Salah ashikilia dili la Federico Chiesa kusajiliwa Juventus
Muktasari:
- Ikiwa Salah ataamua kubaki Anfield, Liverpool itakubali kumwachia Chiesa, lakini endapo atahitaji kuondoka Januari hii basi hawatamwachia Chiesa.
MATUMAINI ya Juventus kumsajili winga wa kimataifa wa Italia, Chiesa, mwenye umri wa miaka 28, yamefifia kwa sasa baada ya Liverpool kuwaeleza kuwa haitamtoa fundi huyo kabla ya kujua mustakabali wa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah, mwenye umri wa miaka 33.
Ikiwa Salah ataamua kubaki Anfield, Liverpool itakubali kumwachia Chiesa, lakini endapo atahitaji kuondoka Januari hii basi hawatamwachia Chiesa.
Napoli pia inadaiwa kuhitaji huduma ya Chiesa, lakini hadi sasa haijaanza mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji wala Liverpool ambayo nayo ikidaiwa kuwa inajaribu kutazama upepo kabla ya kuingia.
Mkataba wa sasa Chiesa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 20 za michuano yote, amefunga mabao mawili na kutoa asisti tatu. hiesa amekuwa akitamani sana kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha.
Michail Antonio
DILI la straika wa zamani wa West Ham, Michail Antoni kujiunga na Leicester City linadaiwa kufeli baada ya kugundulika kuwa na majeraha ya misuli wakati akifanyiwa vipimo vya afya.
Staa huyu wa kimataifa wa Jamaica mwenye umri wa miaka 35, hajacheza mechi yoyote ya tangu apate ajali ya gari Desemba 2024. Leicester ilitaka kumsajili ikiamini angeenda kuwasaidia.
Kim Min-jae
AC Milan inataka kumsajili beki wa kati wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Korea Kusini, Kim Min-jae, mwenye umri wa miaka 29, kwa mkopo wa nusu msimu.
Hata hivyo, dili hilo linaonekana kusuasua kwani Milan haitaki kulipa asilimia mia ya mshahara wa Kim badala yake inahitaji Bayern pia ichangie asilimia kadhaa. Mabosi wa Bayern wanadaiwa kugoma.
Upamecano
BAYERN Munich imempa beki wake wa kimataifa wa Ufaransa, Dayot Upamecano, mwenye umri wa miaka 27, ofa mpya iliyoboreshwa ya kuongeza mkataba wake ambao unatarajiwa kumalizika katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mabingwa hao wa Ujerumani wanataka kumsainisha mchezaji huyu mkataba mpya haraka iwezekanavyo, lakini Upamecano mwenyewe anaonekana kutokuwa na presha.
Klabu kadhaa kubwa barani Ulaya zimeonyesha nia ya kumsajili.
Joshua Zirkzee
MKURUGENZI wa Roma, Ricky Massara, ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na Uholanzi, Joshua Zirkzee, mwenye umri wa miaka 24 baada ya kocha mkuu Ruben Amorim kuondoka.
Zirkzee alikuwa akitajwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Man United, lakini sasa anaweza akataka kubaki ili kuona endapo atapata nafasi mbele ya kocha mpya.
Mkataba wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Robert Lewandowski
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Poland, Robert Lewandowski, mwenye umri wa miaka 37, amesisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka Barcelona katika dirisha hili la usajili la Januari.
Licha ya kuwapo kwa nia kutoka klabu kadhaa zinazotaka huduma yake katika dirisha hili, Lewandoski amekataa kuondoka akisisitiza kuwa atabakia hadi mwisho wa msimu kisha kufikiria kwa umakini kama aendelee kucheza au astaafu.
Lewandowski pia anaamini bado ana mchango mkubwa wa kutoa katika kikosi cha Barca kwa sasa.
Mohammed Kudus
TOTTENHAM Hotspur inaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji mpya katika dirisha hili la usajili la Januari baada ya kuona kuwa jeraha la winga wake wa kimataifa wa Ghana, Mohammed Kudus, mwenye umri wa miaka 25, ni kubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa awali.
Jeraha hilo linaweza kumuweka Kudus nje kwa muda mrefu, jambo linalowalazimu mabosi wa Spurs kutafuta suluhisho la haraka ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Jorgen Strand Larsen
NEWCASTLE United itatakiwa kupambana na Tottenham Hotspur endapo itarudi tena mezani kufanya mazungumzo na Wolves kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa klabu hiyo na Norway, Jorgen Strand Larsen, mwenye umri wa miaka 25.
Larsen ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030, amekuwa katika kiwango kizuri msimu huu, akifunga mabao matatu katika mechi 23 za michuano yote.