Prime
Shalulile vs Mpanzu mziki upo hapa Ngao ya Jamii
MAISHA leo yatakuwa hivi, maofisini, vijiweni na hata mitaani kutakuwa na mikwara tofauti juu ya mchezo wa dabi ya Kariakoo utakaopigwa pale Uwanja wa Amani, Zanzibar kati ya watani wa jadi Yanga na Simba.
Timu hizo mbili zenye mashabiki wengi zaidi nchini zitakutana leo kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, utakaoanza saa 2:30 usiku kuamua kama Yanga itaendelea kushikilia taji hilo au kuliacha kwa Simba ambayo ina misimu miwili haijalibeba.
Gumzo kubwa sio mchezo huo ni makocha wa timu hizo wataamua kuingia na kikosi kipi baada ya kufanya uisajili mkubwa kwa kuingiza mastaa wa maana lakini wakiungana na wale ambao walisalia kutoka msimu uliopita.
Tuanze na Simba ambayo bado inaendelea na kocha Steve Barker, kocha huyu hatakuwa na kazi ngumu sana kutokana na msingi wa kikosi chake bado upo kutoka kile ambacho hakikupoteza dhidi ya Yanga msimu uliopita tangu aanze kuinoa timu hiyo.
UKUTA HUU
Simba ni wazi kwamba ukuta wake unaweza kuwa badiliko moja pekee ambapo golini hakuna shida atakuwa kipa Mamadou Kassali amecheza jumla ya dabi 2 rasmi za Kariakoo tangu ajiunge na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari 2026.
Huku beki wa kulia baada ya kuumia kwa nahodha Shomari Kapombe mkongwe ambaye amecheza dabi 25 na kufunga bao moja anaweza kuanza David Kameta Duchu (mechi 01), au Nathaniel Chilambo na mmoja akaanzia benchi.
Upande kushoto kijana Nickson Kibabage huyu akiwa mmoja kati ya wachezaji wenye uzoefu na michezo hii, ataanza huku mabeki wa kati wakiendelea watu wa kazi wawili Rushine De Reuck na Ismael Toure ambao tangu waanze kucheza pamoja hawajapoteza hata mechi moja dhidi ya Yanga.
VIUNGO NI HAWA HAPA
Barker anaweza tena kuwa badiliko moja tu eneo la kiungo ambapo kiungo wa chini hakuna shaka Yusuf Kagoma ataanza huku Kelvin Nashon akisubiri lakini kama kocha huyo ataamua kuwa katili anaweza kuwatumia wote wawili endapo atahitaji sana kazi ya kukaba.
Juu ya Kagoma Barker anaweza kumpa nafasi Ibrahim Jabaar, ambaye alikuwa naye kule Stellenbosch ya Afrika Kusini wakati viungo wa pembeni wanaweza kuanza Lebase Gueye ambaye kama atatoka baadaye tunaweza kumuona winga mpya Keletso Makgalwa.
Keletso kama ataanza au hata kuingia Yanga itatakiwa kuwa makini kutokana na kasi yake lakini pia ujuzi wake wa kupiga pasi za mwisho ambapo kama yatafanyika makosa ya kumsahau au kushindwa kumdhibiti kwenye mbio zake na hata chenga basi anaweza kama sio kufunga basi kusababisha madhara. Winga mwingine anaweza kuanza Anicet Oura ambaye naye ana kasi.
Huku kiungo wa juu nyuma ya mshambuliaji wa kati hakuna mwingine zaidi ya Clatous Chama ambaye amecheza jumla ya dabi 21 na mabao manne rasmi za Kariakoo tangu atue nchini Tanzania atapewa jukumu hilo la kutengeneza pasi za mwisho.
Barker anaweza kuanza na mshambuliaji Ellie Mpanzu ambaye amecheza jumla ya dabi nne rasmi za Kariakoo tangu ajiunge na klabu ya Simba akifunga bao na asisti moja.
Akiwa na maelewano mazuri na Chama, kumbuka wawili hao kwenye mchezo wa mwisho wa ligi baina ya timu hizo walifanya balaa kubwa kwenye mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kama Mpanzu atachoka basi tunaweza kumuona mshambuliaji mpya Ibrahim Doumbia akipewa nafasi au kama kocha huyo atataka kucheza na wote wawili kwenye kutafuta mabao zaidi lakini pia akiwa na mastaa wa kutosha kwenye benchi ambao wanaweza kuja kubadilisha mchezo.
Kwenye benchi Simba watakuwa na Hussein Abel, Nashon, Neo Maema, Inno Loemba, Doumbia,Morice Abraham, Antony Mligo, ChilamboVedastus Masinde.
Yanga yenyewe ina mtihani wa maamuzi ambapo ikiwa chini ya kocha mpya Mngqithi itakuwa na kazi ya kuamua kwenye kikosi chake itakwenda na mziki gani ili itetee taji hilo ambalo waliitwa msimu uliopita kwa kuwafunga wekundu haohao.
UKUTA ULEULE
Yanga haionyeshi kirahisi kama inaweza kufanya mabadiliko kwenye ukuta wake ambapo beki wa kulia ataanza Yao Akouassi, ambaye ana kasi na utulivu wa kukaba, kule kushoto akiwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, huku mabeki wa kati wakiwa Ibrahim Abdulla ‘Bacca’ na nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto.
Licha ya Manqoba kumleta beki mpya Farouk Koumara, raia huyo wa Ivory Coast anaweza kupumzishwa kutokana na makosa ambayo aliyafanya kwenye mchezo wa Wiki ya Mwananchi aliposhindwa kuokoa na mpira kunaswa kutoka kwenye umiliki wake wakati Aigles Du Congo wakipata bao la kwanza.
VIUNGO WATANO, MPYA MMOJA
Manqoba anaweza kuanza na viungo watano wakiwemo wawili Mohammed Damaro pale chini lakini hana uzoefu na mechi hizo kwani amecheza mara moja.
Huku pembeni yake kidogo Duke Abuya ambaye ana uzoefu akiwa amecheza dabi nne tangu atue Yanga, akipata nafasi ya kuwa na jukumu la kusaidia kukaba na kupandisha mashambulizi.
Kwa viungo washambuliaji kutoka pembeni anaweza kuanza Maxi Nzengeli kulia ambaye pia atakuwa na kazi ya kusaidia kukaba kati wakati Yanga imepoteza mpira, ukiachana na ubora wake ana uzoefu na dabi akiwa amecheza jumla ya dabi nane na kufunga mabao matatu.
Kule kushoto winga Houssein Zakouani akianza kutokana na kasi yake na akili ya kupenya, ingawa hana rekodi ya kucheza mechi yoyote na Yanga kwani ndio ametua dirisha dogo.
Allan Okello, anaweza kuanza kama kiungo namba kumi akiwa na kazi maalum ya kupiga pasi za mwisho kwenda kwa mshambuliaji, lakini sio hivyo tu, amecheza jumla ya dabi tatu rasmi za Kariakoo (dhidi ya Simba) tangu ajiunge na Yanga SC wakati wa dirisha dogo la usajili la mwezi Januari 2026.
Mshambuliaji Peter Shalulile ambaye ametua dirisha hili la usajili akitokea Mamelod Sundowns ana uhakika mkubwa wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, akiwa hajawahi kucheza dabi hata moja.
Shalulile atakuwa na kazi kubwa kwani atakutana na mabeki wa Simba Rushine na Toure ambao wanajuana vizuri, wote wakiwahi kukutana Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambapo akiwahi kucheza sambamba na Rushine huko Mamelodi.
Kwa upande wa Cheikh Toure na Selemani Mwalimu wanaweza akaanzia benchi kutokana na hesabu za kocha ingawa wote ni mastaa wapya wa kikosi hicho.
Manqoba ana benchi pana kwani ataamua kuwapa nafasi mastaa wapi ambao wana nguvu ya kuja kumbadilishia mchezo wakiongozwa na kipa Aboutwalib Mshery, Kouamara, Chadrack Boka,Kangwanda,Mudathir Yahya, Edmund John, Ngoma na Toure.
MAKOCHA WANAJUANA
Kocha Steven Barker alikuwa akiifundisha Stellenbosch FC na Amazulu FC, huku Manqoba Mngqithi akiinoa Mamelodi Sundowns wote hawa walikuwa wapinzani ligi ya Sauzi hivyo unaweza kusema wanajuana.
Rekodi zinaonyesha kuwa wakati wakiwa Sauzi walikutana mara tisa huku Barker akishinda mara tano na Manqoba akichomoa kwenye mechi nne, hawajawahi kutoka sare wanapokutana ni lazima mmoja afe na mwingine apone. Swali ni je? wataendeleza historia hiyo.