Arsenal, Mikel Arteta kuanza mazungumzo baada ya fainali
Muktasari:
- Kwa sasa, Arsenal iko mbioni kuwania ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya England (EPL) tangu mwaka 2004, ikiwa imebakiza mechi tatu pekee huku ikichuana na Manchester City.
LONDON, ENGLAND: UONGOZI wa Arsenal unajiandaa kufanya mazungumzo na kocha wao, Mikel Arteta, kuhusu mkataba mpya utakaosainiwa mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa na nia ya dhati ya kumfanya abaki klabuni hapo kwa muda mrefu zaidi.
Arteta (44), ambaye mkataba wake wa sasa wa pauni milioni 10 kwa mwaka unatarajiwa kumalizika Juni 2027, ameiwezesha Arsenal kufika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya miaka 20, kufuatia ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Atletico Madrid.
Ripoti kutoka gazeti la The Times zinaeleza kuwa, viongozi wa juu wa Arsenal wanaunga mkono juhudi za Arteta, hasa baada ya klabu hiyo kuwekeza zaidi ya pauni milioni 700 (Sh2.47 trilioni) kwenye soko la usajili tangu alipochukua mikoba mwaka 2019. Licha ya kuwa taji lake pekee hadi sasa ni lile la Kombe la FA la mwaka 2019, maendeleo yaliyoonekana chini ya uongozi wake yameleta matumaini makubwa klabuni hapo.
Kwa sasa, Arsenal iko mbioni kuwania ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya England (EPL) tangu mwaka 2004, ikiwa imebakiza mechi tatu pekee huku ikichuana na Manchester City.
Baada ya kurejea kwenye mashindano makubwa ya Ulaya msimu wa 2023-24, Arteta ameiongoza Arsenal kupanda ngazi kutoka hatua ya robo fainali, nusu fainali, na sasa fainali ambapo itakutana na PSG jijini Budapest, Hungary, Mei 30, 2026. Hii ni fursa adhimu kwa ‘The Gunners’ kulipiza kisasi dhidi ya PSG iliyowaondoa katika hatua ya nusu fainali msimu uliopita.
Akizungumzia mustakabali wake, kiungo huyo wa zamani wa Everton na kocha msaidizi wa Pep Guardiola, amesema kwa sasa akili yake yote ipo kwenye kumaliza msimu kwa mafanikio.
"Hakuna habari mpya kuhusu hilo kwa sasa. Mtazamo wetu upo kwenye kile tunachopaswa kufanya kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Nina furaha, familia yangu iko vizuri, na bado nina hamu kubwa ya kufanikisha mambo makubwa na klabu hii," amesema Arteta aliyewahi kuwa nahodha wa Arsenal chini ya Kocha Arsene Wenger.
Hapo awali, Arteta alikuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Barcelona, lakini amesisitiza kujitolea kwake kikamilifu katika mradi wa Emirates. Hadi sasa, ameshaiongoza Arsenal katika mechi 348, huku akibadilisha taswira ya timu hiyo kutoka kwenye miaka ya kusuasua hadi kuwa washindani wa kweli wa mataji.