Arteta atumia AI kusaka taji la EPL
Muktasari:
- Arteta kabla ya mechi za leo Jumamosi kikosi chake cha Arsenal kipo kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita na amesema matumizi ya AI katika uchambuzi wa viwango vya wachezaji wake pamoja na mbinu za kiufundi, zitaleta msaada mkubwa.
LONDON, ENGLAND: KOCHA Mikel Arteta anaamini Akili Mnemba (AI) itaichagiza Arsenal katika mpango mkakati wa kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Arteta kabla ya mechi za leo Jumamosi kikosi chake cha Arsenal kipo kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita na amesema matumizi ya AI katika uchambuzi wa viwango vya wachezaji wake pamoja na mbinu za kiufundi, zitaleta msaada mkubwa.
Kabla mechi ya Sunderland ya Jumamosi, Arteta alisema: “Ni kifaa chenye nguvu kubwa kama utakitumia ipasavyo na kuuliza maswali sahihi. Kinatumika kwenye mambo mengi na kinaweza kusaidia si tu kwenye timu, bali kwenye taasis nyingine pia. Mimi sio mtaalamu, lakini ni kifaa chenye thamani kubwa.
“Tumetengeneza vitu kadhaa ambavyo kwa maoni yetu tunaona vitatusaidia kujifahamu wenyewe ubora wetu na kufanya tathmini ya kile tunachoweza kuboresha.
“Na tutaangalia namna ya kutumia kifaa hicho kwenye maeneo mengine ya klabu. Inanifikirisha sana. Unaweza kuuliza swali lolote. Kama kina umuhimu kiasi hiki, basi kitatusaidia hakika.”
Kocha Arteta alisema wachambuzi wa kiufundi kwenye klabu watafanya upembezi wa taarifa zote za AI katika usahihi mkubwa ili kuleta manufaa yanayohitajika.
“Kutokana na takwimu, utapaswa kuzitafsiri takwimu hizo na maana yake.”