Sura tatu za Feisal Salum
Muktasari:
- Simba inatajwa kumhitaji kuongeza ubora katika kikosi, Yanga inataka kumrudisha Jangwani huku Azam ikitaka kumbakiza mchezaji huyo mwenye mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo unaomalizika mwishoni mwa 2026-2027.
SAKATA la Feisal Salum ‘Fei Toto’ limeingia kwenye saa zake za mwisho wakati dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa Agosti 15, 2026 huku kiungo huyo akiwa katikati ya mjadala wa klabu tatu kubwa za Tanzania.
Simba inatajwa kumhitaji kuongeza ubora katika kikosi, Yanga inataka kumrudisha Jangwani huku Azam ikitaka kumbakiza mchezaji huyo mwenye mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo unaomalizika mwishoni mwa 2026-2027.
Jina la Feisal limeendelea kutawala mijadala ya usajili katika siku hizi za mwisho, hasa baada ya Yanga kuonyesha nguvu kwenye soko kwa kumnasa Selemani Mwalimu kwa mkopo wa msimu mmoja kutoka Wydad Casablanca.
Mshambuliaji huyo alikuwa kwenye mipango ya Simba kwa msimu ujao na alionekana kwenye kambi ya timu hiyo, lakini Yanga iliingia kwenye mazungumzo na waajiri wake na kukamilisha dili haraka.
Hatua hiyo imeifanya Simba kuangalia namna nyingine ya kuongeza makali kwenye kikosi na Feisal sasa anatajwa kuwa miongoni mwa majina yanayopewa uzito katika mipango hiyo. Simba pia inatajwa kuwa katika hatua nzuri ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji mwingine mzawa, Ismail Mgunda kutoka Mashujaa huku taarifa zikieleza klabu hiyo na mchezaji wamefikia makubaliano.
Hata hivyo, changamoto katika suala la Fei ipo kwa Azam kwa sababu bado ina mkataba naye na imeonyesha nia ya kubaki naye. Wakati huohuo, Yanga inatajwa kuwa tayari kumrudisha Jangwani baada ya kuondoka mwishoni 2022-2023.
Kwa hiyo, kinachosubiriwa ni nani ataweza kufikia makubaliano ya mwisho kabla ya muda wa dirisha la usajili kumalizika.
Sakata la Feisal linavutia kwa sababu kila moja ya timu hizo tatu ina sababu ya kumhitaji. Simba inatafuta mchezaji anayeweza kuongeza ubunifu na mabao katika eneo la kiungo mshambuliaji. Yanga inataka kuongeza nguvu kwenye kikosi ambacho kina wachezaji wengi wenye uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi, wakati Azam inataka kuhifadhi sehemu muhimu ya kikosi chake katika mpango wa kuingia kwenye vita ya ubingwa msimu ujao. Kwa maana hiyo, uamuzi wa Fei hautakuwa tu kuhusu kubadilisha klabu, bali unaweza kuwa na athari kwenye namna ambavyo timu hizo tatu zitakavyoshindana katika msimu mpya.
SIMBA ITANOGA
Kumhusisha Fei na Simba siyo jambo lililoanza leo. Kama Feisal akiingia Simba moja ya maeneo ambayo yangepata nguvu zaidi ni kiungo mshambuliaji. Msimu uliopita, Simba ilimtegemea Clatous Chama kuunganisha kiungo na safu ya mbele huku akifunga mabao manane na asisti saba katika Ligi Kuu Bara.
Feisal akiwa Azam alimaliza akiwa na mabao 15 na asisti tisa. Takwimu hizo zinaonyesha tofauti muhimu, kwamba Fei siyo mchezaji anayefanya kazi ya kutengeneza nafasi pekee, bali ana uwezo pia wa kuingia eneo la hatari na kutumia nafasi anazopata.
Ujio wa Feisal Msimbazi unaweza pia kuongeza ushindani na ubora eneo la mbele kutokana na wachezaji ambao Simba tayari i nao. Pembeni kuna Anicet Oura, Libasse Gueye, Elie Mpanzu na Keletso Makgalwa huku eneo la ushambuliaji ikiwa na Ibrahim Doumbia. Ikiwa pia usajili wa Mgunda kutoka Mashujaa utakamilika kama unavyotajwa, Simba itakuwa na machaguo zaidi safu ya mbele.
Katika mazingira hayo, Fei angecheza nyuma ya mshambuliaji, akitumia nafasi kati ya mistari huku wachezaji wa pembeni wakitoa upana na mshambuliaji akivuta mabeki.
Jambo jingine linalomfanya Feisal kuwa mchezaji anayevutia kwa Simba ni uwezo wake wa kucheza zaidi ya nafasi moja. Ingawa anajulikana zaidi kama kiungo mshambuliaji au namba 10, anaweza pia kutumika katika eneo la mwisho la ushambuliaji inapohitajika.
Hili ni jambo linaloweza kuwa muhimu kwa Kocha Steve Barker kutokana na changamoto ambazo Simba ilikuwa nazo msimu uliopita, alipofikia hatua ya kumtumia Elie Mpanzu kama mshambuliaji na akaonyesha uwezo wa kufanya kazi hiyo.
BALAA JANGWANI
Kwa Yanga, kurejea kwa Fei kutakuwa na maana tofauti kwa sababu tayari ana historia na klabu hiyo.
Yanga tayari imeboresho safu ya ushambuliaji na baada ya kumnasa Mwalimu kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ina wachezaji kadhaa wanaoweza kutumika eneo hilo akiwemo Peter Shalulile, Clement Mzize, Hussein Mihambo na Cheick Toure.
Hivyo, kama Fei atatua ataingia kwenye kikosi ambacho tayari kina uwezo mkubwa wa kushambulia. Changamoto kubwa kwa kocha Manqoba Mngqithi itakuwa namna ya kumtumia Fei pamoja na Allan Okello.
Mngqithi atatakiwa kuwaweka Feisal na Okello kwenye mfumo mmoja kwa kuwapa majukumu tofauti. Mmoja angeweza kucheza kama namba 10 anayepokea mpira kati ya mistari, wakati mwingine akawa na uhuru wa kusogea zaidi eneo la mwisho. Chaguo jingine linaweza kutumia mmojawao katika eneo la pembeni au kumrudisha mmoja zaidi kwenye kiungo ili kuongeza uwiano wa timu. Jambo lingine linaloweza ni historia ya Fei ya kucheza katika mazingira yenye presha kubwa.
Mchezaji huyo tayari anafahamu ukubwa wa klabu hiyo na ushindani wa mechi zake, hivyo hatahitaji muda mrefu kuzoea.
MTAOMBA POO
Kama uongozi wa Azam utambakisha Fei utakuwa umehifadhi mchezaji aliyekuwa miongoni mwa vinara wa kikosi chake msimu uliopita.
Fei alimaliza akiwa na mabao 15 na asisti tisa, hivyo kupoteza mchango huo bila kupata mbadala wa kiwango sawa kunaweza kuathiri mipango ya kocha Florent Ibenge.
Kocha huyo ana uzoefu wa kujenga timu zinazocheza kwa ushindani na kama atapata kikosi chenye uimara katika kila eneo, Azam inaweza kuingia kwenye msimu mpya ikiwa tishio kubwa zaidi.
Katika mazingira hayo, Feisal anakuwa sehemu muhimu kwa sababu anaweza kuunganisha kiungo na ushambuliaji, kufunga mwenyewe na pia kutengeneza nafasi. Kumbakisha kutaifanya timu hiyo isilazimike kuanza upya kutafuta mchezaji wa kuziba pengo lake wakati muda wa usajili ukiwa umesalia kidogo.
Lakini kama Azam itambakisha Feisal, kuna uwezekano kiungo huyo akaondoka bure mwisho wa msimu ikitokea amegomea kuongeza mkataba kwani Juni 30, 2027, mkataba wake na Azam unafikia tamati.
MHOLANZI ATIA NENO
Kocha wa zamani wa Yanga na Azam, Mholanzi Hans van der Pluijm anaamini Fei ni miongoni mwa viungo washambuliaji bora, hivyo siyo jambo la kushangaza kuona jina la mchezaji huyo likihusishwa na Simba na Yanga.
“Niwe mkweli Feisal ni kati ya wachezaji ambao nimekuwa nikiwapenda binafsi. Ana kila kitu na kuhusishwa na Simba na Yanga ni kitu cha kawaida kwa sababu ni mchezaji ambaye anafanya vizuri. Kwangu namuona kuwa ni mchezaji mwenye ubora wa kucheza popote kwenye timu hizo,” alisema kocha huyo.