PSG yateteza taji la UEFA Super Cup
Muktasari:
- Kwa ushindi huo, PSG imekuwa klabu ya pili katika historia kutwaa UEFA Super Cup mara mbili mfululizo, ikifuata nyayo za Real Madrid iliyofanya hivyo mwaka 2016 na 2017.
SALZBURG, AUSTRIA. Paris Saint-Germain (PSG) imeendelea kutawala soka la Ulaya baada ya kuifunga Aston Villa kwa mabao 2-1 katika mchezo wa UEFA Super Cup uliochezwa Jumatano usiku, Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa Red Bull Arena, Salzburg.
Kwa ushindi huo, PSG imekuwa klabu ya pili katika historia kutwaa UEFA Super Cup mara mbili mfululizo, ikifuata nyayo za Real Madrid iliyofanya hivyo mwaka 2016 na 2017.
PSG imetetea taji ililolitwaa msimu uliopita baada ya kuifunga Tottenham kwa mikwaju ya penalti.
Katika mchezo wa jana usiku ulianza kwa PSG kupata bao la kuongoza dakika ya 20 kupitia Khvicha Kvaratskhelia, aliyefungua kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Aston Villa na kujaa wavuni.
Aston Villa ilisawazisha dakika ya 45 kupitia kinda Brian Madjo, mwenye umri wa miaka 17, aliyefunga baada ya kupokea krosi ya nahodha John McGinn.
Bao hilo lilimfanya Madjo kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga katika historia ya UEFA Super Cup.
PSG ilirejea kwenye uongozi dakika ya 61 kupitia Desire Doue, aliyefunga baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Ousmane Dembele. Bao hilo lilipitiwa na mfumo wa VAR kabla ya kuthibitishwa kuwa halali.
Licha ya Aston Villa kupambana kwa nguvu na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, haikuweza kupata bao la kusawazisha hadi filimbi ya mwisho.
Ushindi huo unaendelea kuonyesha ubabe wa kocha wa PSG, Luis Enrique, katika soka la Ulaya, huku mabingwa hao wakijiandaa kwa mchezo mwingine wa fainali dhidi ya Lens Jumapili ijayo.