Balotelli afufua ugomvi na Zlatan
Muktasari:
- Licha ya kupita miaka mingi tangu wawili hao walipokuwa wachezaji wenza katika kikosi cha Inter Milan, bado wameendelea kurushiana vijembe kila wanapoamua kufanya hivyo, na safari hii, Balotelli amefufua mjadala huo wakati wa mahojiano na mtayarishaji wa maudhui ya soka kutoka England, Ellis Platten, anayejulikana kupitia chaneli ya YouTube ya Away Days.
MILAN, ITALIA: VITA vya maneno kati ya nyota wa zamani wa soka Mario Balotelli na Zlatan Ibrahimovic vimechukua sura mpya baada ya Balotelli kumkumbusha Mswedeni huyo kuhusu taji moja kubwa ambalo hajawahi kulitwaa katika maisha yake ya soka la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Licha ya kupita miaka mingi tangu wawili hao walipokuwa wachezaji wenza katika kikosi cha Inter Milan, bado wameendelea kurushiana vijembe kila wanapoamua kufanya hivyo, na safari hii, Balotelli amefufua mjadala huo wakati wa mahojiano na mtayarishaji wa maudhui ya soka kutoka England, Ellis Platten, anayejulikana kupitia chaneli ya YouTube ya Away Days.
Mazungumzo yalipomgeukia Ibrahimovic, Balotelli hakusita kutaja tofauti kubwa kati yao, ambapo ingawa Zlatan anahesabiwa kuwa mmoja wa washambuliaji bora kabisa kuwahi kutokea Ulaya na ametwaa mataji ya ligi katika nchi mbalimbali, hakuwahi kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya katika maisha yake ya soka.
Kwa upande wa Balotelli, alikuwamo kwenye kikosi cha Inter Milan kilichotwaa mataji matatu 2010, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya chini ya kocha Jose Mourinho, na hilo ndilo taji ambalo anaamini linamuweka mbele ya Ibrahimovic katika kipengele hicho.
Baada ya mafanikio hayo, Balotelli aliendelea kucheza katika klabu mbalimbali nchini Italia, England, Ufaransa, Uturuki na Uswisi.
Kauli hiyo za Balotelli inakuja baada ya Ibrahimovic kumkosoa hadharani 2023 aliposema alikuwa na kipaji kikubwa cha kuwa mmoja wa wachezaji bora duniani, lakini alishindwa kukitumia ipasavyo kutokana na kushindwa kujituma na kutumia vizuri fursa alizozipata.
Badala ya kujibu kwa maneno mengi, Balotelli aliweka picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa ameshikilia kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akimtaja Zlatan kwenye chapisho.
Balotelli amekuwa mmoja wa wachezaji waliojadiliwa zaidi katika kizazi chake kwani katika ubora wake, alitamba kwa kuwa na nguvu, uwezo mkubwa wa kiufundi na mabao ya kukumbukwa.
Aliisaidia Italia kufika fainali ya Euro 2012, huku pia akitwaa mataji akiwa na Inter Milan na Manchester City. Hata hivyo, maisha yake ya soka yaligubikwa na kutokuwa na mwendelezo wa ubora na kubadilisha klabu mara kwa mara, jambo lililowafanya wengi kuamini hakuwahi kufikia kiwango kikubwa ambacho alitabiriwa akiwa kijana.
Kwa upande mwingine, Ibrahimovic alijijengea heshima kama mmoja wa washambuliaji bora zaidi wa kizazi chake akitwaa mataji ya ligi Uholanzi, Italia, Hispania na Ufaransa, huku akiwa pia ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Sweden.
Katika maisha yake ya soka alizichezea Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, PSG, Manchester United na AC Milan.