Ronaldinho arejea kusaka bao 300
Muktasari:
- Maelfu ya mashabiki walikusanyika katika ufukwe wa jiji hilo kwa ajili ya tukio lililopewa jina la “Ronaldinho Day”, wakistahimili mvua iliyokuwa ikinyesha ili kushuhudia kutambulishwa kwa nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain, Barcelona na AC Milan, ambaye alistaafu soka mwaka 2015.
MILAN, ITALIA: GWIJI wa soka wa Brazil, Ronaldinho ametangaza kurejea uwanjani akiwa na umri wa miaka 46, akijiunga na Ravenna inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Italia (Serie C), huku akitamani kufikisha mabao 300 katika maisha yake ya soka baada ya kufunga mabao 280 hadi wakati anastaafu.
Maelfu ya mashabiki walikusanyika katika ufukwe wa jiji hilo kwa ajili ya tukio lililopewa jina la “Ronaldinho Day”, wakistahimili mvua iliyokuwa ikinyesha ili kushuhudia kutambulishwa kwa nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain, Barcelona na AC Milan, ambaye alistaafu soka mwaka 2015.
Ronaldinho amesema amefurahi kurejea Italia na kuungana na wachezaji wenzake, huku akiamini wanaweza kufanya mambo mazuri msimu huu.
“Je, mtaniona nikicheza? Sijui, hilo analijua kocha pekee. Kurejea Italia ni jambo zuri. Nipo hapa kuwasaidia wenzangu kushinda,” amesema.
Akizungumza kuhusu hali yake ya mwili, Ronaldinho amesema yuko fiti na anajisikia vizuri, huku akifichua kuwa angefurahi zaidi iwapo angefanikiwa kufunga bao lake la 300 katika soka la ushindani.
Ronaldinho alicheza mchezo wake wa mwisho rasmi Septemba 2015 akiwa na klabu ya Brazil, Fluminense, kabla ya kutangaza kustaafu.
Akiwa mchezaji, alishinda Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa na Brazil, akifunga bao la ushindi katika robo fainali dhidi ya England. Pia alitwaa tuzo ya Ballon d'Or mwaka 2005.
Mpango wa kurejea kwake uwanjani ulitangazwa kwa mara ya kwanza Juni na mfanyabiashara raia wa Italia na Marekani, Ignazio Cipriani, ambaye ni mmiliki wa Ravenna tangu mwaka 2024.
Cipriani amesema lengo la Ronaldinho ni la kimapenzi zaidi, akitaka kupata nafasi ya kufunga bao lake la mwisho katika soka.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa Ronaldinho katika klabu hiyo si wa muda mfupi wala haujapangwa kwa ajili ya kutengeneza tu umaarufu au kuitangaza Ravenna.
Hata hivyo, Cipriani alifichua kuwa Ronaldinho hatacheza katika mchezo wa ufunguzi wa msimu wa Serie C dhidi ya Reggiana utakaochezwa Jumatatu.
Ravenna ilimaliza katika nafasi ya tatu katika Kundi B la Serie C msimu uliopita na sasa inalenga kupanda daraja hadi Serie B, ligi ambayo haijacheza tangu mwaka 2008.
Kwa Ronaldinho, kurejea kwake kunaweza kuwa nafasi ya kuongeza sura nyingine katika safari yake ya soka ikiwezekana, kutimiza ndoto ya kufikisha mabao 300 ya ushindani.