Mchezaji atangazwa amekufa, aamka ‘mochwari’
Muktasari:
- Ozor alianguka ghafla katika dakika za mwanzo za mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu dhidi ya Niger Tornadoes, hali iliyowatia hofu mashabiki wa Katsina United.
KATSINA, NIGERIA: Mchezaji wa Katsina United, Chinedu Ozor, anapigania uhai katika Hospitali ya General Katsina baada ya tukio la kushangaza, ambapo alitangazwa kuwa amefariki dunia na baadaye kuonekana akisogeza mkono akiwa mochwari.
Ozor alianguka ghafla katika dakika za mwanzo za mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu dhidi ya Niger Tornadoes, hali iliyowatia hofu mashabiki wa Katsina United.
Baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari waliokuwapo, beki huyo alitangazwa kuwa amefariki dunia.
Hata hivyo, wahudumu wa afya walipigwa na butwaa baada ya Ozor kuonekana akisogeza mkono akiwa tayari amepelekwa mochwari.
Mchezaji huyo wa Nigeria alikimbizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya General Katsina, ambako amewekewa oksijeni huku madaktari wakijitahidi kumrejeshea hali yake na kuhakikisha anakuwa katika hali salama.
Heartland, moja ya klabu ambazo Ozor amewahi kuzichezea, ilitoa taarifa iliyowashangaza mashabiki.
Taarifa hiyo ilisema: “Taarifa za kuaminika zinasema Chinedu Ozor amehamishwa kutoka mochwari kwenda hospitalini baada ya kuripotiwa kuonyesha dalili za kusogea.
“Kwa sasa amewekewa oksijeni huku madaktari wakifanya kila wawezalo kumrejeshea hali yake.”
Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Katsina United awali kutangaza kupitia mitandao ya kijamii kwamba Ozor alikuwa amefariki dunia.
Katika taarifa yao ya awali, klabu hiyo ilisema: “Tunaomboleza kifo cha kusikitisha cha mchezaji wetu mpya, Chinedu Ozor, kufuatia tukio la kiafya lililotokea katika mchezo wa kirafiki wa leo dhidi ya Niger Tornadoes.
“Mawazo, dua na nguvu zetu ziko pamoja na familia yake na wapendwa wake. Pumzika shujaa.”
Ofisa wa habari wa Katsina United, Nasir Gide, amesema Ozor alikimbizwa hospitalini baada ya kuanguka uwanjani na kuthibitishwa kuwa amefariki na daktari.
“Tulipomkimbiza katika hospitali iliyokuwa karibu, daktari alithibitisha kuwa amefariki.
“Tulipata ripoti ya polisi na kumpeleka tena katika Hospitali ya General Katsina, ambako pia ilielezwa kuwa amefariki,” amesema Gide.
Taarifa za awali za kifo chake zilipelekea Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL) pamoja na Kano Pillars, moja ya klabu alizowahi kuzichezea, kutoa salamu za pole kwa familia na wapenzi wa soka.
Mkurugenzi Mkuu wa Rivers United, Okey Kpalukwu, pia alitoa salamu za pole baada ya taarifa hizo kusababisha mshtuko mkubwa katika soka la Nigeria.
Amesema: “Tunatoa pole za dhati kwa familia yake, wapendwa wake, uongozi, wachezaji, wafanyakazi na mashabiki wa Katsina United.
“Mawazo na dua zetu ziko pamoja na familia nzima ya soka la Nigeria katika kipindi hiki kigumu.”
Ozor alijiunga rasmi na Katsina United mapema mwezi huu, wakati klabu hiyo ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya.
Kwa sasa, macho ya familia, klabu na mashabiki wa soka nchini Nigeria yameelekezwa katika Hospitali ya General Katsina, zikisubiri taarifa zaidi kuhusu hali yake.