Kocha Nigeria ajibebesha zigo WAFCON
Muktasari:
- Kocha huyo alisema anaelewa maumivu waliyonayo mashabiki wa Super Falcons na alaumiwe yeye na si wachezaji akiwakingia kifua walipambana dakika zote 90.
KOCHA Mkuu wa Nigeria, Justin Madugu amesema atabeba lawama zote baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Cameroon kwenye robo fainali ya fainali za Wafcon zinazoendelea Morocco.
Kocha huyo alisema anaelewa maumivu waliyonayo mashabiki wa Super Falcons na alaumiwe yeye na si wachezaji akiwakingia kifua walipambana dakika zote 90.
Madugu alisema kama wangeshinda mchezo huo wangefuzu moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia hivyo watatumia nafasi ya mchujo ili kutetea nafasi ya kucheza michuano mikubwa ya dunia.
Iko hivi, Nigeria na Afrika Kusini ambazo zilitolewa robo fainali, bado zina nafasi kupitia mchujo wa CAF na zitakutana katika mechi ya play in na mshindi atasonga mbele katika mchujo wa mabara.
"Wasichana walifanya kila walichoweza, lakini ndivyo mchezo ulivyokwenda. Tunaomba radhi na ninachukua jukumu hilo. Bado tuna nafasi ya pili na tutafanya kila tuwezalo,” alisema.
Kocha huyo amekanusha taarifa za kupoteza mchezo huo kulisababishwa na migogoro na mgawanyiko katika kikosi hicho, baada ya tukio la Esther Okoronkwo kushindwa kumpasia Asisat Oshoala aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kufunga.
Kocha huyo alisema uamuzi wa Okoronkwo haupaswi kutafsiriwa kama dalili ya migogoro kambini, akisisitiza wachezaji wote bado wana mshikamano.
“Kwa kadiri ninavyojua, hakuna tatizo kambini. Hakuna makundi kwa wasichana. Wote wako pamoja nina uhakika Esther alihisi angeweza kufunga, ndiyo maana alijaribu. Hilo halimaanishi kuna mgawanyiko katika timu,” alisema Madugu.
“Katika mechi zote walizocheza, hawakuwahi kutengeneza nafasi za aina ile walizotengeneza leo (Jumapili iliyopita), lakini tatizo ni hatukuzitumia vizuri. Hatukuwa sahihi na makini katika umaliziaji,” alisema.
Nigeria ambao ni mabingwa watetetzi wa michuano hiyo mwaka huu wamejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuanza vibaya na ilipokea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Malawi katika mechi ya kundi C, kisha ikashinda bao 1-0 dhidi ya Zambia kabla ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Misri na kumaliza ya pili.
Nigeria ndiyo taifa lililoandika historia ya kuwa mwenyeji wa kwanza wa mashindano hayo mwaka 1991, katika mashindano ya kwanza yaliyojulikana kama African Women’s Championship na ndiyo ilikuwa ya kwanza kubeba taji hilo la kihistoria. Tangu hapo imebeba mataji 10 kati ya 13 na kuwa moja ya mataifa yenye rekodi nzuri Wafcon.