Palace yamtumia mchumba kumvuta staa
Muktasari:
- Uhamisho wa McNeil kwenda Selhurst Park ulithibitishwa jana Jumanne asubuhi, baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kufanyiwa vipimo vya afya siku moja kabla.
LONDON, ENGLAND: CRYSTAL Palace inadaiwa kufanya mazungumzo na Megan Sharpley ambaye ni mchumba wa mshambuliaji Dwight McNeil, kabla ya kukamilisha usajili wa nyota huyo kutoka Everton katika dili lisilo la kawaida la kubadilishana wachezaji moja kwa moja.
Uhamisho wa McNeil kwenda Selhurst Park ulithibitishwa jana Jumanne asubuhi, baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kufanyiwa vipimo vya afya siku moja kabla.
McNeil anakwenda Palace kwa kubadilishana na Brennan Johnson, ambaye alijiunga na klabu hiyo kwa ada ya rekodi ya klabu miezi saba iliyopita. Dili hilo limefanyika kwa kubadilishana wachezaji moja kwa moja bila klabu yoyote kulipa ada ya uhamisho, jambo ambalo siyo la kawaida katika soka la kisasa.
Kwa mujibu wa The Times, mwenyekiti wa Palace, Steve Parish, alimtafuta Sharpley kwa ajili ya mazungumzo ya kuweka mambo sawa baada ya uhamisho wa McNeil kwenda Palace kushindikana Februari, mwaka huu.
McNeil alikuwa anatarajiwa kujiunga na Palace siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo, akilenga kuchukua nafasi ya Jean-Philippe Mateta, ambaye wakati huo alitarajiwa kuhamia AC Milan. Hata hivyo, baada ya Mateta kushindwa vipimo vya afya, Palace ilisitisha nia ya kumsajili McNeil. Klabu hiyo iliwasilisha nyaraka za dili hilo Ligi Kuu England, hatua iliyoipa muda wa ziada kukamilisha uhamisho huo, lakini baadaye ikaamua kujiondoa katika dakika za mwisho.
Uamuzi huo ulimkasirisha Sharpley, ambaye kupitia Instagram alisema Palace ilikuwa imekaa kimya na kwamba hali hiyo ilikuwa imeathiri afya ya akili ya McNeil. Aliandika: “Usiku wa leo na siku 48 zilizopita, imenivunja moyo kuona namna ambavyo ulimwengu wa soka unaoupenda sana unaweza kuwa mkatili kwako. Tunaishi katika dunia ambayo kila mtu anafahamu ukubwa wa tatizo la afya ya akili.
“Kwa hiyo, katika soka, kwa nini tunaona ni jambo linalokubalika kwa sababu vijana hawa wanapata fedha nyingi, hivyo ni sawa kuchezea na kuvuruga afya yao ya akili, kana kwamba hiyo ni sehemu tu ya kazi?”
Miezi sita baada ya uhamisho wake wa kwanza kushindikana, McNeil hatimaye amejiunga na Palace akiwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na klabu hiyo katika dirisha hili la majira ya kiangazi.