Pogba, Monaco wakaribia kuvunja mkataba
Muktasari:
- Pogba, 32, alijiunga na Monaco msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kurejea katika soka la ushindani kufuatia kutumikia adhabu ya kusimamishwa kwa miezi 18 kutokana na kosa la kutumia dawa iliyopigwa marufuku.
MONACO, Ufaransa. Kiungo wa kimataifa wa Ufaransa na mshindi wa Kombe la Dunia 2018, Paul Pogba, yuko mbioni kuachana na klabu ya Monaco kabla ya mkataba wake kumalizika.
Pogba, 32, alijiunga na Monaco msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kurejea katika soka la ushindani kufuatia kutumikia adhabu ya kusimamishwa kwa miezi 18 kutokana na kosa la kutumia dawa iliyopigwa marufuku.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza Monaco uliathiriwa na majeraha, huku mabadiliko ya kocha yakiongeza sintofahamu kuhusu nafasi yake katika kikosi.
Kocha Filipe Luis alichukua nafasi ya Sebastien Pocognoli na mabadiliko hayo yanaonekana kuathiri nafasi ya Pogba, hasa katika eneo la kiungo ambalo ushindani wake umeongezeka.
Pogba awali alipewa adhabu ya kusimamishwa kucheza kwa miaka minne baada ya kukutwa na dawa iliyopigwa marufuku mwaka 2023. Hata hivyo, Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ilipunguza adhabu hiyo hadi miezi 18 na kumruhusu kurejea uwanjani Machi 2025.
Kwa sasa, Monaco haijatoa taarifa rasmi kuhusu uwezekano wa kuvunjwa kwa mkataba huo.
Hata hivyo, hali ya Pogba imeendelea kuwa tete baada ya kupata jeraha wakati wa mazoezi. Kiungo huyo sasa anasubiri kufanyiwa vipimo zaidi na timu ya madaktari iliyohusika na uchunguzi wake ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo.