LeBron na wenzake 76ERS wanatosha ubingwa NBA?
Muktasari:
- Hata hivyo, mafanikio hayatategemea majina makubwa, bali jinsi watakavyocheza kwa ushirikiano na kama kutakuwa na ubora wa kutosha kwa kila mmoja.
PHILADELPHIA, MAREKANI: KUWASILI kwa LeBron James katika timu ya Philadelphia 76ers akitokea Los Angeles Lakers kunakwenda kutengeneza kikosi kinachovutia macho kutokana na wingi wa wachezaji wenye vipaji.
Hata hivyo, mafanikio hayatategemea majina makubwa, bali jinsi watakavyocheza kwa ushirikiano na kama kutakuwa na ubora wa kutosha kwa kila mmoja.
Huu ni uchambuzi wa jinsi kikosi hicho kinavyoweza kuendana katika safari ya kusaka ubingwa wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) msimu ujao.
Huenda haikuonekana hivyo baada ya Philadelphia 76ers kufagiliwa na New York Knicks katika nusu fainali ya Kanda ya Mashariki, lakini ukweli ni kwamba ilikuwa karibu zaidi na ubingwa wa NBA kuliko timu nyingine nyingi msimu uliopita. Kwa hakika, ilikuwa mbele ya timu 22 katika mbio hizo.
Na sasa inaingia msimu wa 2026/27 ikiwa imeondokana na Paul George, Quentin Grimes, Kelly Oubre Jr na Andre Drummond, huku ikiwakaribisha LeBron James, Jaylen Brown, Dean Wade, Anfernee Simons, Kentavious Caldwell-Pope, Labaron Philon Jr pamoja na wengine.
Bila shaka, kikosi ambacho tayari kilikuwa na vipaji vingi kimeimarika zaidi. Lakini je, hilo linatosha kuifanya Philadelphia maarufu kama City of Brotherly Love kuanza kusherehekea ubingwa wake wa kwanza wa NBA tangu 1983?
SIXERS WANA NINI?
Kwa upande wa mastaa, Sixers wamejaza vipaji kupita kiasi. Ukiunganisha mafanikio ya kila mchezaji katika kikosi chao kinachotarajiwa kuanza, kabati la kuhifadhi mataji lingeonekana dogo. Mlinzi Tyrese Maxey ni mchezaji aliyeitwa mara mbili katika kikosi cha NBA All-Star, alichaguliwa katika kikosi cha tatu cha All-NBA 2026 na ndiye aliyeshinda tuzo ya ‘Most Improved Player’ 2024.
Mkali wa kutupia nyavuni Valdez Drexel Edgecombe Jr maarufu VJ Edgecombe, aliyechaguliwa wa tatu katika NBA Draft 2025 aliingia moja kwa moja kwenye Kikosi Bora cha Wachezaji Chipukizi (All-Rookie Team) na kumaliza wa tatu katika kura za tuzo ya Rookie of the Year.
Jaylen Brown, aliyesajiliwa kutoka Boston Celtics mapema Julai ana rekodi ya kuchaguliwa mara tano kwenye All-Star, mara mbili All-NBA na alimaliza ndani ya sita bora katika kura za MVP msimu uliopita. Pia, 2024 alitwaa tuzo za MVP wa Fainali za Kanda ya Mashariki na Fainali za NBA.
Kwa upande wa LeBron James, kinara wa muda wote wa NBA kwa michezo aliyocheza na pointi alizofunga, mafanikio yake ni mengi kiasi kwamba ni vigumu kuyaorodhesha yote. Katika msimu wake wa 23 rekodi katika historia ya NBA akiwa na Los Angeles Lakers tamu, akicheza michezo 60 na wastani wa pointi 20.9, ribaundi 6.1 na asisti 7.2 kwa kila mchezo.
Mchezaji wa nafasi ya ‘senta’ Joel Embiid ni All-Star wa mara saba, amechaguliwa mara tano katika kikosi cha kwanza au cha pili cha All-NBA, mara tatu kikosi cha pili cha walinzi bora wa NBA, mfungaji bora wa ligi mara mbili na ndiye MVP wa msimu wa 2022/23. Kwa ujumla, Sixers wana hazina kubwa ya mafanikio na ubora wa wachezaji. Timu hiyo iliyomaliza msimu uliopita ikiwa na rekodi ya ushindi 45 na kupoteza 37 ikishika nafasi ya saba Mashariki, hivi sasa ina uwezo wa kupambana uso kwa uso na timu yoyote kubwa NBA. Wanne kati ya watano wanaotarajiwa kuanza walimaliza ndani ya 35 bora kwenye kipimo cha ‘Offensive DRIP’, jambo linalotarajiwa kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo ilimaliza nafasi ya 17 msimu uliopita (kabla ya kuwasili kwa LeBron na Brown). Pia, Sixers wana benchi lenye nguvu, jambo ambalo siyo la kawaida kwa timu yenye mastaa wengi kiasi hicho.
Dean Wade ni mchezaji anayefanya kazi nyingi uwanjani; analinda vizuri, hutumia mashuti ya wazi na huunganisha vizuri mchezo wa mastaa wengine. Anfernee Simons ni mfungaji hatari mwenye uwezo wa kufikisha pointi 20 au zaidi katika usiku wowote. Msimu wa 2023/24 akiwa na Portland Trail Blazers, alikuwa na wastani wa pointi 22.6 kwa mchezo.
Kentavious Caldwell-Pope ni bingwa wa NBA mara mbili. Mataji hayo aliyapata kwa kuwa mchezaji hodari wa kulinda na kutupia mishuti ya pointi tatu (three-and-D player), ikiwemo alipocheza pamoja na LeBron 2020. Na sasa anatarajiwa kuwa kile ambacho Shane Battier alikuwa kwa LeBron wakati walipokuwa Miami Heat. Labaron Philon ni chaguo la raundi ya kwanza katika Draft ya 2026, akiwa na mtindo wa mchezo unaofanana kwa kiasi fulani na Simons.
Adem Bona na Ariel Hukporti, ambaye pia alisajiliwa kipindi hiki cha kiangazi, ni wachezaji wa ndani wasiokata tamaa, wanaopenda kudaka ribaundi, kulinda na kumalizia mashambulizi kwa ‘danki’. Jambo la kushangaza ni kwamba, huenda Tyrese Maxey ndiye mchezaji bora zaidi katika kikosi hicho, na sasa amezungukwa na mazingira bora zaidi ya kucheza.
Tangu James Harden alipoondoka, Maxey amekuwa akibeba mzigo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi. Katika misimu mitatu iliyopita amekuwa na wastani wa angalau pointi 25.9 kwa mchezo. Hata hivyo, licha ya uwezo wake mkubwa wa kufunga, ameonekana kubebeshwa jukumu kubwa kama mtengenezaji mkuu wa mashambulizi.
Baada ya kuwa na ‘True Shooting Percentage’ ya asilimia 61 alipocheza na Harden 2021/22, hajawahi tena kufikisha kiwango hicho katika misimu mitatu iliyofuata. Kwa asili, Maxey anafaa zaidi kucheza kwa kubadilishana majukumu ya kudaka na kutodaka mpira kuliko kuwa injini pekee ya mashambulizi.
Na sasa ana nafasi ya kucheza vizuri zaidi kupitia ushirikiano na Embiid katika ‘dribble handoff’, kutupia mashuti ya wazi ya pointi tatu wakati LeBron na Brown wanapovunja ulinzi kuelekea kikapuni, pamoja na kushirikiana na Simons au Edgecombe katika mipango mingine ya kushambulia. Kwa kifupi, mazingira ya sasa yanampa Maxey nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa wanagombea tuzo ya MVP.
SIXERS WANAKOSA NINI?
Katika Ligi ya Kikapu Marekani sasa, ili kushinda ubingwa unahitaji mambo matatu makubwa; vipaji, kina cha kikosi na wachezaji wanaoendana vizuri. Sixers tayari wana vipaji na kina cha kikosi kwa kiwango cha juu. Kwa upande wa Maxey, inaonekana pia amewekwa katika mazingira yanayomfaa. Lakini, kwa ujumla, namna vipande vingine vya kikosi vinavyoungana bado haijaridhisha.
Kwanza kabisa, karibu wote wanaotarajiwa kuanza ni wachezaji wanaotanguliza ushambuliaji kuliko ulinzi. Hakuna hata mmoja anayeshika nafasi ndani ya 75 bora kwenye kipimo cha Defensive DRIP. Edgecombe ndiye mwenye alama bora zaidi ya ulinzi (0.85), lakini ni vigumu kwa mlinzi mwenye urefu wa futi 6 na inchi 4 kubeba jukumu la kuongoza safu ya ulinzi peke yake.
Katika ushambuliaji, Brown na LeBron wanafanana sana. Wote hutegemea nguvu katika ulinzi na kujitengenezea nafasi au kuwatengenezea wenzao nafasi. Pia, hakuna anayejulikana sana kwa kutupia mipira nyavuni kwa ufanisi mashuti ya pointi tatu, kwani wote walikuwa chini ya asilimia 35 msimu uliopita.
Swali linabaki, kufanana huko kutapunguza kasi na mtiririko wa mashambulizi ya Sixers? Kwa upande wa Embiid, hata akiwa mzima siyo lazima awe senta anayemfaa zaidi LeBron na Brown. Embiid hupenda kucheza akianzia kwenye eneo la ‘elbow au post’, au kupitia ‘pick-and-pop’, wakati LeBron hufanya vizuri zaidi akiwa na senta anayekimbilia kikapuni (rim-running center), kama ilivyokuwa kwa Anthony Davis.
Kwa Embiid hupendelea mchezo wa ‘handoff’ akiwa na walinzi, lakini huo siyo mfumo ambao LeBron wala Brown huutumia sana. Kwa mtazamo wa juu juu, kikosi hicho cha kwanza kinakosa wale wachezaji wanaofanya kazi zisizoonekana lakini muhimu yaani wanaojitolea kwa ajili ya timu, wanaofanya uamuzi wa haraka, kudaka ribaundi na kubeba majukumu magumu ya ulinzi.
Edgecombe anaonekana kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufanya kazi hiyo, lakini ni mtu mmoja tu. Kwa historia, Wade na Caldwell-Pope pia wana sifa hizo, lakini ni vigumu kusema kama unaweza kuwaamini waanze au wamalize mechi badala ya mastaa wengine. Hii haimaanishi kwamba kipindi cha usajili cha Sixers kilikuwa kibaya.
Kwa kweli, timu yoyote ingeipenda nafasi ya kuwasajili wachezaji wa kiwango cha LeBron, Brown na wengine. Hakuna shaka kuwa usajili huo umeifanya Sixers kuwa timu bora zaidi kuliko ilivyokuwa. Lakini kikosi hicho kwa muundo wake wa sasa bado hakijaungana kikamilifu.
Na kama Sixers wanataka kumaliza ukame wa zaidi ya miaka 40 bila ubingwa wa NBA, bado wana masuala kadhaa muhimu ya kuyatatua kabla ya kuanza kufikiria kunyanyua taji.