Real Betis, Antony sasa mambo ni freshi
Muktasari:
- Inaelezwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 huenda akakubali kupunguza mshahara ili kujiunga na miamba hiyo ya La Liga.
REAL Betis bado ina matumaini ya kumsajili winga wa kimataifa wa Brazil, Antony kutoka Manchester United kwa mkataba wa moja kwa moja baada ya kuvutiwa sana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita alipokuwa akicheza kwa mkopo.
Inaelezwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 huenda akakubali kupunguza mshahara ili kujiunga na miamba hiyo ya La Liga.
Man United inahitaji Euro 40 milioni kama ada ya uhamisho ya Antony kiasi ambacho Betis ipo tayari kukilipa lakini siyo kwa pamoja.
Mpango wa Betis ni kulipa Euro 20 milioni msimu ujao na kiasi kinachobakia kulipa msimu wa 2026/27.
Inaelezwa Antony mwenyewe yupo tayari kurudi tena Betis na ndio timu anayotamani zaidi kujiunga nayo kwa sababu anaamini ataendelea kuonyesha kiwango kilekile alichoonyesha nusu ya msimu uliopita.
Kuhusu mshahara, Antony yupi tayari kipokea kati ya euro 5 hadi 6 milioni kwa mwaka ambazo Betis inaweza kumlipa bila ya shida kutokana na uchumi wao.
Mkataba wa sasa wa staa huyu ambaye ni mmoja kati ya wachezaji watano ambao Man United inawauza katika dirisha hili unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Nayef Aguerd
BEKI wa West Ham na timu ya taifa ya Morocco, Nayef Aguerd, mwenye umri wa miaka 29, yupo kwenye rada za Marseille ya Ufaransa inayohitaji kumsajili katika dirisha hili. Marseille inapambana kuboresha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao kuanzia ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.
Cristian Romero
REAL Madrid ina mpango wa kumsajilj beki kisiki wa Tottenham Hotspur, Cristian Romero, 27, dirisha hili la majira ya kiangazi lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao Atletico Madrid ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza kuingia katika mazungumzo na wawakilishi wake kwa ajili ya kumsajili. Spurs ipo tayari kumruhusu fundi huyu aondoke dirisha hili lakini kwa kiasi kisichopungua pauni 50 milioni.
Ethan Nwaneri
ARSENAL inaamini kiungo wao mshambuliaji anayeichezea pia timu ya taifa ya England kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21, Ethan Nwaneri atasaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye kikosi chao kwa muda mrefu zaidi. Arsenal inapambana kuhakikisha staa huyu anasaini mkataba mpya kwa sababu timu kadhaa hususani Chelsea zimeanza kufanya mazungumzo na wawakilishi wake ili kumsajili.
Victor Osimhen
NAPOLI imesimamisha mazungumzo na Galatasaray kuhusu ada ya uhamisho ya Victor Osimhen, 26, ikielezwa timu hiyo haitojadili tena na kama Galatsaray inahitaji huduma itatakiwa kulipa zaidi ya Euro 70 milioni ambayo ipo katika kipengele cha kuvunja mkataba wake. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Nigeria alicheza Galatasaray kwa mkopo msimu uliopita na akaonyesha kiwango bora.
Romaine Mundle
Sunderland iko katika mazungumzo na winga raia wa England, Romaine Mundle, mwenye umri wa miaka 22, ili kumsainisha mkataba mpya dirisha hili baada ya kuona timu mbalimbali ikiwemo huku PSV Eindhoven zinainyatia saini yake. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Leandro Trossard
KOCHA wa Fenerbahce, Jose Mourinho amewasilisha jina la mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya Ubelgiji, Leandro Trossard, katika orodha ya wachezaji anaohitaji wasajiliwe katika dirisha hili. Inadaiwa Arsenal ipo tayari kumuuza mchezaji huyo mwenye miaka 30 ili kupata pesa itakazoongezea katika usajili wa dirisha hili.
Jamie Vardy
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Leicester City, Jamie Vardy, 38, ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika na aliyekuwa kocha wa West Brom, Carlos Corberan, ambaye sasa ni kocha mkuu wa Valencia.
Corberan amemjumuisha Vardy katika orodha ya mastraika anaowahitaji kwa sababu anavutiwa sana na uchezaji wake na anaamini ataongeza kitu katika timu kutokana na uzoefu wake.