Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Twiga Stars inapenya hivi WAFCON 2026

TWIGA Pict

Muktasari:

  • Twiga Stars imepangwa kundi B na Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso, wengi wanaliita kama kundi la kifo kutokana na timu alizopangwa nazo. Lakini je, kweli hakuna njia ya Stars kuvuka?

KAMA kuna timu ambayo imepewa kundi gumu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026, basi ni Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars.

Twiga Stars imepangwa kundi B na Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso, wengi wanaliita kama kundi la kifo kutokana na timu alizopangwa nazo. Lakini je, kweli hakuna njia ya Stars kuvuka?

Tanzania inaingia kwenye mashindano hayo ikiwa ni miongoni mwa timu zisizopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, lakini inaweza kuishangaza Afrika mwaka huu.

Kinachofanya isipewe nafasi kubwa ya kufanya vizuri ni historia yake ya nyuma. Stars imecheza WAFCON mbili mwaka 2010 na 2022 na zote iliishia hatua ya makundi.

Lakini Stars hii imekwenda Morocco ikiwa na wachezaji wenye uzoefu wa ligi mbalimbali duniani na benchi la ufundi lililosheheni makocha wenye ubora mkubwa wa kusaidia timu kuandika historia mpya kwenye mashindano hayo.

TWIG 01

AFRIKA KUSINI

Hakuna ubishi ndiyo kipimo kikubwa zaidi katika kundi hili. Banyana Banyana ni miongoni mwa timu bora Afrika kwa zaidi ya muongo mmoja na walitwaa ubingwa wa WAFCON mwaka 2022.

Kikosi chao kina uzoefu wa kucheza Kombe la Dunia mara mbili mwaka 2019 nchini Ufaransa hii ilikuwa mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo wakapoteza mechi zote tatu za makundi dhidi ya Hispania 3-1, China 1-0 na Ujerumani 4-0.

Mwaka 2023 iliandika histori ya kuvuka hatua ya 16 bora mashindano yaliyofanyika Australia na New Zealand.

Hapa Stars ina kazi ya kufanya mbele ya Afrika Kusini ambayo imeweka rekodi mbalimbali kwenye michuano ya Wafcon. Ndiyo timu iliyoshiriki mara nyingi zaidi kwenye michuano hiyo, mara 13.

Mbali na ubingwa timu hiyo imeibuka mshindi wa pili wa WAFCON mara tano (1995, 2000, 2008, 2012 na 2018).

Timu hiyo inamtegemea mshambuliaji wake hatari, Thembi Kgatlana anayekipiga Tigres UANL ya Mexico, ligi moja na kiungo wa Tanzania, Enekia Lunyamila anayeitumikia Querétaro.

Mshambuliaji huyo ana kasi na anapenda kushambulia maeneo ya pembeni kabla ya kuingia ndani. Akipewa nafasi moja tu anaweza kubadili mchezo. Pembeni yake yupo Linda Motlhalo, kiungo anayepunguza tempo ya mchezo na kutengeneza nafasi za mabao.

Lakini pamoja na ubora huo, Afrika Kusini ina udhaifu ambao Twiga inaweza kuutumia. Mara nyingi timu hiyo inapopanda kushambulia huacha nafasi kubwa nyuma ya mabeki wa pembeni.

Stars inaenda kukutana na Banyana hii ikiwa mara tatu sasa ni wazi tayari inaifahamu timu hiyo baada ya kupangwa na kucheza nao WAFCON zote mbili zilizopita.

Twiga ikiwa na nidhamu ya kujilinda na kutumia mashambulizi ya kushtukiza kupitia mawinga wake inaweza kupata kitu kutoka kwa vijana hao wa ardhi ya Soweto.

TWIG 02

IVORY COAST

Kwenye mashindano hayo Ivory Coast si timu inayozungumzwa sana kama Nigeria au Morocco, lakini ndani ya uwanja ni moja ya timu zinazocheza kwa nguvu na kasi.

Tanzania na Ivory Coast zimewahi kukutana mara mbili katika mechi za mashindano ya CAF, huku Ivory Coast ikishinda zote mbili kwa jumla ya mabao 3-0.

Rekodi hiyo inaonyesha Twiga bado haijaipata njia ya kuifunga timu hiyo, lakini tofauti ya sasa ni kikosi cha Tanzania kina uzoefu mkubwa zaidi kuliko kilivyokuwa miaka ya nyuma.

Licha ya kutokuwa kwenye ramani ya WAFCON kwa zaidi ya muongo mmoja, Ivory Coast si timu ya kubezwa. ‘The Elephants’ wanarejea fainali za mwaka 2026 wakiwa na kumbukumbu ya kumaliza nafasi ya tatu mwaka 2014, ambayo ndiyo mafanikio makubwa zaidi katika historia yao lakini pia imeshiriki michuano hiyo mara nne (2010, 2012, 2014,2026).

Hatari kubwa ya Ivory Coast ipo kwa Rosemonde Kouassi, winga anayejulikana kwa kasi na uwezo wa kuwapita mabeki.

Mbele yake yupo Inès Konan, mshambuliaji anayejua kutafuta nafasi ndani ya boksi na kutumia makosa madogo ya mabeki.

Hata hivyo, udhaifu wa Ivory Coast ni kwamba inapokabiliwa na timu zinazocheza kwa umiliki wa mpira huwa inapoteza mpangilio eneo la kiungo.

Hapo ndipo Twiga inaweza kutumia uwezo wa viungo wake Diana Msewa na Donisia Minja kutuliza mchezo na kuwafanya wapinzani wakimbizane na mpira.

TWIG 03

BURKINA FASO

Ingawa Burkina Faso haina historia ndefu katika WAFCON, ‘Stallions Ladies’ wanashiriki fainali kwa mara ya pili baada ya kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 2022.

Kwenye ushiriki wao wa kwanza tu waliondolewa hatua ya makundi, safari yao ya kufuzu WAFCON 2026 imeonyesha mabadiliko makubwa baada ya kushinda mechi zote nne za hatua ya mchujo dhidi ya Burundi na Togo.

Mchezaji wa kwanza wa kuchungwa ni nahodha Aïssata Traore, mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi. Wa pili ni Alimata Bélem, beki mwenye nguvu na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.

Burkina Faso ina faida ya kucheza kwa nidhamu kubwa ya kujihami, lakini inapokutana na timu zinazobadilisha haraka muelekeo wa mashambulizi huonekana kupata tabu.

Hapo ndipo kasi ya washambuliaji wa Twiga Opah Clement, Stumai Abdallah na Clara Luvanga inaweza kubadilisha mechi.

TWIG 04
TWIG 04

TWIGA INA NINI CHA ZIADA?

Ingawa wengi hawaipi nafasi kubwa, Twiga Stars inaingia Morocco ikiwa na kikosi kilichoiva zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2024.

Nahodha Opah Clement ameendelea kuwa kiongozi wa safu ya ushambuliaji, huku Clara Luvanga akibeba matumaini ya kutengeneza na kufunga mabao.

Mechi za maandalizi pia zimemsaidia kocha kuona mapungufu yaliyokuwepo, hasa kwenye mipira iliyokufa.

Nahodha Opah Clement amekiri wazi kuwa eneo hilo lilikuwa tatizo katika mechi za kirafiki, lakini limefanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa kuelekea WAFCON.

Kitu kingine kinachoweza kuipa Twiga nafasi ni kutokuwa na presha. Afrika Kusini inaingia ikiwa inapewa nafasi ya kutwaa ubingwa, Ivory Coast inahitaji kurejesha heshima yake, huku Burkina Faso ikitaka kuandika historia mpya. Tanzania pekee ndiyo inaingia ikiwa wengi hawaitarajii kufanya makubwa.

Mara nyingi katika mashindano makubwa, timu ambazo hazipewi nafasi ndizo huandika historia.

Ndiyo maana, licha ya ugumu wa Kundi B, bado kuna sababu ya Watanzania kuamini kuwa Twiga Stars inaweza kufanya jambo ambalo haijawahi kulifanya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya ushiriki wake WAFCON.


WASIKIE HAWA

Kiungo kinda wa Twiga Stars, Elizabeth Chenge, anasema: “Hii ni WAFCON yangu ya kwanza, natamani kupafomu kwa kiwango kikubwa na kuandika historia kwenye mashindano hayo ambayo tunaamini sisi kama wachezaji tukipambana tunaweza kufanya vizuri.”

Nahodha wa Twiga Stars, Opah Clement, anasema: “Ni mashindano makubwa sisi kama wachezaji tuko vizuri na tunaamini tunaweza kufanya kitu kikubwa kwenye mashindano haya kwa sababu tuna timu nzuri na tumekuwa na maandalizi mazuri.”