Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fei Toto mlangoni Yanga, GSM aweka mzigo


WAKATI dirisha la usajili likibakiza siku 10 kufungwa, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wanaonekana kujiandaa kufanya usajili utakaotikisa soka la Tanzania kwa kumrejesha kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kutoka Azam.


Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kuwa, Yanga bado ina nafasi ya usajili mmoja wa mwisho, huku viongozi wa klabu hiyo wakiamini mchezaji watakayemtambulisha atakuwa gumzo kubwa kwa mashabiki wa soka nchini.

Imeelezwa kuwa, Mfadhili wa Yanga, Ghalib Said Mohammed (GSM), ameweka mezani dau la takribani Sh3 bilioni kwa ajili ya kumshawishi Fei Toto kurejea Jangwani, miaka mitatu baada ya kuondoka na kujiunga na Azam FC.


DILI LA KIHISTORIA

Iwapo usajili huo utakamilika, utakuwa miongoni mwa dili kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika soka la Tanzania.

Fei Toto aliondoka Yanga mwishoni mwa msimu wa 2022-2023 na kujiunga na Azam FC katika uhamisho uliotikisa soka la nchi, huku mvutano mkubwa kati ya klabu hizo ukifikia hatua ya kuhitaji usuluhishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Sasa, Yanga inaonekana kuwa tayari kufanya kila linalowezekana ili kumrudisha kiungo huyo ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na Azam FC.


DAU LA KUFURU

Mbali na dau la Sh3 bilioni, taarifa zinaeleza kuwa Yanga imemuandalia Fei Toto mshahara unaozidi mara mbili anaolipwa Azam FC, pamoja na ahadi ya kumpatia gari jipya la kisasa atakalochagua mwenyewe.

Chanzo cha karibu na familia ya mchezaji huyo kimeeleza kuwa, tayari Fei Toto ameridhia kurejea Yanga ikiwa makubaliano yote yatakamilika.

"Hata sisi familia tumeridhia arudi kama wamekubaliana. Hakuna uhasama wa milele. Kilichopita kimepita, na ukizingatia mpira ni maisha ya muda mfupi, fedha kama hizi ni ngumu kuzikataa," kimesema chanzo hicho.


JEZI NAMBA SITA YAMSUBIRI

Inaelezwa pia kuwa Yanga haijamkabidhi mchezaji mwingine jezi namba sita, namba aliyokuwa akiitumia Fei Toto kabla ya kuondoka, ikiwa ni ishara ya matumaini ya kumrudisha kiungo huyo Jangwani.


KIKWAZO KILICHOBAKI

Hata hivyo, dili hilo bado halijafungwa rasmi.

Taarifa zinaeleza kuwa Fei Toto amewaelekeza viongozi wa Yanga kwenda Zanzibar kuzungumza na mama yake ili kumaliza tofauti zilizojitokeza wakati alipokuwa anaondoka klabuni hapo miaka mitatu iliyopita.

"Wakati wowote kuanzia sasa viongozi wa Yanga watakuja Unguja kuzungumza na mama. Wakati ule kulikuwa na maneno mengi kutoka kwa baadhi ya mashabiki, hivyo kuna haja ya kuweka mambo sawa. Hilo likikamilika, basi safari ya kurejea Yanga itakuwa wazi," kimeongeza chanzo hicho.


AENDELEA NA MAANDALIZI AZAM

Kwa sasa Fei Toto yupo na kikosi cha Azam FC nchini Rwanda kwa maandalizi ya msimu mpya, ingawa hakuhusika katika mchezo wa kirafiki wa hivi karibuni baada ya kuwaeleza viongozi wa klabu kuwa bado hajapona kikamilifu.

Endapo mazungumzo yatafikia makubaliano kati ya pande zote, kurejea kwa Fei Toto, Yanga kutakuwa moja ya usajili mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.