Ronaldo aonyesha pete ndoa mazoezini
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, na mwanamitindo Georgina walifunga ndoa katika sherehe ya faragha iliyofanyika mapema wiki hii.
RIYADH, SAUDI ARABIA: MSHAMBULIAJI Cristiano Ronaldo akiwa na pete yake ya ndoa mkononi amepokea mapokezi ya upendo kutoka kwa wachezaji wenzake wa Al-Nassr baada ya kurejea kambini kufuatia kufunga ndoa na Georgina Rodriguez.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, na mwanamitindo Georgina walifunga ndoa katika sherehe ya faragha iliyofanyika mapema wiki hii.
Nyota huyo wa Ureno alionekana akiwa na muonekano mpya baada ya kubadilisha rangi ya nywele, huku akiwa amevalia pete ya ndoa aliporejea na kukutana na wachezaji wenzake wa Al-Nassr.
Klabu hiyo ya Saudi Pro League inaendelea na maandalizi ya msimu mpya, ambapo itaanza kampeni dhidi ya Al-Fateh kesho.
Kocha mpya wa Al-Nassr, Ange Postecoglou, aliyewahi kuinoa Tottenham na Nottingham Forest, alimpongeza Ronaldo mwanzoni mwa mazoezi yake ya kwanza tangu arejee kambini.
Katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, kocha huyo raia wa Australia amesema “karibu tena Cris. Hongera na baraka kwako na familia yako, rafiki.”
Ronaldo, akiwa amesimama huku mikono ikiwa kifuani, alionekana akitabasamu wakati wachezaji wenzake wakimpigia makofi.
Postecoglou ameongeza “kwa upande wangu, ni vizuri kuwa nawe tena, rafiki.”
Wiki iliyopita, mashabiki walijaa katika mitaa ya Funchal, Ureno, wakiamini Ronaldo na Rodriguez, mwenye umri wa miaka 32, wangefunga ndoa katika kanisa kuu la jiji hilo.
Hata hivyo, mashabiki hao walibaki wakishangaa baada ya wawili hao kutotokea kwenye kanisa hilo kama ilivyotarajiwa.
Sasa Ronaldo anaelekeza nguvu zake katika kuiongoza Al-Nassr kutetea ubingwa wa Saudi Pro League, baada ya ndoto zake za Kombe la Dunia kufutwa na Hispania msimu huu.
Ronaldo na wenzake wa timu ya taifa ya Ureno walitolewa katika hatua ya 16 bora na Hispania, ambayo baadaye ilitwaa ubingwa huo.
Ronaldo pia hatarajiwi kushiriki Kombe la Dunia lijalo, licha ya Ureno kuwa miongoni mwa mataifa yatakayokuwa wenyeji wa mashindano hayo.
Mshambuliaji huyo anaingia katika msimu mpya wa Saudi Pro League akiwa ametoka kufunga mabao 30 katika mechi 37 alizoichezea Al-Nassr msimu uliopita.
Al-Nassr itakuwa na jukumu la kutetea taji lake baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa na tofauti ya pointi mbili dhidi ya Al-Hilal iliyomaliza nafasi ya pili.
Huo ulikuwa ubingwa wa kwanza ambao Ronaldo alinyanyua tangu alipojiunga na Al-Nassr miaka mitatu iliyopita.