PSG yamng’oa Messi kibabe Kombe la Dunia la Klabu

Muktasari:
- Messi mwenye rekodi ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mara nane, alishindwa kulizuia chama lake hilo la zamani la PSG katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande mmoja hasa kipindi cha kwanza ambapo wababe hao wa Ufaransa walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.
ATLANTA, MAREKANI: SAFARI ya Lionel Messi katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu inayoendelea nchini Marekani imefikia tamati baada ya timu anayoichezea kwa sasa, Inter Miami ya Marekani jana usiku kufumuliwa mabao 4-0 na PSG na kung’oka katika hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.
Messi mwenye rekodi ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or mara nane, alishindwa kulizuia chama lake hilo la zamani la PSG katika mechi hiyo iliyokuwa ya upande mmoja hasa kipindi cha kwanza ambapo wababe hao wa Ufaransa walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.
Nyota huyo wa Argentina sambamba na swahiba wake, Luis Suarez walishiriki michuano hiyo kama zali kupitia tiketi ya uenyeji, lakini walishindwa kuivusha timu hiyo kwenda robo fainali kutokana na PSG kuwakimbiza mwanzo mwisho na kuiacha ipenye robo fainali kibabe ikizifuata Chelsea ya England na Palmeiras ya Brazili zilizofuzu mapema juzi usiku dhidi ya Batagogo na Benfica.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Wilton Sampaio kutoka Brazili kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Atlanta, PSG ilipata mabao kupitia kwa Joao Neves aliyefunga mawili katika dakika ya 6 na 39 akimalizia pasi za Vitinha na Fabio Luis kabla ya Tomas Aviles aliyeingia katika dakika ya 19 kumpokea Noah Allen aliyeumia, kujifunga dakika ya 44 katika harakati za kuokoa shuti la Desire Doue.
Wakati Miami ikijiuliza namna ya kurejesha mabao hayo matatu, sekunde chache kabla ya mapumziko Achraf Hakimi alikwamisha chuma cha nne.
Mabao hayo yalidumu kwa dakika 45 za kipindi cha pili licha ya kipindi hicho Messsi na wenzake kuonyesha kiu ya kutaka kuyachomoa, lakini umakini wa ngome ya PSG uliwanyima fursa hiyo hadi filimbi ya mwisho ikiwa imelala mabao 4-0.
PSG ilikuwa inasikilizia mshindi wa mchezo uliofuata usiku wa jana kati ya Bayern Munich ya Ujerumani na Flamingo ya Brazili, ili kujua itakayocheza nayo siku ya Julai 5 katika mechi ya robo fainali kwenye uwanja huo huo iliyopata ushindi mbele ya Inter Miami.
Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi moja tu ya 16 Bora kati ya Inter Milan ya Italia na Fluminense ya Brazili itakayopigwa saa 4:00 usiku na alfajiri ya kesho Jumanne, Manchester City ya Englnd itamalizana na Al Hilal ya Saudi Arabia kabla ya saa 4:00 usiku Real Madrid ya Hispania na Juventus ya Italia kufunga hesabu za hatua hiyo ili kupisha mechi za robo fainali.