Ronaldinho: Messi ndiye bora duniani... hata Mbappe ameukubali mziki
Muktasari:
- Ronaldhino anadai katika kizazi hiki cha soka hakuna mchezaji anayeweza kujilinganisha au kutamba kulingana na Messi, ingawa kwa sasa anaelekea kuutupa mkono mchezo huo kutokana na umri kuanza kumvuta.
MADRID, HISPANIA: KWA miaka mingi, mjadala kuhusu nani ndiye mchezaji bora zaidi duniani umeendelea kutawala ulimwengu wa soka, lakini kwa Ronaldinho Gaucho, gwiji wa soka wa Brazil amekuwa na jibu akisema: “mbona rahisi tu, ni Lionel Messi”.
Ronaldhino anadai katika kizazi hiki cha soka hakuna mchezaji anayeweza kujilinganisha au kutamba kulingana na Messi, ingawa kwa sasa anaelekea kuutupa mkono mchezo huo kutokana na umri kuanza kumvuta.
Gwiji huyo wa soka mwenye moja ya medali za mwisho za ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Brazil, anaweka wazi hata sasa Messi ndiye mchezaji bora duniani, akisisitiza nyota huyo wa Argentina anaendelea kushikilia nafasi hiyo, kwani anaamua mechi muhimu na hata asipofanya hivyo lakini timu pinzani hukiona cha moto kukabiliana naye.
Akizungumza katika mahojiano na Ole, Ronaldinho anasema huo ni msimamo wake alipokuwa akitafakari ubora wa Messi ambao umeendelea kudumu muda mrefu katika maisha yake ya soka.
“Bado ndiye bora duniani,” anasema Ronaldinho aliyewahi kucheza na staa huyo katika kikosi cha Barcelona.
Kauli hiyo ina uzito mkubwa kutokana na hadhi ya Ronaldinho mwenyewe ambaye anatambuliwa kama mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa zaidi katika kizazi chake.
Akiwa Barcelona, Ronaldinho alikuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya awali ya Messi wakati huo akichipukia katika La Masia.
Wakiwa pamoja, Ronaldinho mara nyingi alizungumzia uwezo wa Messi akiwa bado mdogo na hata kutabiri kuwa angekuja kung’ara zaidi siku za usoni, utabiri ambao ulitimia baada ya miaka takribani 10 tangu Mbrazili huyo alipoondoka Barcelona.
Hadi leo, Messi anaendelea kupambana na umri na matarajio, akiwa na klabu au timu ya taifa ya Argentina, kiwango chake bado ni cha juu na kwa mujibu wa Ronaldhino hiyo inatokana na mazoezi, kujituma na kujitunza vitu alivyo navyo mchezaji huyo.
Baada ya kuiongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia 2022, wengi walidhani amefikia kilele cha mafanikio yake. Hata hivyo, badala ya kupoteza kabisa ameendelea kuonyesha ubora na kuimarisha nafasi yake miongoni mwa magwiji wa muda wote wa soka.
Ronaldinho pia anaonyesha matumaini kuhusu mustakabali wa Messi katika timu ya taifa, akidokeza bado anaweza kuwa na mchango mkubwa katika Kombe la Dunia 2026, kutokana na uimara wake wa kimwili na kiakili, sifa ambazo zimekuwa alama ya maisha yake ya soka.
Wakiwa Barcelona, Ronaldinho aliwahi kutoa pasi iliyomwezesha Messi kufunga bao lake la kwanza katika timu ya wakubwa, tukio lililoashiria mwanzo wa enzi mpya wa kijana huyo kutoka Argentina aliyekuja kuifungia timu hiyo mabao zaidi ya 600 katika misimu 18. Tangu hapo, Messi ameandika rekodi nyingi akishinda tuzo nane za Ballon d’Or.
Zaidi ya takwimu na mataji, ushawishi wa Messi umebadilisha namna soka linavyochezwa na kutazamwa. Mtindo wake wa kucheza uliojaa ubunifu, akili ya mchezo na udhibiti wa mpira umehamasisha kizazi cha wachezaji duniani kuupenda kufanya vitu vya kukumbukwa.
Wakati Ronaldinho akiyasema hayo, maneno yake yaliungwa mkono na nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe ambapo amezungumza kwa mara ya kwanza juu ya uhusiano wake na Messi akimtaja kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa waliowahi kuwapo duniani.
Mbappe anayeichezea Real Madrid kwa sasa, alicheza na Messi walipokuwa pamoja katika kikosi cha PSG kati ya mwaka 2021 hadi 2023 na alieleza licha ya kucheza na mshindi huyo mara nane wa Ballon D’or, lakini jamaa ni fundi kwelikweli kwani mpira anaucheza kirahisi sana, lakini kwa uhakika.
Akieleza kwa nini anaamini Messi ni mchezaji bora, Mbappe alitumia maneno yanayoonyesha mshangao mkubwa kuhusu uwezo wa nyota huyo wa Argentina.
Amesema uzoefu wake wa kufanya mazoezi na Messi walipokuwa PSG, ulikuwa wa kiwango cha kipekee kiasi kwamba haamini kama kuna mchezaji wa soka anayemfikia gwiji huyo katika kizazi cha sasa.
Mbappe alikumbushia wakati wa mazoezi ya kupiga mashuti, yeye na Neymar wangefunga mabao kadhaa, lakini Messi angepiga mashuti karibu yote na kufunga kwa usahihi uleule kila mara, kana kwamba ni jambo rahisi.
Kwa mujibu wa Mbappe, jambo la kushangaza zaidi ni jinsi Messi alivyokuwa akifanya hivyo bila hata kuonekana kujituma sana kama anapasia tu mpira wavuni.
Kauli hiyo inaonyesha namna Mbappe alivyoathiriwa na ubora wa Messi, akisisitiza uwezo wake ni wa kipekee na wa kiwango ambacho si rahisi kuelezeka kwa maneno ya kawaida.
Mbappe anayedaiwa kumchukulia nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo, kuwa mchezaji wa kawaida, anadai fursa ya kushuhudia kipaji cha Messi kwa karibu kila siku lilikuwa ni jambo lililomshangaza kwani alivuna ujuzi mwingi kutoka kwa mchezaji huyo.
Kuhusu mchezaji ambaye amewahi kufanya naye mazoezi na ambaye anaamini ni wa “ajabu” katika soka, nyota huyo aliyewahi kucheza na wachezaji wengi wa viwango vya juu duniani, alidai: “Hakuna kama Messi na hatatokea kamwe.”
Akijibu juu ya ubora wa Messi na Neymar, Mbappe amesema: “Sio kitu kilekile, Messi anafanya kila kitu vizuri.”
Kisha alisimulia tukio linaloonyesha uwezo mkubwa wa Messi katika kufunga na ufundi wake wa hali ya juu ambapo Mbappe amesema: “Nitawaambia kisa. Tulikuwa Paris tukifanya mazoezi ya kupiga mashuti ya kumalizia, na wakati huo PSG ilikuwa kileleni mwa soka la dunia. Tulikuwa tukipiga mashuti 10… Mimi na Neymar tungefunga mabao sita au saba. Messi angepiga mashuti tisa na kufunga bao lilelile kila mara, kana kwamba ni mazoezi ya watoto. Alionekana mchovu, kama vile anapasia tu mpira wavuni. Nilimtazama na sikuweza kuelewa.”