PSG, Barcelona, Arsenal kwenye vita kali ya ubingwa wikiendi hii
Muktasari:
- PSG itawakaribisha Stade Brestois kwenye dimba la Parc des Princes usiku wa Jumapili huku ikibebwa na rekodi nzuri nyumbani.
PARIS/BARCELONA: BAADA ya kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa, mabingwa watetezi wa Ligue 1, Paris Saint-Germain wapo bize wikiendi hii kupigania taji lao la tano mfululizo la Ligi Kuu Ufaransa huku Barcelona nao wakiwa na hesabu kali dhidi ya Real Madrid wakati huo Arsenal na Manchester City wakitegeana kwenye mbio za ubingwa wa EPL.
Hiki ni kipindi cha kufunga hesabu katika ligi nyingi kubwa barani Ulaya ambapo kila mechi imekuwa na presha kubwa ya kuamua hatima ya ubingwa, nafasi za kucheza michuano ya Ulaya pamoja na vita ya kushuka daraja. Kwa upande wa Italia na Ujerumani, Inter Milan na Bayern Munich tayari wameshafanya yao kwa kutwaa mataji ya ligi hizo lakini vita kali bado ipo kwa timu zinazowania tiketi za Ulaya.
PSG itawakaribisha Stade Brestois kwenye dimba la Parc des Princes usiku wa Jumapili huku ikibebwa na rekodi nzuri nyumbani.
Kikosi hicho cha kocha Luis Enrique hakijachemka kufunga katika mechi zake 49 za nyumbani za Ligue 1, jambo linaloonyesha namna walivyo imara mbele ya mashabiki wao.
Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Bayern Munich katikati ya wiki kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, PSG sasa inarejea kwenye mashindano ya ndani ikiwa kileleni mwa msimamo kwa pointi 70, tofauti ya pointi sita dhidi ya Lens wanaoshika nafasi ya pili.
Endapo Lens watateleza kwenye mchezo wao wa wikiendi na PSG wakaibuka na ushindi mbele ya mashabiki wao, hatua hiyo inaweza kuwakaribisha rasmi kwenye ubingwa mwingine wa Ligue 1 kabla hata ya msimu kumalizika.
Katika mechi zao za hivi karibuni nyumbani, PSG imekuwa moto wa kuotea mbali kwa wapinzani wake. Kabla ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Lorient, mabingwa hao walikuwa wameshinda michezo mitano kati ya sita ya mwisho Parc des Princes huku wakionyesha uwezo mkubwa wa kushambulia.
Kwa upande wa Brest, mambo si mazuri hata kidogo. Timu hiyo imeingia kwenye mfululizo wa mechi sita bila ushindi katika Ligue 1, ikitoa sare mbili na kupoteza nne. Wiki iliyopita walichapwa mabao 4-0 na Paris FC katika mchezo uliowaacha mashabiki wao wakiwa na maswali mengi kuhusu kiwango cha timu hiyo.
Mbali na matokeo mabaya, Brest pia imekuwa dhaifu ugenini ambapo imeshinda mechi moja pekee kati ya 10 za mwisho za ugenini. Katika mechi zao nne zilizopita wamefungwa mabao 10, hali inayoongeza hofu ya kupata kipigo kingine kizito mbele ya PSG.
Historia pia ipo upande wa PSG. Miamba hiyo ya Paris haijapoteza dhidi ya Brest katika mechi 33 mfululizo kwenye michuano yote, wakishinda 25 na kutoka sare nane. Rekodi hiyo ni moja ya rekodi zao bora kabisa dhidi ya timu yoyote nchini Ufaransa.
Macho ya wengi katika mchezo huo yataelekezwa kwa nyota wa PSG, Khvicha Kvaratskhelia ambaye tangu mwezi Machi amehusika kwenye mabao 13 katika mashindano yote akiwa amefunga tisa na kutoa pasi nne za mabao.
Huko Hispania, macho yote yatakuwa kwenye mchezo mkubwa wa El Clasico ambapo Barcelona watawakaribisha Real Madrid katika pambano linaloweza kuamua ubingwa wa La Liga.
Barcelona wanahitaji pointi moja pekee kutangaza ubingwa wao wa 29 wa ligi hiyo huku Madrid wakihitaji ushindi ili kuendelea kuwa na matumaini ya mwisho ya kufufua mbio za taji.
Kikosi cha kocha Hansi Flick kipo kwenye kiwango bora baada ya kushinda mechi 10 mfululizo za La Liga huku pia kikiwa na nafasi ya kumaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote wa nyumbani.
Kwa upande wa Real Madrid, presha imeendelea kuongezeka ndani na nje ya uwanja. Licha ya ushindi wao dhidi ya Espanyol wiki iliyopita, bado wameendelea kukumbwa na mijadala kuhusu kiwango cha baadhi ya nyota wao akiwemo Kylian Mbappé.
Nchini England, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England nazo zimechukua sura mpya huku Arsenal na Manchester City wakitegeana. City watakuwa nyumbani dhidi ya Brentford wakijaribu kupunguza pengo dhidi ya Arsenal wanaoendelea kuongoza ligi.
Kikosi cha Pep Guardiola kilipoteza pointi muhimu baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Everton, matokeo yaliyofanya mbio za ubingwa kuwa ngumu zaidi kwa mabingwa hao watetezi.
Arsenal wao watakuwa na kazi ngumu dhidi ya West Ham United katika dabi ya London yenye presha kubwa kwa pande zote mbili.
Wakati Arsenal wakisaka ushindi wa kuendelea kubaki kileleni, West Ham wanapambana kujiokoa kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.
Kwa ujumla, wikiendi hii inaonekana kuwa ya moto katika soka la Ulaya huku vigogo mbalimbali wakipambana kwa nguvu kuhakikisha wanafikia malengo yao kabla ya pazia la msimu halijafungwa rasmi.