Depay aituhumu Corinthians kuvunja makubaliano
Muktasari:
- Corinthians imethibitisha kuwa haitamuongezea mkataba Depay, mwenye umri wa miaka 32, ikisema uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kulinda “hali ya kifedha” ya klabu.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Memphis Depay, ameukosoa uamuzi wa Corinthians wa kutomwongezea mkataba, akidai klabu hiyo ya Brazil imekiuka makubaliano waliyofikia ya kuongeza mkataba wake kwa miaka miwili.
Corinthians imethibitisha kuwa haitamuongezea mkataba Depay, mwenye umri wa miaka 32, ikisema uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kulinda “hali ya kifedha” ya klabu.
Hata hivyo, Depay amesema tayari walikuwa wamefikia makubaliano ya kuongeza mkataba wake kwa miaka miwili, huku akidai mpango huo ulikuwa umepitishwa na rais wa klabu pamoja na idara za michezo, sheria na fedha.
Kutokana na hali hiyo, nyota huyo wa Uholanzi ameishutumu Corinthians kwa kile alichokiita “tabia isiyokubalika” na kutishia kuchukua hatua ili kulinda maslahi yake.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, Depay alisema:
“Nimekatishwa tamaa kusoma kwamba Corinthians imeamua kutoheshimu makubaliano tuliyokuwa tumefikia ya kuongeza mkataba wangu kwa miaka miwili zaidi.
“Makubaliano hayo yalikuwa yamepitishwa wazi na rais pamoja na idara za michezo, sheria na fedha.
“Hata hivyo, baadhi ya watu wameamua kukiuka makubaliano hayo.
“Sikutaka hali hii itokee na wakati wote nimeiheshimu klabu katika mchakato huu, lakini sasa ninalazimika kuchukua hatua kali ili kulinda maslahi yangu.
“Katika siku zijazo nitaeleza hadharani kuhusu suala hili, lakini msione shaka kwamba sitaruhusu tabia hii isiyokubalika ipite bila kuchukua hatua.”
Kauli hiyo inaashiria kuwa safari ya Depay katika klabu hiyo yenye maskani yake São Paulo inaweza kuwa inafikia mwisho baada ya kuitumikia kwa takribani miaka miwili.
Depay alijiunga na Corinthians baada ya kuondoka Ulaya, akitarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa kikosi hicho. Hata hivyo, mustakabali wake sasa umeingia shakani kutokana na mvutano huo kuhusu mkataba wake.