Rekodi nane zinazosubiriwa WAFCON 2026
Muktasari:
- Kila mwaka wa mashindano huwa na simulizi ya aina yake. Wapo wanaocheza kutafuta ubingwa, wengine wanawania heshima ya taifa, lakini kuna kundi lingine linaloingia uwanjani likisaka kuandika historia mpya.
FAINALI za Mataifa ya Afrika kwa wanawake mwaka 2026, zimekuja tofauti kabisa kuanzia kwenye ongozeko la timu hadi pesa za washindi.
Kila mwaka wa mashindano huwa na simulizi ya aina yake. Wapo wanaocheza kutafuta ubingwa, wengine wanawania heshima ya taifa, lakini kuna kundi lingine linaloingia uwanjani likisaka kuandika historia mpya.
Ndivyo ilivyo kwa WAFCON 2026 itakayoanza Julai 26, 2026 nchini Morocco, ambapo mbali na ubingwa macho ya mashabiki yataelekezwa kwenye rekodi ambazo zinaweza kuandikwa ndani ya siku 21 za mashindano.
Rekodi nyingine zimekaa kwa zaidi ya miaka 20, nyingine zinaonekana kuwa hatarini kuvunjwa kutokana na ubora wa kizazi cha sasa cha wachezaji wa Afrika.
1. NIGERIA TAJI LA 11
Hakuna taifa lililotawala WAFCON kama Nigeria. Super Falcons tayari wamebeba mataji 10 ya mashindano hayo, zaidi ya mataifa yote yaliyowahi kushinda kwa pamoja. Wakifanikiwa kutwaa ubingwa Morocco, watafikisha mataji 11 na kuendelea kujiweka mbali zaidi katika historia ya soka la wanawake Afrika.
2. MOROCCO NA MKOSI WA FAINALI
Atlas Lionesses wamefika fainali mara mbili mfululizo mwaka 2022 na 2024, lakini wakashindwa kutwaa taji hilo mbele ya mabingwa wa muda wote, Nigeria na Afrika Kusini. Safari hii wanacheza kwenye ardhi ya nyumbani, mbele ya mashabiki wao. Swali sasa ni je kama wataandika historia kwa kutwaa ubingwa wao wa kwanza au wataendelea kuwa miongoni mwa timu zilizofika fainali nyingi bila kubeba kombe.
3. TWIGA STARS KUVUKA MAKUNDI
Tanzania inashiriki WAFCON kwa mara ya tatu, lakini haijawahi kuvuka hatua ya makundi, ilianza kushiriki mwaka 2010 na 2024, zote ilishindwa kuvuka. Ikiwa itaingia robo fainali mwaka huu, itakuwa historia kubwa zaidi kuwahi kuandikwa na Twiga Stars katika mashindano hayo.
4. REKODI YA PERPETUA
Kwa zaidi ya muongo mmoja hakuna aliyefanikiwa kumfikia Mnigeria Perpetua Nkwocha. Mshambuliaji huyo wa zamani alifunga mabao 34 katika historia ya WAFCON na mabao 11 katika mwaka moja 2010, bado ndiye mfungaji bora wa muda wote wa mashindano.
Kizazi cha sasa kinaongozwa na nyota kama Rasheedat Ajibade na Barbra Banda, Clara Luvanga, Opah Clement na wengineo wanaweza kuvunja rekodi hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.
5. WAFCON YA REKODI
Kwa mara ya kwanza tangu mashindano haya yaanzishwe mwaka 1998, timu 16 zitashiriki kuwania fainali hiyo badala ya 12. Hii ni rekodi mpya inayotarajiwa kuongeza ushindani na kutoa nafasi kwa mataifa mapya kuonyesha uwezo wao.
6. CAPE VERDE NA MALAWI
Cape Verde na Malawi zinaingia kwenye WAFCON kwa mara ya kwanza katika historia yao. Ushindi mmoja tu unaweza kuwasaidia kuandika rekodi kwa mataifa hayo, huku kufuzu robo fainali kukiwa moja ya maajabu makubwa yanayoweza kushuhudiwa mwaka huu.
7. AFRIKA KUSINI
Banyana Banyana walivunja utawala wa Nigeria mwaka 2022 kwa kutwaa ubingwa wao wa kwanza. Safari hii wana nafasi ya kuthibitisha kuwa hawakuwa mabingwa kwa msimu mmoja tu, bali wameingia rasmi kwenye orodha ya vigogo wa soka la wanawake Afrika.
Lakini ni kama kumezuka wasiwasi kwa baadhi ya mashabiki wa Afrika Kusini kwenye muenendo wake kwenye michuano hiyo ambayo hawajawa na muendelezo mzuri.
8. ZAMBIA KUBEBA UBINGWA
Zambia imekuwa moja ya timu zinazopewa sifa na kutabiriwa makubwa mwaka huu kutokana na nyota wake Barbra Banda na Racheal Kundananji wanaofanya vizuri. Hata hivyo, haijawahi kucheza fainali ya WAFCON. Ikiifikia mwaka huu itakuwa mafanikio makubwa zaidi katika historia ya taifa hilo.