Mateso kwa Mikel Arteta
Muktasari:
- Baada ya msimu mrefu na mgumu, nyota wa Arsenal wamehitimisha safari yao ya Kombe la Dunia wakiwa wamecheza dakika nyingi zaidi kuliko karibu timu zote za Ligi Kuu England, hali inayoongeza wasiwasi kuelekea msimu mpya.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amekumbana na changamoto kubwa kufuatia baadhi ya wachezaji wake muhimu kurejea kutoka Kombe la Dunia wakiwa na majeraha na uchovu mkubwa.
Baada ya msimu mrefu na mgumu, nyota wa Arsenal wamehitimisha safari yao ya Kombe la Dunia wakiwa wamecheza dakika nyingi zaidi kuliko karibu timu zote za Ligi Kuu England, hali inayoongeza wasiwasi kuelekea msimu mpya.
Kiungo Declan Rice ndiye aliyecheza dakika nyingi zaidi baada ya kumaliza msimu na mashindano ya Kombe la Dunia akiwa ametimiza dakika 5,482 katika mechi 69 alizoichezea klabu na timu ya taifa.
Bukayo Saka bado anasumbuliwa na tatizo la mshipa wa kisigino (Achilles) ambalo limemsumbua kwa miezi kadhaa, huku beki William Saliba akihofia kufanyiwa upasuaji kutokana na maumivu ya mgongo yaliyojitokeza tena katika mchezo wa nusu fainali wa Ufaransa.
Katika fainali ya Kombe la Dunia, kiungo Mikel Merino naye alipata pigo usoni baada ya kupigwa na shuti kali la Lionel Messi. Baada ya mchezo huo alionekana akiwa amevimba jicho na kuweka picha kwenye mitandao ya kijamii akionyesha majeraha hayo, huku akitumia chupa ya bia kupunguza uvimbe. Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hali yake si mbaya.
Sasa jukumu kubwa lipo kwa idara ya tiba ya Arsenal kuhakikisha wachezaji hao wanapona kwa wakati, huku wakitarajiwa kupewa angalau wiki tatu za mapumziko kabla ya kurejea kambini.
Arsenal ilikuwa na jumla ya wachezaji 15 katika Kombe la Dunia, akiwemo Leandro Trossard ambaye tayari ameondoka klabuni, huku wachezaji wanane wakifika hatua za mwisho za mashindano.
Kwa ujumla, nyota wa Arsenal walikusanya dakika 4,224 uwanjani katika mashindano hayo. Ni Manchester City pekee iliyokuwa na jumla kubwa zaidi ya dakika 5,925 miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England.
Hali hiyo imeongeza presha kwa Arteta, hasa ikizingatiwa Arsenal ilicheza mechi 63 msimu uliopita uliomalizika Mei 30, huku siku mbili baadaye baadhi ya wachezaji wakielekea moja kwa moja kwenye Kombe la Dunia.
Ligi Kuu England inatarajiwa kurejea ndani ya mwezi mmoja, na Arsenal itaingia msimu mpya ikiwa bingwa mtetezi lakini ikiwa na wasiwasi kuhusu utimamu wa Rice, Saka na Saliba.
Kutokana na ratiba hiyo ngumu, Arsenal imebadili maandalizi yake ya msimu mpya. Badala ya ziara ndefu ya kimataifa, timu imechagua kufanya maandalizi nchini Hispania.
Baada ya kambi fupi jijini Marbella, kikosi kilianza rasmi mazoezi wiki hii na kitacheza mechi ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Girona Agosti 1, kabla ya kuvaana na Real Betis mjini Dublin siku nne baadaye.
Baada ya hapo, Arsenal itarejea London kucheza mechi mbili za kirafiki katika Uwanja wa Emirates kabla ya kuikabili Manchester City kwenye mchezo wa Community Shield utakaopigwa Agosti 16 mjini Cardiff.
Wakati huohuo, klabu hiyo imefanya mabadiliko makubwa katika idara yake ya afya na utimamu wa mwili. Daktari wa klabu Zafar Iqbal na mkuu wa sayansi ya michezo Tom Allen wameondoka, sambamba na kocha wa utimamu Sam Wilson aliyejiunga na Parma ya Italia.
Nafasi zao zimejazwa na Dk. Arnaldo Abrantes aliyewasili kutoka Aston Villa, mtaalamu wa marekebisho ya majeraha Eneko Angulo kutoka Real Betis, pamoja na kocha wa mazoezi ya viungo Jose Jimenez kutoka Bayer Leverkusen.
Wataalamu hao wapya wanatarajiwa kuanza kazi kwa kuhakikisha Ben White na Jurrien Timber wanarejea katika kiwango bora, huku pia wakisaidia kupunguza tatizo la majeraha lililoisumbua Arsenal msimu uliopita.
Aidha, kuchelewa kurejea kwa baadhi ya nyota kutokana na Kombe la Dunia kunaweza kufungua milango kwa vipaji chipukizi kama Max Dowman (16), Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly kupata nafasi zaidi katika kikosi cha kwanza wakati wa maandalizi ya msimu mpya.