Afrika Kusini katika mtego wa Super Falcons WAFCON
Muktasari:
- Afrika Kusini ilitolewa hatua ya robo fainali baada ya kupokea kichapo cha bao 2-1 dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.
KOCHA wa Banyana Banyana ya Afrika Kusini, Desiree Ellis amesema wana kibarua kigumu cha kukutana na Nigeria katika mchujo wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake.
Afrika Kusini ilitolewa hatua ya robo fainali baada ya kupokea kichapo cha bao 2-1 dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.
Timu hizo sasa zitakutana katika mechi ya play-in itakayopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Moulay Rachid, Casablanca na mshindi atasonga mbele kwenye hatua ya mchujo wa mabara na kuendelea kuwa na matumaini ya kushiriki Kombe la Dunia 2027, Brazil.
Ellis licha ya ugumu watakaokutana nao dhidi ya Nigeria, lakini hawako tayari kupoteza nafasi hiyo ya mwisho ya kutetea nafasi ya kucheza Kombe la Dunia.
“Bado hatujatolewa, hatukutaka kupitia njia hii, lakini sasa tumelazimishwa kuipitia. Tunahitaji kujiandaa kwa mechi inayofuata kiakili na kimwili na tunahitaji kupona haraka,” alisema Ellis.
Kocha huyo alisema anafahamu changamoto inayowakabili kutokana na kukutana na Nigeria, timu yenye historia kubwa katika soka la wanawake Afrika.
Mshindi wa mchezo huo atasonga kwenye mchujo wa mabara yote utakaozikutanisha timu 10, kati ya hizo timu tatu tu zitakazofanya vizuri ndizo zitakata tiketi ya Kombe la Dunia.