Rais Barcelona ashtukia jambo, atupa kombora Real Madrid
Muktasari:
- Real Madrid itaikaribisha Barcelona kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu katika mechi hiyo, ambayo itaamua hatma ya wenyeji kuendelea kukaa kileleni, au kukubali kushindwa na mahasimu wao endapo watapoteza nyumbani.
Rais wa Barcelona, Joan Laporta, ameishambulia klabu ya Real Madrid kwa madai ya kujaribu kuwatuhumu marefa kabla ya mechi ya El Clásico itakayopigwa leo Jumapili, Oktoba 26, 2025.
Real Madrid itaikaribisha Barcelona kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu katika mechi hiyo, ambayo itaamua hatma ya wenyeji kuendelea kukaa kileleni, au kukubali kushindwa na mahasimu wao endapo watapoteza nyumbani.
Kumekuwa na sintofahamu na utata mwingi kuelekea mechi hii ya El Clásico, na sasa Laporta ameibuka na kuishutumu Real Madrid kwa kujaribu kuingilia uamuzi wa marefa.
Televisheni ya Real Madrid (Real Madrid TV) imekuwa ikiwakosoa marefa wa La Liga mara kwa mara msimu huu, jambo ambalo Laporta amesema halina haki. Pia amesisitiza kwamba Barcelona hawajifanyi wahanga wa tuhuma hizo, na kwamba watajitahidi kushinda tena kwenye Uwanja wa Bernabéu.
Akizungumza na Madrid Universal, kiongozi huyo wa Barcelona amesema: “Hii si njia sahihi ya kufanya ili kurahisisha mechi ya leo. Hicho kinachofanywa na kituo chao cha televisheni kinaathiri marefa kwa kiasi kikubwa sana.
“Tunafahamu ni mbinu ambayo wanaitumia ili waweze kushinda kirahisi, lakini haipaswi kuwa hivyo. Hawawezi kudai kwamba marefa wanawadhuru au wanaipendeleza Barça. Sisi hatujifanyi wahanga, tutajaribu kushinda tena Bernabéu,” amesema Laporta na kuongeza.
“Tumejitayarisha kwa mechi kubwa, tunaamani timu yetu itatupa furaha kubwa katika mechi ya leo kwenye uwanja wa ugenini. Wapinzani wetu wameunda mazingira yasiyofaa kuzunguka timu ya waamuzi, lakini hilo halitowasaidia hata kidogo.”
Kwa sasa, Real Madrid inaongoza msimamo wa La Liga ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi tisa, ikiwa imepoteza mechi moja pekee. Barcelona ina pointi mbili nyuma ya kikosi cha Xabi Alonso, lakini inaweza kupanda kileleni endapo itashinda El Clasico ya leo.
El Clásico inachukuliwa kuwa moja ya mechi zenye upinzani mkali zaidi duniani. Timu hizo zimekutana mara 260 hadi sasa, Real Madrid ikishinda mara 105, huku Barcelona ikishinda mara 104.