Prime
Simba yabadili ‘gia angani’ yamfuata muuaji wa Yanga
BAADA ya dakika 90 za mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa juzi Jumatano, Simba na Yanga zimeibuka na hesabu mpya za usajili na sasa Wekundu hao wanataka kuongeza mashine ya mabao.
Simba inataka kuhakikisha inaingiza mshambuliaji mwingine wa maana ili kuja kuongeza kitu kwenye safu yake ya ushambuliaji na sasa imewasiliana na Tonny Talasi raia wa DR Congo anayeichezea Aigles Du Congo ili kumuongeza haraka kwenye kikosi hicho.
Kama humfahamu, Talasi ni yule ambaye wikiendi iliyopita aliwafunga Yanga mabao mawili wakati Aigles Du Congo ikishinda 2-1 kwenye Yanga Day pale Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Simba haimtaki Talasi kwa kuwa aliwafunga Yanga tu, bali hesabu zao zinatokana na ubora wa mshambuliaji huyo ambaye msimu wa juzi kwenye Ligi Kuu ya DR Congo alifanikiwa kuwa mfungaji bora.
Mabosi wa Wekundu hao wameshawasiliana na mshambuliaji huyo aliyezaliwa Desemba 23, 2005 akiwa na umri wa miaka 20 ambaye amekubali kila kitu akiwaachia kazi ya kumalizana na Aigles Du Congo ambayo bado ana mkataba nao wa miaka miwili.
Simba haitaki kuingia msimu mpya kwa kumtegemea mshambuliaji Ibrahim Doumbia peke yake ambapo mabosi wa klabu hiyo wameanza kupata wasiwasi juu ya ubora wake licha ya kwamba kocha wa Wekundu hao, Steve Barker anaamini raia huyo wa Mali atakuja kushangaza baadaye akishaweza kuzoeana na wenzake.
“Kocha anatuambia tutulie lakini kaka ni vigumu kuamini hilo kirahisi, kadiri ya muda unavyowenda mashabiki wetu nao wanazidi kupoteza imani naye na hata sisi tumeanza kupata hayo mashaka, tunaona ni bora tumuongeze Talasi,” amesema bosi huyo wa juu.
Endapo usajili wa Talasi utakamilika, mshambuliaji huyo atakwenda kuungana na Doumbia na Ismail Mgunda ambao wote watakuwa wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha kubwa la msimu wa 2026-2027.