Ronaldo, Georgina wafunga ndoa katika harusi binafsi Ureno
Muktasari:
- Wawili hao, ambao wamekuwa pamoja tangu mwaka 2017, walitangaza uchumba wao mwaka mmoja uliopita, tarehe 11 Agosti 2025.
Cristiano Ronaldo amemuoa mwenza wake wa muda mrefu, Georgina Rodríguez, katika sherehe binafsi ya ndoa ya kiserikali iliyofanyika Cascais, Ureno, tarehe 11 Agosti 2026. Harusi hiyo ya kifamilia ilihudhuriwa na watoto wao watano.
Wawili hao, ambao wamekuwa pamoja tangu mwaka 2017, walitangaza uchumba wao mwaka mmoja uliopita, tarehe 11 Agosti 2025.
Ronaldo alithibitisha ndoa hiyo kwa kuchapisha picha ya mikono yao ikiwa na pete za ndoa, pamoja na maelezo mafupi yaliyosomeka “C❤G”.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, na Rodríguez, mwenye miaka 32, ni wazazi wa Alana Martina na Bella Esmeralda.
Watoto wengine watatu wa Ronaldo Cristiano Jr. pamoja na mapacha Eva na Mateopia ni sehemu ya familia yao. Kwa masikitiko, wanandoa hao walimpoteza pacha wa Bella, Angel, muda mfupi baada ya kuzaliwa mwaka 2022.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza Rodríguez alipokuwa akifanya kazi katika duka la Gucci. Uhusiano wao ulianza kujulikana hadharani mwaka 2017, na kwa miaka iliyofuata wamejenga maisha ya kifamilia yanayofuatiliwa kwa karibu na umma.
Rodríguez pia ameonyesha maisha yao ya uhusiano na familia kupitia kipindi chake cha Netflix, I Am Georgina.
Harusi hiyo inaashiria kilele cha karibu muongo mmoja wa maisha yao pamoja, huku wanandoa hao wakichagua sherehe tulivu nchini Ureno badala ya sherehe kubwa na ya hadhara ambayo ilikuwa imezua uvumi mbalimbali hivi karibuni.