Prime
Mgunda, Mwalimu wawekwa ‘kikaangoni’
MASTAA wa zamani wa Simba na Yanga wamezungumzia tofauti ya uchezaji wa washambuliaji Ismail Mgunda aliyesajiliwa na Simba na Selemani Mwalimu aliyejiunga na Yanga akitokea Simba ambapo alikuwa akicheza kwa mkopo.
Simba ilipata pigo hivi karibuni Yanga ilipomsajili Mwalimu muda mfupi baada ya mchezaji huyo wa zamani wa Fountain Gate kutua kambini Simba.
Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel amesema Mgunda aliyesajiliwa na Simba akitokea Mashujaa licha ya kumaliza na mabao mawili na asisti moja msimu uliopita ni namba tisa halisi na endapo akiwa bora atawashangaza wengi.
Amesema Mgunda ana uwezo wa kucheza mipira ya juu, nguvu ya kukabiliana na mabeki, kucheza kitimu akimtofautisha na Mwalimu aliyemaliza na mabao tisa msimu uliopita, asisti moja akiwa na Simba kwamba anapenda kushambulia akitokea pembeni zaidi kuliko katikati.
“Mwalimu akilishwa mipira vizuri na akapata nafasi ya kucheza basi anaweza akafunga zaidi, lakini kama atashindwa kuklini mapema, uwepo wa wachezaji kama, Peter Shalulile ambao wana uwezo wa kuzunguka uwanja mzima, basi inaweza ikawa changamoto kwake,” amesema Gabriel.
Staa mwingine wa zamani wa Yanga na Stars, Sekilojo Chambua amesema: “Mwalimu atahitaji zaidi alishwe mipira na mawinga ili aweze kufunga sana, kwa sababu siyo mchezaji mwenye mizunguko mingi uwanjani, tofauti na Mgunda ingawa ana mabao machache lakini ana nguvu na ana haha sana uwanjani, endapo akiendana na mifumo ya Simba anaweza akafanya vizuri.”
Beki wa zamani wa Simba, Frank Kasanga amesema: “Ukiona wachezaji wanasajili basi wamefanyiwa tathmini na kuona huduma zao zinafaa kwenye timu, Mgunda ni mshambuliaji mzuri, anachotakiwa ni kupambana ili kuendana na kasi ya Simba, vivyo hivyo na kwa Mwalimu kujua Yanga ina wachezaji wa aina gani ili aweze kupata nafasi.”
Akizungumzia tofauti ya mastaa hao nyota wa zamani wa Yanga Edibily Lunyamila amesema: “Ingawa binafsi naona Simba ilikuwa na uhitaji zaidi na Mwalimu, kwani aliingia katika mfumo ndiyo maana alifunga mabao mengi na ni mchezaji anayekaa zaidi eneo la kufunga, ila kwa Mgunda ana ubora mkubwa uwanjani, ingawa atatakiwa kujituma sana na kujua klabu hiyo inataka nini kutoka kwake.”