Prime
Presha ya Fei Toto kila usajili
KWA miaka ya karibuni, kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amekuwa akiiteka jamii ya michezo hasa soka kila linapofunguliwa dirisha la usajili hapa nchini. Jina lake limekuwa likihusishwa kutakiwa na klabu kongwe za Simba na Yanga. Pia nje ya mipaka ya Tanzania.
Unaweza ukajiuliza kwa nini Fei Toto! Muendelezo wa kiwango chake ni sababu ya Simba na Yanga kutamani awe sehemu ya vikosi vyao. Inafahamika kabla ya kujiunga na Azam FC mwanzoni mwa msimu wa 2023-2024, alitokea Yanga.
Fei Toto kwa mara ya kwanza kucheza Tanzania Bara alijiunga na Singida United ambako hakucheza na kuhamia Yanga mwaka 2018, aliondoka mwisho wa msimu wa 2023-2024 kwenda Azam alipo sasa.
Baada ya kucheza msimu wa 2022-2023, presha yake ya usajili ikawa kubwa kutoka Yanga kwenda Azam, dili lake lilizua utata mkubwa hadi Rais Tanzania, Samia Suluhu alipoingia kati ndipo ilipokamilika. Tangu hapo, Fei Toto amekuwa akitajwa zaidi kila kipindi cha usajili kinapofika.
Hiyo ilianza baada ya kufanya vizuri zaidi msimu wa 2023-2024 alipomaliza na mabao 19 akiwa nyuma ya aliyekuwa kinara Stephane Aziz KI aliyefunga 21, alirejea katika tetesi za kutakiwa na Simba na Yanga. Pia timu za nje.
Msimu huo licha ya Fei Toto kumaliza mfungaji namba mbili ndani ya Ligi Kuu Bara, pia alikuwa na asisti saba, hivyo alihusika na jumla ya mabao 26.
Msimu wa 2024-2025, alikuwa kinara wa asisti 13, pia alifunga mabao manne, hivyo alihusika na jumla ya mabao 17, kisha 2025-2026, alikuwa na mabao 15 akiwa mfungaji namba mbili nyuma ya Mossi Nduwumwe wa Singida BS aliyemaliza na mabao 17. Ukiacha mabao, Fei Toto alikuwa na asisti tisa.
Fei Toto siyo mchezaji wa kwanza kuwa katika rada za Simba na Yanga kila linapofika dirisha la usajili, kuna wachezaji wengine ambao walikuwa hawakauki kuhusishwa na klabu hizo, kutokana na viwango vyao.
Clatous Chama
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama aliyemaliza na mabao manane, asisti saba msimu uliopita wa 2025/26, 2024/25 alikuwa na mabao sita, asisti tatu, 2023/24 alikuwa na mabao saba asisti sita kutokana na kiwango chake kikubwa aliwahi kuziweka kwenye presha ya usajili klabu kongwe.
Yanga aliyowahi kuichezea msimu wa 2024/24 ilianza kuwinda huduma ya Chama baada ya kuibuka MVP wa Ligi Kuu msimu wa 2019/20 hata baada ya kuachana naye na akaenda kujiunga Singida BS na kilichomrejesha tena kwa Wanamsimbazi Januari 20, 2026 ni kiwango chake.
Fiston Mayele
Kutokana na kiwango alichokionyesha Fiston Mayele wakati akiwa Yanga aliyokuwa amejiunga nayo kwa mara ya kwanza 2021–2023 akitokea AS Vita ya DR Congo, kilifanya awe anahusishwa zaidi kuhamia Simba.
Mayele ambaye ndani ya misimu miwili aliyocheza Yanga (2021/22 alimaliza na mabao 16, 2022/23 mabao 17) alifunga jumla ya mabao 33 baadaye akaenda kujiunga na Pyramids ya Misri, lakini katika usajili unaoendelea bado kulikuwa na fununu za kutakiwa na Simba, hilo linatokana na kiwango chake kikubwa anachokionyesha na hata Yanga pia ilikuwa inatajwa kumrejesha.
Stephane Aziz Ki
Wakati kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki akiwa Yanga msimu wa 2023/24 alikuwa kinara wa mabao 21, asisti nane, 2024/25 alikuwa na mabao tisa, asisti saba, Ki katika usajili wake wa kwanza kuja Tanzania, Wanajangwani waliwahi Wanamsimbazi kumsajili kwani walikuwa wanawania saini yake kwa pamoja.
Max Nzengeli
Japokuwa zilikuwepo tetesi za Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kuzungumza na Max Nzengeli aliyejiunga na Yanga kwa mara ya kwanza 13/07/2023, lakini hakumpa umuhimu baada ya kuonyesha kiwango akiwa na Wanajangwani, bado Wanamsimbazi walirudi kuhitaji huduma yake.
Nzengeli amekuwa na kiwango kizuri ndani ya Yanga msimu wa 2023/2024 alikuwa na mabao 11, asisti mbili, 2024/25 alimaliza na mabao sita, asisti 10 na 2025/26 alikuwa na mabao sita, asisti saba.
Ibrahim Hamad 'Bacca'
Beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Hamad ingawa taarifa zake hazikuwa na presha kubwa, lakini ni mchezaji ambaye mara kadhaa Simba imekuwa ikimpigia rada mara kadhaa kumtaka katika kikosi chake, awamu hii ilibakia kidogo tu, lakini Wanajangwani waliwahi hilo na kuboresha maslahi yake.
KAULI ZA WADAU
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi 'Boban' anasema: "Ukiona mchezaji anawaniwa na timu mbalimbali basi siyo kitu kingine bali ni kiwango chake kuwa juu, hakuna timu ambayo haitamani kuwa na mchezaji muhimu, ndiyo maana unakuta Fei Toto anatajwa kila msimu kuhusishwa na Simba na Yanga."
Mwingine aliyeunga mkono hilo ni kiungo mkabaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Nurdin Bakari alisema: "Japokuwa kuna muda sifuatilii mpira nakuwa na shughuli zangu, ila kwa ishu ya Fei Toto ukiona kila msimu anatakiwa na timu basi ujue kiwango chake ndicho kinachombeba."
Beki wa kati wa zamani wa Yanga, Ladislaus Mbogo alisema: "Ukitaja wachezaji wenye viwango vya juu nchini basi huwezi kuacha kulitaja jina la Fei Toto, hata zamani wakati tunacheza sisi walikuwepo wachezaji wa viwango vya juu waliokuwa wanaleta presha kwenye usajili."