Prime
Mkopo wa Mwalimu Simba uliisha kabla ya kuisha
WASWAHILI wanasema haiishi mpaka iishe wakimaanisha kuwa mtu hatakiwi kujihakikishia kuwa ameshindwa au amefanikiwa mpaka afike mwisho wa jambo alilokuwa analifuatilia au anataka kulipata.
Kitendo cha kujihakikishia kuwa umeshafanikiwa na pengine kutangaza kuwa umeshalifanikisha kabla halijafikia mwisho kunaweza kukufedhehesha iwapo mambo yatabadilika. Ndivyo inavyoonekana ilitokea kwenye sakata la mshambuliaji wa Wydad Casablanca, Selemani Mwalimu ambaye alfajiri ya Jumanne, Agosti 11, alitambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Yanga baada ya mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara kufikia makubaliano na vigogo hao wa Morocco.
Ni vigumu kuamini kilichotokea kwa kuwa viongozi wa Simba walimtambulisha Mwalimu Jumamosi wakati wa tamasha la Siku ya Simba, ambalo hutumika kutambulisha wachezaji kwa ajili ya msimu unaofuata.
Ingawa hawakuwepo, runinga kubwa iliyosimikwa uwanjani ilitumika kumuonyesha mchezaji huyo akitoa ujumbe wa kuwatuliza mashabiki na wanachama wa Simba kuwa ni mchezaji halali wa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi na atakuwa nayo msimu mpya wa 2027-28 unaoanza wiki hii.
Na kushindilia zaidi hilo, Mwalimu alisharipoti kambini Simba Jumatatu kisiwani Unguja akitokea Casablanca kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi ya Ngao ya Jamii inayochezwa Jumatano, Agosti 12, ikikutanisha vigogo hao wa soka nchini.
Na Jumatatu akafanya mazoezi na timu hiyo iliyosaka ubingwa kwa misimu mitano bila ya mafanikio na inataka kukomesha ubabe wa watani wake wa jadi waliotamba kwa misimu hiyo mitano kuanzia mwaka huu.
Taarifa zinasema sinema ilitokea usiku wa Jumatatu wakati mchezaji huyo wa zamani wa Alliance alipofuatwa na kutakiwa kupanda ndege ya mwisho ya kwenda Dar es salaam kwa ajili ya kusaini mkataba wa mkopo wa kuichezea Yanga.
Habari zinasema pamoja na kumtambulisha, viongozi wa Simba walishindwa kukamilisha suala la malipo mapema wakati mambo yalikwenda kasi sana Casablanca ambako rais wa klabu aliyekuwepo wakati Mwalimu akitolewa kwa mkopo kwenda Simba, aliondoka madarakanI akiacha dau la Dola 50,000 ili mchezaji huyo asaini mkataba mwingine wa mkopo wa kuendelea kuitumikia Simba.
Hata hivyo, inaripotiwa kuwa rais mpya wa Wydad alipandisha dau hadi Dola 150,000 (takriban Sh400 milioni) na kuwakabidhi mkataba wa mkopo. Hata hivyo, suala hilo halikukamilishwa mapema wakati klabu nyingine zikionyesha kutaka huduma yake hadi Yanga walipofika na kupandisha dau na hivyo kuruhusiwa kumchukua kwa mkopo.
Vipengele vya mkataba wake wa mkopo bado havijawekwa bayana kama Yanga itapewa fursa ya kumnunua mwishoni mwa mkopo au atalazimika kurejea Wydad baada ya kupata fursa ya kucheza kikosi cha kwanza na kukomaa kimchezo na kiushindani.
Huyu anakuwa mchezaji wa tano wa Simba kuibukia Yanga ndani ya msimu mitano ambayo Yanga imetawala soka la Tanzania Bara. Ilianza na Jonas Mkude, baadaye ikamchukua Jean Baleke kabla ya kuinasa saini ya Cloutus Chama na baadaye beki imara wa kushoto, Mohamed Hussein.
Ingawa wote wana umri mkubwa, Yanga inaonekana ama inacheza na akili za Simba kwa kuitikisa kila msimu unapokaribia kuanza au inataka kunufaika na uzoefu wao kama ambavyo Mkude aliishika timu nyakati muhimu ambazo chaguo la kwanza lilikosekana.
Kwa wakati wote huo, Simba imekuwa ikiripotiwa kuwa ilihitaji huduma ya wachezaji kadhaa muhimu, lakini ikaishia njiani ama kwa kushindwa kufikia dau lililowekwa ama kuzidiwa kete.
Khalid Aucho, Stephanie Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Bakari Mwamnyeto na sasa Peter Shelulile ni baadhi ya wachezaji ambao Simba ilihusishwa nao kabla ya mipango kusambaratika kwa sababu moja au nyingine. Na hili la Selemani Mwalimu limekuwa kubwa zaidi kwa kuwa alishaichezea Simba kwa mkopo kwa msimu mmoja na jitihada za kumuongezea mkataba zimekwama wakati akiwa kambini Zanzibar.
Hili limekuwa kubwa zaidi na linaweza kuwa linatoa picha ya tatizo kubwa la Simba wakati wa usajili. Inaonekana propaganda zinawekwa mbele zaidi kabla ya kukamilisha jambo lao muhimu.
Wakati Yanga walisita kumtangaza namba sita mpya kabla na siku ya tamasha lao pengine kwa sababu ya zuio la Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) ama kutokamilika kwa ununuzi, Simba walishajihakikishia kuwa wamemaliza suala la Mwalimu hadi kufikia kumtangaza.
Hili ni kosa kubwa kwa mchezaji mwenye soko na ambaye bado yupo chini ya umiliki wa klabu yake. Isingekuwa tatizo kama Simba wasingemtambulisha Mwalimu na kusubiri kwanza kukamilisha mkataba wa mkopo wake. Lakini, kisiasa, si vizuri kumkosa mchezaji ambaye umeshakubaliwa kila kitu na yupo kambini kwako halafu unasikia amekwenda klabu nyingine kwa sababu ya kasoro ndogo katika utekelezaji wa makubaliano.
Kama kwa Mwalimu hali ni hii, Simba inawakosa wachezaji wangapi inaowataka ambao hawajajulikana kwa staili kama hii? Ni dhahiri kwamba kwa uongozi wa Hersi Said na wenzake, haikuwa imeisha hadi walipoona wamemnasa.
Uongozi wa Yanga ungeweza kukurupuka kumtuma ofisa habari wake, Ali Kamwe atangaze kuhusu uwezekano wa kumpata Mwalimu kabla ya mambo kuwa sawa. Lakini, Kamwe akaamua kutumia fasihi katika hilo aliposema “wana mchezaji wetu wanafanya naye mazoezi†, akionekana kuwa alishadokezwa kuhusu mipango ya kumpata na kwamba wanachosubiri ni Simba kuanzia mguu mbaya ndipo wakamilishe.
Kwa vyovyote vile kwa Simba, suala la Selemani Mwalimu liliisha kabla halijaisha na hili ni fundisho kwa viongozi kuwa usajili si siasa wala propaganda, ni kupigana hadi dakika ya mwisho.