Sababu kifo cha staa NBA
Muktasari:
- Clarke, aliyekuwa mchezaji wa Memphis Grizzlies, alipatikana akiwa hajitambui katika chumba chake cha kulala nyumbani kusini mwa California, Marekani, Mei 11, na baadaye kutangazwa kuwa amefariki.
CALIFORNIA, MAREKANI: SABABU ya kifo cha mchezaji wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), Brandon Clarke, mwenye umri wa miaka 29, imefahamika baada ya mtaalamu wa uchunguzi wa vifo kusema alifariki dunia kutokana na madhara ya heroini na cocaine.
Clarke, aliyekuwa mchezaji wa Memphis Grizzlies, alipatikana akiwa hajitambui katika chumba chake cha kulala nyumbani kusini mwa California, Marekani, Mei 11, na baadaye kutangazwa kuwa amefariki.
Wahudumu wa afya waliitwa katika nyumba hiyo iliyopo eneo la San Fernando Valley majira ya saa 11 jioni, ambapo vyanzo visivyo rasmi vilidai baadaye kwamba vifaa vinavyohusishwa na matumizi ya dawa za kulevya vilikutwa karibu na mwili wake.
Idara ya uchunguzi wa vifo ya Los Angeles County sasa imesema kifo cha Clarke kilisababishwa na “madhara ya heroini na cocaine” na kwamba kilikuwa cha bahati mbaya. Maofisa wa idara hiyo pia walitaja madhara ya pamoja ya dawa kadhaa za kuandikiwa na daktari kama chanzo kilichochangia kifo hicho, ingawa hawakutaja dawa hizo.
Katika taarifa fupi iliyotolewa, ofisi hiyo ilisema: “Ripoti ya mtaalamu wa uchunguzi wa vifo itapatikana baadaye.”
Matokeo ya uchunguzi wa mwili yalionyesha pia kuwa dawa za kuandikiwa na daktari zilichangia katika kifo hicho, jambo lililoibua maswali zaidi kuhusu vitu vilivyokuwa katika mfumo wa mwili wake katika saa zake za mwisho.
Kifo cha Clarke kilitokea baada ya miaka yake ya mwisho NBA kuathiriwa na majeraha makubwa, ambapo kuna wakati alikaa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuchanika kwa tendoni 2023. Mwaka 2025 alifanyiwa upasuaji mara mbili kwenye goti lake la kulia, na msimu wa 2025/26 alicheza mechi mbili pekee baada ya kupata jeraha kubwa la misuli.
Wiki sita kabla ya kifo chake, Clarke pia alikamatwa Arkansas baada ya polisi kumfuatilia katika tukio la kuendesha gari kwa mwendo kasi uliodaiwa kufikia zaidi ya kilomita 140 kwa saa, kisha wakasema walikuta begi lenye gramu 235 za kratom, kiasi kinachokadiriwa kuwa karibu vidonge 1,200.
Katika tukio hilo Clarke alidaiwa kuwaambia polisi: “Ni kratom tu.” Kratom ni mmea unaotumiwa na baadhi ya watu kujitibu maumivu ya muda mrefu, msongo wa mawazo au dalili za kujiondoa kwenye matumizi ya opioid. Ingawa kratom ni halali huko Tennessee, ambako Clarke aliishi, huko Arkansas imeainishwa kama tiba inayodhibitiwa kisheria na kosa lake linaweza kuwa la jinai.
Mtaalamu wa uchunguzi wa vifo hakusema kama kratom ilikuwepo katika mwili wa Clarke wakati alipofariki dunia.
Nyota huyo alichaguliwa katika nafasi ya 21 kwenye drafti ya NBA 2019 baada ya kuchezea timu ya Chuo Kikuu cha Gonzaga na alitumia kipindi chote cha miaka saba ya taaluma yake NBA akiwa na Memphis Grizzlies.
Alikuwa na wastani wa pointi 10.2 na ribaundi 5.5 kwa kila mchezo, akiwa mchezaji muhimu wa akiba mwenye nguvu na juhudi kubwa, huku akiheshimiwa na wachezaji na makocha kutokana na mtazamo wake chanya mara kwa mara.