Dunia, na hakuna hata moja lililoipa Poland uongozi katika mechi hiyo.

Kwa namna fulani, Kylian Mbappe anaweza kuhesabiwa kuwa wa nne baada ya hat-trick yake kwa Ufaransa katika fainali ya 2022, ingawa kipigo hicho kilikuja kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya 3-3 dhidi ya Argentina. Mchezaji mwingine aliyefunga hat-trick bila kumaliza upande wa ushindi ni Cristiano Ronaldo dhidi ya Hispania 2018, ambapo mchezo huo uliisha kwa sare ya 3-3.


HAT-TRICK NYINGI ZAIDI

Just Fontaine ni mmoja wa wachezaji watatu waliowahi kufunga hat-trick katika mechi mbili tofauti ndani ya Kombe la Dunia moja pamoja na Sándor Kocsis (1954) na Gerd Müller (1970). Fontaine alifanya hivyo kupitia hat-trick yake dhidi ya Paraguay na mabao manne zaidi dhidi ya Ujerumani 1958. Mshambuliaji maarufu wa Ujerumani, Gerd Muller alifunga hat-trick mfululizo dhidi ya Bulgaria na Peru katika Kombe la Dunia kule Mexico 1970, zikiwa zimepishana kwa siku tatu. Mchezaji mwingine aliyefunga hat-trick katika mechi mbili mfululizo za Kombe la Dunia ni Kocsis wa Hungary 1954.

Mchezaji mwingine aliyefunga zaidi ya hat-trick moja katika fainali za Kombe la Dunia ni Gabriel Batistuta wa Argentina katika mashindano mawili tofauti. Alifunga mabao matatu dhidi ya Ugiriki 1994 kabla ya kurudia tena dhidi ya Jamaica 1998. Hat-trick zake zote mbili zilifungwa Juni 21 na zote zilikuwa dhidi ya mataifa yaliyokuwa yanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, na katika zote bao la mwisho la kukamilisha hat-trick alifunga kwa penalti.


MWAKA WA HAT-TRICK

Je, ilikuwa rahisi zaidi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia la zamani? Inaonekana hivyo. Mchanganyiko wa sheria zilizokuwa na manufaa zaidi kwa washambuliaji pamoja na tofauti kubwa ya viwango kati ya mataifa inaweza kuwa sababu zinazowezekana.

Kati ya hat-trick 54 za Kombe la Dunia, 26 zilifungwa katika mashindano manane ya kwanza, wakati 28 zilizofuata zimegawanyika katika michuano 14 iliyofuata licha ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya mechi. Karibu asilimia 15 ya hat-trick zote za Kombe la Dunia zilifungwa 1958 na hakuna mashindano mengine yaliyoshuhudia hat-trick nyingi kama nane zilizofungwa mwaka huo. Kombe la Dunia 2006 nchini Ujerumani ndilo pekee ambalo halikushuhudia hata hat-trick moja.


JUMAPILI NDIYO SIKU YAKE

Jumapili ndiyo 'siku ya hat-trick' ambapo 23 zimefungwa ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi zilizofungwa Jumamosi (11), ambayo ndiyo siku inayofuata kwa wingi. Kila siku ya wiki imeshuhudia hat-trick ya Kombe la Dunia, lakini ni moja tu iliyowahi kufungwa Jumatatu katika historia ya mashindano hayo. Hat-trick hiyo ilifungwa na Pedro Miguel Carreira Resendes maarufu Pauleta wa Ureno dhidi ya Poland katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2002.


HAT-TRICK FAINALI

Geoff Hurst alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kufunga hat-trick katika fainali. Hat-trick yake maarufu kwa England dhidi ya Ujerumani Magharibi 1966 katika Uwanja wa Wembley ilikamilishwa katika dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza na kuisaidia England kushinda mabao 4-2 ikiwa ni taji pekee la Kombe la Dunia. Hurst alifunga mabao mengi zaidi katika mechi hiyo (matatu) kuliko alivyofunga katika mechi zake nyingine tano za Kombe la Dunia kwa pamoja (mawili).

Kylian Mbappe ndiye mchezaji mwingine pekee aliyefanikiwa kufanya hivyo, akifunga mabao matatu kwa Ufaransa katika fainali ya 2022. Hata hivyo, haikutosha kwani Argentina iliyoongozwa na Messi ilipeleka mchezo kwenye mikwaju ya penalti baada ya sare ya 3-3, na hatimaye kushinda kwa penalti 4-2.

Ademir alikuwa mfungaji wa mabao manne katika ushindi wa Brazil wa 7-1 dhidi ya Sweden katika raundi ya mwisho ya kundi la Kombe la Dunia 1950. Hata hivyo, fainali ya Kombe la Dunia mwaka huo kwa kawaida huchukuliwa kuwa ni kipigo cha Brazil cha mabao 2-1 dhidi ya Uruguay katika mechi ya mwisho ya kuamua bingwa wa mashindano hayo.



Orodha hat-trick Kombe la Dunia

URUGUAY 1930

Julai 17,  1930 (Bert Patenaude vs Paraguay)

Julai 19, 1930 (Guillermo Stabile vs Mexico)

Julai 27, 1930 (Pedro Cea vs Yugoslavia)


ITALIA 1934

Mei 27, 1934 (Angelo Schiavio vs Marekani)

Mei 27, 1934 (Edmund Conen vs Ubelgiji)

Juni 3, 1934 (Oldrich Nejedly vs Ujerumani)


UFARANSA 1938

Juni 5, 1938 (Leonidas vs Poland)

Juni 5, 1938 (Ernst Wilimowski vs Brazil bao 4)

Juni 12, 1938 (Gustav Wetterström vs Cuba)

Juni 12, 1938 (Harry Andersson vs Cuba)


BRAZIL 1950

Julai 2, 1950 (Oscar Miguez vs Bolivia)

Julai 9, 1950 (Ademir vs Sweden bao 4)


USWISI 1954

Juni 17, 1954 (Sandor Kocsis vs Korea Kusini)

Juni 19, 1954 (Carlos Borges vs Scotland)

Juni 19, 1954 (Erich Probst vs Czech)

Juni 20, 1954 (Burhan Sargun vs Korea Kusini)

Juni 20, 1954 (Sandor Kocsis vs Ujerumani bao 4)

Juni 23, 1954 (Max Morlock vs Uturuki)

Juni 26, 1954 (Josef Hugi vs Austria)

Juni 26, 1954 (Theodor Wagner vs Uswisi)


SWEDEN 1958

Juni 8, 1958 (Just Fontaine vs Paraguay)

Juni 24, 1958 (Pele vs Ufaransa)

Juni 28, 1958 (Just Fontaine vs Ujerumani bao 4)


CHILE 1962

Juni 3, 1962 (Florian Albert vs Bulgaria)


ENGLAND 1966

Julai 23, 1966 (Eusebio vs Korea Kaskazini bao 4)

Julai 30, 1966 (Geoff Hurst vs Ujerumani)


MEXICO 1970

Juni 7, 1970 (Gerd Müller vs Bulgaria)

Juni 10, 1970 (Gerd Muller vs Peru)


UJERUMANI MAGHARIBI 1974

Juni 18, 1974 (Dusan Bajevic vs DR Congo)

Juni 19, 1974 (Andrzej Szarmach vs Haiti)


ARGENTINA 1978

Juni 3, 1978 (Rob Rensenbrink vs Iran)

Juni 11, 1978 (Teofilo Cubillas vs Iran)


HISPANIA 1982

Juni 15, 1982 (Laszlo Kiss vs El Salvador)

Juni 20, 1982 (Rummenigge vs Chile)

Juni 28, 1982 (Zbigniew Boniek vs Ubelgiji)

Julai 5, 1982 (Paolo Rossi vs Brazil)


MEXICO 1986

Juni 8, 1986 (Preben Elkjær vs Uruguay)

Juni 11, 1986 (Gary Lineker vs Poland)

Juni 15, 1986 (Igor Belanov vs Ubelgiji)

Juni 18, 1986 (Butragueno vs Denmark bao 4)


ITALIA 1990

Juni 17, 1990 (Michel vs Korea Kusini)

Juni 23, 1990 (Tomas Skuhravy vs Costa Rica)


MAREKANI 1994

Juni 21, 1994 (Batistuta vs Ugiriki)

Juni 28, 1994 (Salenko vs Cameroon bao 5)


UFARANSA 1998

Juni 21, 1998 (Batistuta vs Jamaica)


KOREA KUSINI 2002

Juni 1, 2002 (Miroslav Klose vs Saudia)

Juni 10, 2002 (Pauleta vs Poland)


UJERUMANI 2006

Hakukuwa na hat-trick


AFRIKA KUSINI 2010

Juni 17, 2010 (Higuaín vs Korea Kusini)


BRAZIL 2014

Juni 16, 2014 (Thomas Muller vs Ureno)

Juni 25, 2014 (Xherdan Shaqiri vs Honduras)


RUSSIA 2018

Juni 15, 2018 (Ronaldo vs Hispania)

Juni 24, 2018 (Harry Kane vs Panama)


QATAR 2022

Des 6, 2022 (Goncalo Ramos vs Uswisi)

Des 18, 2022 (Kylian Mbappe vs Argentina)


CANADA, MEXICO, MAREKANI 2026

Juni 16, 2026 (Lionel Messi vs Algeria)