William Saliba nje miezi mitano
Muktasari:
- Saliba alipata maumivu makali wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Hispania, ambapo alishindwa kuendelea na mchezo baada ya dakika 30 pekee.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imepata pigo kubwa baada ya beki wake tegemeo, William Saliba, kuripotiwa kuwa huenda akakaa nje ya uwanja kwa miezi minne hadi mitano kutokana na majeraha ya mgongo.
Saliba alipata maumivu makali wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya Ufaransa na Hispania, ambapo alishindwa kuendelea na mchezo baada ya dakika 30 pekee.
Ripoti zinaeleza beki huyo atafanyiwa upasuaji, jambo litakalomfanya kuukosa mwanzo wa msimu mpya wa Ligi Kuu England na kuiacha Arsenal bila mmoja wa mabeki wake muhimu.
Inaelezwa Saliba alimwambia mwenzake Dayot Upamecano kuwa hakuwa na uwezo wa kuendelea kutokana na maumivu makali ya mgongo yaliyokuwa yakimsumbua hata kabla ya mashindano hayo kuanza.
Kutokuwepo kwake ni pigo kubwa kwa Arsenal ambayo imekuwa ikimtegemea kama nguzo ya safu ya ulinzi katika misimu ya hivi karibuni na hivyo atakosa baadhi ya michezo ya mwanzoni mwa msimu ujao unaoanza Agosti.