LeBron hafikii ukali wa Jordan, Kobe
Muktasari:
- Jordan alijulikana kwa kuwataka wachezaji wenzake kufikia ukamilifu na hakuvumilia makosa, huku Bryant akiendeleza falsafa hiyo kupitia Mamba Mentality, iliyojengwa kwenye nidhamu kali na kiu ya kuendelea kuboresha kiwango chake kila siku.
NEW YORK, MAREKANI: MJADALA wa nani ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya NBA umeendelea kugawanya maoni kwa miaka mingi, huku majina ya Michael Jordan, Kobe Bryant na LeBron James yakitajwa mara kwa mara.
Wanaomuunga mkono Jordan hujivunia mataji yake sita ya NBA na ushindani wake usio na kifani, huku mashabiki wa Kobe Bryant wakisifu nidhamu, kujituma na falsafa yake maarufu ya Mamba Mentality. Kwa upande mwingine, wafuasi wa LeBron James huamini uwezo wake wa kudumu kileleni kwa muda mrefu na kung'ara katika nyakati tofauti za mchezo unamfanya astahili kuitwa mchezaji bora wa muda wote.
Sasa aliyekuwa nyota wa Philadelphia 76ers na Chicago Bulls, Andres Nocioni, ameongeza mtazamo wake kwenye mjadala huo.
Nocioni, ambaye aliwahi kukutana na LeBron mara kadhaa akiwa Chicago Bulls, amesema anamkubali LeBron kama mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kutokea NBA, lakini anaamini hana ukali wa ushindani kwa kiwango cha Jordan na Kobe.
"Ukiwa mpinzani wa Kobe Bryant ilikuwa kama unakutana na muuaji. Alikuwa na ushindani wa hali ya juu sana. Nafikiri ndiye aliyekuwa karibu zaidi na Jordan kwa mtazamo huo wa kisaikolojia, kwa sababu mimi nilicheza pia dhidi ya LeBron James," alisema Nocioni.
Ameongeza kuwa"kwangu LeBron ni miongoni mwa wachezaji wawili au watatu bora kuwahi kutokea NBA, lakini sijui kama ana kile walichokuwa nacho Kobe na Jordan."
TOFAUTI YA UONGOZI
Jordan alijulikana kwa kuwataka wachezaji wenzake kufikia ukamilifu na hakuvumilia makosa, huku Bryant akiendeleza falsafa hiyo kupitia Mamba Mentality, iliyojengwa kwenye nidhamu kali na kiu ya kuendelea kuboresha kiwango chake kila siku.
Kwa upande wa LeBron, mtindo wake wa uongozi umekuwa tofauti. Badala ya kutumia ukali, mara nyingi amekuwa akiongoza kwa mawasiliano mazuri, kujenga umoja ndani ya timu na kuwapa wachezaji wenzake kujiamini.
Wachezaji wengi waliowahi kucheza naye wamekuwa wakimsifu kwa uwezo wake wa kuwaunganisha wenzake na kuwahamasisha katika nyakati ngumu.
Hata hivyo, tofauti hiyo haimaanishi kwamba LeBron hana ushindani. Katika kipindi chote cha kazi yake ameonyesha uwezo mkubwa wa kubeba jukumu katika mechi muhimu, kustahimili presha na kung'ara kwenye hatua za mtoano.
Kwa sasa, mjadala huo umeibuka tena wakati LeBron akianza sura mpya ya maisha yake ya NBA baada ya kujiunga na Philadelphia 76ers, hatua inayompa nafasi ya kuwania ubingwa mwingine akiwa kwenye kikosi chenye nyota wengi na nguvu kubwa ya ushambuliaji.