Dabi za Kariakoo na Mashemeji ni zaidi ya dakika 90
Muktasari:
- Nchini Tanzania ni Dabi ya Kariakoo inayowakutanisha Simba na Yanga ambazo zinacheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex leo, huku nchini Kenya kukiwa na Dabi ya Mashemeji kati ya Gor Mahia na AFC Leopards.
AFRIKA Mashariki ina dabi mbili zinazotajwa miongoni mwa zenye mvuto mkubwa zaidi barani Afrika.
Nchini Tanzania ni Dabi ya Kariakoo inayowakutanisha Simba na Yanga ambazo zinacheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex leo, huku nchini Kenya kukiwa na Dabi ya Mashemeji kati ya Gor Mahia na AFC Leopards.
Ingawa zote zimejengwa juu ya ushindani wa muda mrefu, kila moja imebeba historia, utamaduni na utambulisho wake, hali inayozifanya kuwa zaidi ya mechi za dakika 90.
Kwa Tanzania, Kariakoo Derby ni pambano kati ya Yanga na Simba, klabu mbili kongwe na zenye mashabiki wengi zaidi nchini Tanzania.
Dabi hiyo imepewa jina la “Kariakoo Derby” kutokana na historia ya timu hizo kuasisiwa na kukulia katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, ambalo kwa miaka mingi lilikuwa kitovu cha maendeleo ya soka nchini ingawa kwa miaka mingi haichezwi Kariakoo.
Historia ya watani hawa inaanza kabla ya Tanzania kupata uhuru. Yanga ndiyo klabu kongwe zaidi, iliyoanzishwa mwaka 1935 kwa jina la New Young, kabla ya baadaye kubadili jina na kuitwa Yanga. Mwaka mmoja baadaye, mwaka 1936, baadhi ya wanachama wa Yanga walijitenga kutokana na tofauti za kiuongozi na kuanzisha klabu mpya iliyoitwa Queens. Klabu hiyo ilibadilisha majina mara kadhaa, ikiitwa Eagles na baadaye Sunderland, kabla ya mwaka 1971 kubadili jina rasmi na kuwa Simba.
Kutokana na historia hiyo, ushindani wa Simba na Yanga haukuanzia uwanjani pekee, bali ulitokana na mgawanyiko wa kihistoria ndani ya klabu moja.
Hilo ndilo linaloifanya Kariakoo Derby kuwa mojawapo ya dabi zenye historia ndefu na ushindani wa kipekee barani Afrika.
Umaarufu wa dabi hiyo unatokana na sababu kadhaa. Inawakutanisha klabu mbili zilizotwaa mataji mengi zaidi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ina mashabiki wengi kuliko klabu nyingine yoyote nchini, na mara nyingi matokeo yake huamua mbio za ubingwa au nafasi za kushiriki mashindano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Aidha, ndiyo mchezo unaoingiza mapato makubwa zaidi kupitia mauzo ya tiketi, udhamini, matangazo na haki za urushaji wa televisheni. Kwa mujibu wa takwimu za kihistoria, watani hao walikutana kwa mara ya kwanza katika ligi mwaka 1965, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sunderland, ambayo baadaye ilikuja kuwa Simba.
Rekodi ya ushindi mkubwa zaidi katika historia ya Kariakoo Derby bado inashikiliwa na Simba baada ya kuichapa Yanga mabao 6-0 mwaka 1977.
Kwa zaidi ya miaka 90, tangu kuanzishwa kwa Yanga na karibu miaka 60 ya Kariakoo Derby katika mfumo wa ligi, pambano hili limeendelea kuwa sehemu muhimu ya historia na utamaduni wa soka la Tanzania. Leo, Kariakoo Derby si mchezo wa kawaida bali ni tukio linalounganisha historia, ushindani, uchumi na mapenzi ya mamilioni ya mashabiki, na limejijengea hadhi ya kuwa miongoni mwa dabi kubwa na maarufu zaidi barani Afrika.
Leo ni mchezo wa ufunguzi wa ligi yaani Ngao ya Jamii unaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, huu ni kati ya michezo ambayo inaonyesha mvutano, ubora na umuhimu wa dabi hii.
MASHEMEJI DERBY
Wakati Tanzania ikijivunia Dabi ya Kariakoo, Kenya nayo ina Dabi ya Mashemeji, pambano linalozikutanisha Gor Mahia na AFC Leopards.
Ushindani huo ulianza mwaka 1968 wakati Gor Mahia ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Abaluhya United, ambayo baadaye ilibadilika na kuwa AFC Leopards. Tofauti na Kariakoo Derby ambayo jina lake limetokana na eneo la kijiografia, Dabi ya Mashemeji imejengwa zaidi kwenye uhusiano wa kijamii na kitamaduni.
Gor Mahia kwa miaka mingi imekuwa ikihusishwa na jamii ya Waluo, huku AFC Leopards ikitambulika zaidi na jamii ya Waluhya.
Hata hivyo, ukuaji wa soka la Kenya umeifanya dabi hiyo kuwa mali ya taifa zima, ikipewa jina la “Mashemeji” kutokana na ushindani wenye ukaribu wa kijamii uliotafsiriwa na vyombo vya habari.
UTOFAUTI WA DABI
Licha ya kufanana kwa ukubwa wa ushindani, dabi hizi mbili zina utofauti wa kipekee.
Kariakoo Derby imekuwa ikijitofautisha kwa kiwango kikubwa cha uwekezaji wa klabu, ushawishi wa kibiashara, ubora wa vikosi, idadi ya mashabiki na uwakilishi wa mara kwa mara katika mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kwa miaka ya hivi karibuni, Simba na Yanga zimekuwa miongoni mwa klabu zenye mafanikio makubwa zaidi Afrika Mashariki katika michuano ya kimataifa, jambo lililoiongezea hadhi dabi hiyo. Kwa nini Gor Mahia na AFC Leopards zinaitwa “Mashemeji Derby”? Mashemeji Derby ni moja ya mechi zenye historia kubwa na ushindani mkali zaidi katika soka la Afrika Mashariki.
Jina hilo linatokana na asili ya timu hizo mbili, ambazo zinawakilisha jamii mbili kubwa za Kenya zenye uhusiano wa kijamii na kifamilia.
Gor Mahia ni klabu iliyoanzishwa mwaka 1968 baada ya kuunganishwa kwa timu mbili za jamii ya Wajaluo, Luo Union na Luo Sports Club. Jina Gor Mahia limetokana na jina la mganga maarufu wa Wajaluo aliyeitwa Gor wuod Ogada Nyakwar Ogalo, ambaye aliaminika kuwa na nguvu za kipekee za kiroho na ushawishi mkubwa katika jamii yake. Katika lugha ya Dholuo, Mahia humaanisha uchawi au uganga, hivyo Gor Mahia humaanisha “uganga wa Gor” au “nguvu za Gor.”
Kutokana na jina la babu huyo, mashabiki wa Gor Mahia pia hujulikana kwa jina la utani K’Ogalo, likimaanisha wazawa au wajukuu wa Ogalo. Kwa upande mwingine, AFC Leopards ni kifupi cha Abaluhya Football Club Leopards.
Neno Abaluhya katika lugha ya Kiluhya linamaanisha Waluhya, hivyo klabu hiyo ilianzishwa kuwakilisha jamii ya Waluhya nchini Kenya.
Uhusiano wa kihistoria na kijamii kati ya Wajaluo na Waluhya, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakioana na kuunda undugu wa kifamilia, ndio uliozaa jina la “Mashemeji Derby.”