Sare ya 2-2 yamnyong’onyesha Mikel Arteta
Muktasari:
- Arsenal iliruhusu lao la kwanza dakika 36, na kisha ikafungwa tena katika muda wa nyongeza, jambo lililowafanya wapoteze pointi muhimu dhidi ya Black Cats, timu hizo zikitoka sare.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amekiri kwamba haikuwa rahisi kuamini kama kikosi chake kimelazimishwa sare, baada ya wenyeji wao Sunderland kupata bao la dakika za mwisho jana Jumamosi, Novemba 8, 2025.
Arsenal iliruhusu lao la kwanza dakika 36, na kisha ikafungwa tena katika muda wa nyongeza, jambo lililowafanya wapoteze pointi muhimu dhidi ya Black Cats, timu hizo zikitoka sare.
Matokeo hayo yanaweza kufufua upya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England, kutokana na timu pinzani kupata nafasi ya kupumua kwa kuifukuzia The Gunners inayoendelea kuongoza msimamo wa EPL kwa kufikisha pointi 26.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema hakuamini kilichotokea, lakini hana budi kukubaliana na uhalisia, kwani ndivyo soka lilivyo.
Amesema upungufu uliojitokeza kwenye mechi hiyo, ulitoa nafasi kwa wenyeji wao kupata bao la kusawazisha ambalo anaamini kila shabiki wa Arsenal hataki hata kuliona.
“Nilihisi maumivu tumboni, sipendi kuruhusu bao lolote. Bao lile liliweka mechi katika hali ngumu sana,” alisema Arteta.
Daniel Ballard alianza kuifungia Sunderland dhidi ya timu yake ya zamani, kabla ya mabao ya Bukayo Saka na Leandro Trossard kugeuza mchezo kwa muda.
Lakini katika dakika ya 90+4, Brian Brobbey alifunga bao la kusawazisha, na hivyo kumaliza rekodi ya Arsenal ya kushinda michezo mitano mfululizo kwenye EPL.
Matokeo hayo sasa yanaacha Arsenal ikiwa na pengo la pointi saba juu ya Manchester City, ambayo inatarajiwa kucheza dhidi ya bingwa mtetezi Liverpool leo Jumapili, Novemba 09, 2025.