Rafael Benitez arudi kazini Ugiriki
Muktasari:
- Benitez, 65, alikuwa hana kazi yoyote tangu alipoachana na Celta Vigo mwaka 2024 na ataonekana kwenye michuano ya Ulaya baada ya PAO kucheza kwenye Europa League, michuano ambayo alishawahi kunyakua ubingwa.
ATHENS, UGIRIKI: KOCHA, Rafa Benitez amerejea mzigoni baada ya kukubali kuwa kocha mpya wa Panathinaikos.
Benitez, 65, alikuwa hana kazi yoyote tangu alipoachana na Celta Vigo mwaka 2024 na ataonekana kwenye michuano ya Ulaya baada ya PAO kucheza kwenye Europa League, michuano ambayo alishawahi kunyakua ubingwa.
Kocha huyo Mhispaniola amesaini dili nono kwa miamba hiyo ya Ugiriki na hivyo anakuwa kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye historia ya Super League.
Benitez, ambaye aliwahi kuzinoa Liverpool, Chelsea, Newcastle na Everton amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu. Ripoti zinadai kwamba kocha huyo wa zamani wa Real Madrid atakuwa analipwa Pauni 4.4 milioni kwa mwaka.
Benitez alikuwa chaguo la kwanza la rais wa Panathinaikos, Yiannis Alafouzos na mkurugenzi wa klabu hiyo, Franco Baldini.
Benitez, aliyewahi kuinoa pia Inter Milan alisafiri kwenda Athens, Alhamisi iliyopita kwa ndege ya kukodi kumaliza kusaini dili hilo. Alafouzos amempa Benitez kazi ya kuirudisha PAO kwenye chati za juu kwenye soka la Ugiriki baada ya timu hiyo kutoshinda taji lolote tangu 2010 na sasa inajiandaa kuhamia kwenye uwanja wao mpya, Votanikos utakaokamilika 2027.
Panathinaikos ilishawahi kufika fainali ya Kombe la Ulaya mwaka 1971 ilipochapwa 2-0 na Ajax uwanjani Wembley. Ilifika pia nusu fainali na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1996 na 2002 mtawalia. Benitez ataiongoza Panathinaikos kwenye mchezo wa kwanza Jumapili, wakati itakapokabiliana na Asteras Tripolis inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Fulham, Chris Coleman.