Kisa Vinicius Jr, Real Madrid yaweka mezani Pauni 19 milioni
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa Vinicius ndani ya kikosi cha Real Madrid unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, hali ambayo imeifanya Arsenal kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo hayo.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid inaonekana kuwa na imani kubwa ya kuzima kabisa nia ya Arsenal ya kumsajili nyota wao wa Brazil, Vinicius Jr, baada ya kumwekea mezani ofa mpya ya mkataba wenye nyongeza ya thamani inayozidi pauni 19 milioni kwa mwaka.
Mkataba wa sasa wa Vinicius ndani ya kikosi cha Real Madrid unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, hali ambayo imeifanya Arsenal kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo hayo.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu England tayari imemfahamisha mchezaji huyo kuwa ipo tayari kuingilia kati endapo atashindwa kufikia makubaliano mapya na miamba hiyo ya Hispania.
Mazungumzo muhimu kati ya mawakala wa Vinicius, Mkurugenzi Mkuu wa Real Madrid, Jose Angel Sanchez, pamoja na Mkuu wa Idara ya Usajili, Juni Calafat, yalifanyika jijini Madrid siku ya Jumatano.
Wakati huohuo, kocha Jose Mourinho alisisitiza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 bado ni sehemu muhimu ya mipango yake ndani ya kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa viongozi wa Real Madrid wameongeza kiwango cha kujiamini kwamba watafanikiwa kumbakisha Vinicius Santiago Bernabeu na kumshawishi aendelee kuitumikia klabu hiyo kwa miaka ijayo.
Hata hivyo, licha ya hali hiyo kuonekana kuwa nzuri kwa upande wa Real Madrid, Vinicius aliongeza gumzo kuhusu hatima yake baada ya kufanya uamuzi uliozua mjadala mkubwa usiku wa Jumatano, alipofuta historia yote ya machapisho kwenye akaunti yake ya Instagram.
Kwa sasa, ukurasa wa Vinicius wenye wafuasi milioni 63.9 hauna picha yoyote wala maelezo ya wasifu (bio), huku pia akiwa ameondoa picha yake ya wasifu.
Hatua hiyo, ambayo si jambo geni kwa baadhi ya wanasoka wa kiwango cha juu, inaweza kutafsiriwa kwa namna mbalimbali. Mara nyingi imekuwa ikionekana kama ishara ya kutoridhishwa na hali ilivyo ndani ya klabu anayochezea mchezaji husika.
Picha zote zilizokuwa zikimuonyesha Vinicius akiwa mazoezini na akicheza mechi akiwa na jezi ya Real Madrid zimeondolewa kabisa kwenye akaunti hiyo.
Wakati sintofahamu hiyo ikiendelea, Arsenal inaendelea kusubiri kwa matumaini makubwa ikiwa tayari kutumia nafasi yoyote itakayojitokeza.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England walifanya mawasiliano ya awali kuhusu uwezekano wa kumsajili Vinicius wiki iliyopita, huku kocha Mikel Arteta akisisitiza kuwa klabu yake itakuwa na malengo makubwa katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, taarifa zilizotolewa Jumatano zilieleza kuwa Real Madrid ina imani kubwa ya kuzuia jaribio lolote kutoka Kaskazini mwa London, hasa kutokana na uungwaji mkono wa Mourinho kwa mchezaji huyo.
Moja ya changamoto kubwa katika mazungumzo ya mkataba mpya kati ya Real Madrid na upande wa Vinicius imekuwa ni kiwango cha fedha za kusaini mkataba mpya (signing bonus).
Lakini baada ya Real Madrid kuongeza thamani ya ofa yao ya mwisho, viongozi wa klabu hiyo wanaamini Vinicius Jr atakubali kuendelea kuitumikia miamba hiyo ya Hispania.
Real Madrid haitaki kabisa kumpoteza nyota huyo wa Brazil bure, wakati mkataba wake ukiwa umesalia na chini ya mwaka mmoja kabla ya kumalizika.
Inaelezwa kuwa Vinicius anaiona mkataba wowote mpya atakaousaini na Los Blancos, klabu ambayo ameichezea tangu mwaka 2018, kuwa ndiyo mkataba muhimu zaidi katika maisha yake ya soka na utakaokuwa ishara ya kuthamini mchango wake mkubwa ndani ya timu hiyo.
Katika misimu ya hivi karibuni, kiwango chake bora kimefanya atajwe miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo ya Ballon d'Or akiwa na jezi ya Real Madrid.
Vinicius alirejea kuungana na wenzake kambini Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, ambapo alifanyiwa vipimo vya kawaida vya afya kabla ya kuanza mazoezi chini ya kocha mpya, Jose Mourinho.
Kwa upande mwingine, Mikel Arteta ameendelea kuonyesha matumaini makubwa kuhusu mipango ya Arsenal katika kipindi kilichosalia cha dirisha la usajili, kufuatia kukamilisha usajili wa winga Christos Tzolis kutoka Club Brugge kwa ada ya pauni 34 milioni.
Akizungumza baada ya mchezo wa kirafiki wa maandalizi dhidi ya Girona, Arteta amesema:
"Tunatarajia kuona mabadiliko katika wiki chache zijazo. Ni jambo la kawaida."
"Tunataka kuwa bora zaidi kama ambavyo kila timu nyingine inataka. Ukiangalia kinachoendelea kwenye soko la usajili pamoja na wapinzani wetu, hatutakaa kimya. Tuna malengo makubwa sana katika kile tunachokifanya."
"Tofauti za ushindani ni ndogo sana. Tunataka kuendelea kuboresha kikosi chetu kwa sababu kiwango cha ushindani kitaongezeka."
"Tunahitaji kuongeza ushindani wa ndani ya kikosi na kuhakikisha tunabaini maeneo ambayo bado hayajakamilika ili tuyafanyie kazi."